KAMBI YA MAGARI TEMBEZI YA VYUMBA VYA UPASUAJI YA MADAKTARI BINGWA WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAANZA KUTOA HUDUMA KWA WANANCHI WA ZANZIBAR

Na Jeremiah Mbwambo, Zanzibar , 28/09/2024.

Wananchi visiwani Zanzibar wamejitokeza kwa wingi kupata huduma ya matibabu kwenye kambi ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) chini ya Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la SOTAC katika Hospitali ya Mwera Pongwe, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini, Unguja.

Katika kambi hiyo ya matibabu BMH inatumia magari maalumu yenye vyumba vya upasuaji huduma ambayo imewezeshwa na Shirika la SOTAC kutoka Uholanzi.

Daktari Bingwa wa Ubongo na mishipa ya fahamu wa BMH, Henry Humba, amesema magari haya yanasaidia kutoa huduma ya upasuaji mahali popote wanapokuwa.

“Wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata matibabu ya Madaktari Bingwa kutoka BMH. Mpaka sasa, tumeona Wananchi zaidi ya 200 ndani ya hizi siku mbili na kati yao wagonjwa watano wamefanyiwa upasuaji kwenye magari haya” alisema Dkt. Humba

Ameongeza kuwa Madaktari wataendelea kutoa huduma kwa kadri ya wagonjwa watakavyo jitokeza.

“Tumepanga kuona wagonjwa kuanzia Saa 2:00 Asubuhi hadi Saa 9:30 Alasiri lakini wagonjwa wakijitokeza wengi tutaongeza muda wa kutoa huduma,” alisema Dkt. Humba.

Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa watakuwepo Zanzibar mpaka tarehe 04.10.2024.

Related Posts