SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi ipo mbioni kuanza ujenzi wa vituo vya dharura vya zimamoto katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kukabiliana na majanga ya Moto yanapotokea.
Hayo yamebainishwa na Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Goodluck Zelote, ambaye pia ni Mkuu wa kitengo cha oparesheni za kuzima moto kutoka makao makuu ya Jeshi hilo akiwa Wilayani Same kufuatilia suala la upatikanaji wa viwanja kwaajili ya ujenzi wa vituo hivyo, lakini pia kufuatilia upatikanaji na usimikaji wa vifaa vya visima vya maji vya dharura vya Zimamoto.
Aidha Naibu Kamishna Zelote amesema kuwa Jeshi hilo linatarajia kuwa na mradi mkubwa ambao utaleta magari mengi ya kuzimamoto kila Wilaya Nchi nzima hivyo ziara hiyo ni shemu pia ya maandalizi ya kupokea mradi huo kuhakikisha kwamba huduma ya kuzimamoto na uokoaji inapatikana kwa ufanisi zaidi.
“Nipo katika ziara ya Mikoa mitano na leo hii nimefika kuonana na mkuu wa wilaya ya Same, hapa kufuatilia suala la upatikanaji wa viwanja kwaajili ya ujenzi wa vituo vya Zimamoto, tunajiandaa kuhakikisha tunakuwa na visima vya Zimamoto vya kutosha katika Wilaya zetu zote ndani ya Tanzania na kuhakikisha kwamba mahitaji mengine wezeshi kama maeneo ya kujenga vituo yanakuwepo”. Alisema Naibu Kamishna Zelote.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Kasilda Mgeni amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuona umuhimu kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa na vifaa kwa Wilaya zote Nchi nzima, kwa upande wa Same itakuwa ni mkombozi kwa sababu ni Wilaya kubwa kuliko Wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro inachukua asilimia 40 ya Mkoa wa Kilimanjaro na ipo mbali zaidi na makao makuu ya Mkoa huo.
“Mradi huu wa vifaa ikiwemo Magari kwa kweli nimefurahishwa sana na nimpongeze Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani, kwa kipindi cha mwishoni mwa mwaka jana 2023 na mwanzoni mwa mwaka huu 2024 Wilaya ya Same tumepata mafuriko kwa kiwango kikubwa kufuatia mvua kubwa zilizonyesha, tuliona adha ambayo ilikuwepo” Alisema Kasilda.
Na kuongeza “Zimamoto Ofisi Same ipo na wapo maaskari lakini hawana vifaa jambo ambalo linawapa wakati mgumu kwenye utendaji wao wa kazi, lakini kwa mpango huu itasaidia kufanya kazi kwa ufanisi na kuweza kuokoa mali na maisha ya watu yanapotokea majanga mbalimbali”.
Pia Kasilda ameomba endapo vifaa hivyo ikatokea vinakuja kwa awamu basi hiyo awamu ya kwanza waiangalie kwa jicho la kipekee sana Wilaya ya Same kutokana na jiografia yake ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya Zimamoto na Uokoaji.