Dk Mwigulu aonya taasisi za ununuzi kukimbilia bidhaa za nje

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amezitaka taasisi na mashirika ya umma yanayotekeleza miradi ya maendeleo kuacha utaratibu wa kununua malighafi nje ya nchi, bali watumie zinazozalishwa nchini ili kukuza uchumi na ajira kwa Watanzania.

Pia, amezitaka kuacha mazoea ya kwamba samani za ofisi zinazotoka nje ya nchi ndizo bora, badala yake wahakikishe wananunua zinazozalishwa na viwanda vya ndani.

Dk Mwigulu amesema kama kuna anayetaka kununua samani kutoka nje ya nchi, afanye hivyo kwa fedha zake na kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwake.

Amesema hayo leo Jumamosi Septemba 28, 2024 alipopokea ripoti ya utendaji kazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka 2023/24.

Waziri huyo amesema kununua bidhaa zinazozalishwa nchini, kunatengeneza fursa za ajira na kujenga uchumi wa ndani.

Kwa mara kadhaa Serikali imekuwa ikisisitiza kuwekwa kipaumbele kwa bidhaa za ndani kutumika kwenye miradi ili kuimarisha uchumi wa ndani.

“Waambieni watumie malighafi zinazozalisha nchini nyaraka zile zinaletwa kwenu (PPRA), wakisema wanatumia sijui nondo au marumaru hapohapo kataeni kwa wino wa rangi nyekundu, mawe yanayoweza kupatikana Manyara kwa nini yaletwe kutoka nchi nyingine?

“Nondo ziko hapa nchini kwa nini walete kutoka nchi zingine, PPRA zingatieni kwamba malighafi zinazolishwa nchini zitumike, kuna viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo nchini,” amesema.

Dk Mwigulu amesema malighafi inayotakiwa kuagizwa nje ni ile ambayo haipo nchini na ikitokea mradi unahitaji nondo ya milimita 16 na hazipatikani taasisi inaweza kuingia mkataba na kiwanda cha ndani ili zitengenezwe.

“Kutopatikana kwa nondo ya milimita 20 kisiwe kigezo cha malighafi hiyo kuagizwa nje ya nchi, malighafi za miradi zitumike za nchi yetu na PPRA simamieni hili,” amesisitiza.

Dk Mwigulu ameiagiza PPRA kuhakikisha bidhaa zikiwemo samani zinazotaka kununuliwa kwa ajili ya matumizi ya taasisi za Serikali, basi zinunue zinazozalishwa nchini ili kuongeza uzalishaji, viwango vya kodi na ajira ndani ya Taifa.

“Anayependa samani za nje, anunue kwa ajili ya nyumbani kwake, kwa fedha yake siyo kuonyesha umwamba kwa fedha za walipakodi,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, kuna bidhaa za kisasa zinazopatikana katika viwanda vya ndani, lakina mazoea yanawafanya watu kuona vitu vinavyotoka nje ya nchi ndiyo bora zaidi na kusababisha Serikali kuingia kwenye gharama kubwa.

“Wenye viwanda wananiambia waziri ukiweka kiwanda hapa ndani ninyi (Serikali) mnaikwepa ile bidhaa, lakini ikizalishiwa nchi jirani mnaiunua,” amesema.

Katika hatua nyingine, amezitaka taasisi za Serikali kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), akisema kwa namna mambo yaliyo hauepukiki kutumika ili kutoka analojia kwenda dijitali.

“Nimesikia kuwa zipo baadhi ya taasisi nunuzi bado zinasitasita kutumia NeST ingawa zimewezeshwa kuutumia mfumo, nazielekeza kuzingatia matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma, na kutumia mfumo huu ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha tunapata thamani halisi ya fedha,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Dk Leonada Mwagike amesema katika kipindi cha mwaka 2023/24 taasisi hiyo imepata mafanikio kadhaa, ikiwemo maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024.

“Hizi zimejenga mazingira mazuri na wezeshi katika mnyonoro wa ununuzi wa umma, kujenga na kuanza kutumika kwa mfumo wa NeST kupitia wataalamu wa ndani, kuokoa Sh14.94 bilioni  kupitia ukaguzi na Sh2.7 trilioni kupitia ufuatiliaji,” amesema.

Related Posts