Baba jela miaka 30 kwa kumpondaponda nyeti mtoto wa kufikia

Morogoro. Mahakahama ya Hakimu Mkazi Morogoro imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela Mohamed Omary Salange (37), baada ya kumkuta na hatia katika kosa la ukatili dhidi ya mtoto wake wa kufikia, mwenye umri wa miaka tisa.

Akisoma hukumu hiyo jana Alhamisi Mei 2, 2024 Hakimu Mkazi Mwandamizi Lameck Mwamkoa alisema kuwa mahakama hiyo baada ya kuzingatia ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa mshtakiwa, imejiridhisha pasipo na shaka kwamba mshtakiwa ana hatia kwa kosa aliloshtakiwa nalo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 8101/2024, Mohamed alishtakiwa kwa makosa sita ya ukatili dhidi ya mtoto wake huyo wa kufikia kinyume cha kifungu  cha 167 ( 1) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (PC), na kumsababishia madhara makubwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Januari 2023 na Januari 2024 katika  kijiji cha Kimamba A, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.

Ilielezwa kuwa katika kipindi hicho mshtakiwa alimfanyia ukatili mtoto huyo kwa kumng’oa meno, kumchoma moto sehemu ya juu ya mdomo na kwenye makalio, kumpiga na kumvunja kiwiko cha mkono,  kumponda na kuvunja korodani na kumtoboa sehemu ya ngozi ya uume wake (govi).

Katika hukumu hiyo, baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi na kupitia vifungu vya sheria na kesi rejea, Hakimu Mwamkoa alisema kuwa ushahidi ulioletwa unamnyooshea vidole mshtakiwa kwamba ana hatia na kwamba .

“Baada ya kupitia ushahidi wote na mazingira ya kesi hii mahakama hii imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa”, alisema Hakimu Mwamkoa na kuongeza:

“Mshtakiwa alisema hana cha kujitetea maana aliiambia mahakama kuwa ni kweli alimuua mkewe (mama wa watoto wake hao wa kufikia) lakini watoto hao na majirani wameamua kumkomoa kwa hasira kwakua alimuua Mama yao.”

Kisha Hakimu Mwamkoa alisema; “Hivyo mahakama hii imemtia hatiani mshtakiwa Mohamed Omary Salange, katika mashtaka yote manne ya unyanyasaji kama alivyoshtakiwa na Jamhuri na anastahili adhabu sahihi”.

Kabla ya kumsomea adhabu mshtakiwa, mwendesha mashtaka, Wakili  wa Serikali Maria Kaluse, aliyesaidiana na Wakili wa Serikali Jackkine Nyoka aliieleza mahakama hiyo kuwa hawana kumbukumbu za nyumba za makosa ya mshtakiwa na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza.

Hata hivyo alieleza kuwa vitendo hivyo vimefanyika dhidi ya mtoto mdogo ambaye alikuwa ni nguvu kazi ya Taifa, hivyo  adhabu kali itolewe ili iwe fundisho kwa wanaume wenye watoto wa kiume na wanaufanya ukatili dhidi yao.

Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea dhidi ya adhabu, aliieleza Mahakama kuwa anapokea adhabu yoyote.

Akisoma adhabu, Hakimu Mwamkoa alisema kuwa katika kutoa adhabu hiyo amezingatia hoja za pande zote pamoja na matakwa ya sheria.

“Mtu akifanya makosa kwenye makundi maalumu atatumikia kifungo cha miaka mitano jela. Hivyo katika makosa hayo mshtakiwa Mohamed Omary Salange atatumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela kila kosa, na adhabu zote zinajitegemea”, amesema Hakimu Mwamkoa.

Kwa amri hiyo kwamba adhabu zote zinajitegemea, basi mfungwa atatumikia adhabu moja moja na hivyo atatumikia kifungo cha jumla ya miaka 3o jela.

Ushahidi wa upande wa mashtaka uliowasilishwa mahakamani

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, mashahidi wa upande wa mashtaka akiwemo mtoto huyo mwathirika, waliieleza Mahakama jinsi mshtakiwa alivyomfanyia ukatili wa kutosha, waliieleza kuwa alimpondaponda korodsno mtoto huyo na kumpidilia msuri kwenye uume.

Mtoto huyo mwathirika ambaye alikuwa shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, aliieleza mahakama kuwa, kati ya Januari 2023, na Januari 2024 mshtakiwa alimpiga mtoto huyo kwa kipande cha nondo, kumponda kwa jiwe korodani ya kulia na damu zilipotoka alimwagia maji ya moto.

Pia alieleza kuwa mshtakiwa alimng’oa jino la juu akimtuhumu kula kupande cha nyama cha mdogo wake na kisha alimpiga kwa kipande cha nondo na  kumvunja mkono wake sehemu ya kiwiko na kumsababishia mkono usirurudi kwenye hali yake ya kawaida.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, wakati mshtakiwa akimfanyia ukatili huo mtoto huyo, mama yake alikuwepo lakini alishindwa kutoa msaada wowote.

Shahidi wa pili ambaye ni dada mkubwa wa huyo mwathirika aliieleza Mahakama kuwa kati ya Januari 2023 na 2024, mshtakiwa alimtesa mtoto wake wa kufikia wa kiume  kwa madai ya kufanya mapenzi na dada yake.

Shahidi huyo alieleza kuwa mshtakiwa alichukua jiwe, kipande cha nondo akaweka korodani na nondo kwa juu, kisha  akasaga korodani ya kulia huku akimwambia mtoto wake huyo wa kufikia kuwa anamtia ulemavu,.

Pia shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa alishuhudia uume wa kaka yake ukipigiliwa msumari na kisha kumpiga kwa kipande cha mbao mpaka mkono kuvunjika.

Shahidi wa tatu ambaye ni daktari, aliyemhudumia mtoto huyo, alisema kuwa baada ya kumchunguza mtoto huyo aligundua kuwa korodani ya kulia ilikua imepondwa na kuharibiwa na kwamba pia uume wa mtoto huyo ulikuwa na majeraha yaliyokuwa yamedumu kwa  muda kuanzia siku 90 kurudi nyuma.

Hii ni moja kati ya kesi nne zinazomkabili Salange zikiwemo kesi nyingine tena ya ukatili, kesi ya ubakaji dhidi mtoto wake wa kufikia wa kike pamoja na kesi ya mauaji ya mkewe (mama wa watoto wake hao wa kufikia).

Katika kesi hiyo ya mauaji ambayo anadaiwa kuwa alimuua mkewe kisha akamzika ndani ya nyumba, ambayo bado inaendelea mahakamani hapo katika hatua ya uchunguzi, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu itakakosikilizwa na kuamuriwa kwa kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Related Posts