Mikopo ya ada elimu ya juu yapanda

Dar es Salaaam. Wakati Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikitangaza awamu ya kwanza ya walionufaika, kiwango cha chini cha mkopo kwa mnufaika kimeongezeka.

HESLB imetangaza wanafunzi 21,509 wamepangiwa mikopo katika awamu ya kwanza.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 28, 2024 jijini Dar es Salaam amesema kiwango cha chini cha mkopo kwa mnufaika mmoja mmoja kimepanda hadi Sh3 milioni kutoka Sh2.7 milioni mwaka uliopita wa 2023/2024.

“Hii inafanya wastani wa ada kiwango cha chini unaotolewa kufikia Sh530,000 kutoka Sh230,000, hela hii inawafanya sasa wanafunzi wanaosoma kozi za bei nafuu kuwa na uwezo wa kulipiwa karibu ada yote wanayopaswa kulipa,” amesema.

Dk Kiwia amesema idadi ya waliopangiwa katika awamu ya kwanza ni ndogo lakini mikopo itaendelea kutolewa kadri bodi itakavyokuwa ikipokea majina ya waliodahiliwa katika vyuo vyao.

Amesema awamu hii ya kwanza inajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo ya Shahada ya awali, Shule ya Sheria kwa Vitendo na Shahada ya Uzamili.

“Wanafunzi watapata taarifa hizi kupitia akaunti zao walizotumia kuombea mikopo SIPA (Student’s Individual Permanent Account) lakini bado tunaendelea kufanyia kazi maombi yao… kila mwombaji anapata taarifa yake kwenye akaunti ileile aliyotumia kuombea mkopo, huhitaji kufika ofisi za HESLB,” amesema.

Serikali imetenga Sh787 bilioni kwa ajili ya wanafunzi 245,799 wakiwamo zaidi ya 88,000 wa mwaka wa kwanza waliotengewa Sh284.8 bilioni.

Bajeti hiyo ya mikopo katika mwaka 2024/2025 ni ongezeko la Sh38 bilioni sawa na asilimia 5.1 kulinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/2024 iliyokuwa Sh749.4 bilioni.

Kuhusu wanafunzi wanaonufaika na mkopo wanaoendelea na vyuo, Dk Kiwia amevitaka vyuo kuwasilisha matokeo ya wanafunzi kwa wakati ili wapewe mikopo.

“Kuwasilisha matokeo haya kwa wakati kunaiwezesha Bodi ya Mikopo kuandaa malipo kwa wakati na sasa hakutakuwa na ucheleweshaji ambao ulikiwa ukionekana siku za nyuma,” amesema.

Rais wa Shirikisho la Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (Tahliso), Zainab Kitima amesema ongezeko la ada iliyotolewa inaongeza ahueni kwa wananfunzi.

“Kuna ongezeko kutoka Sh230,000 hadi Sh530,000 haikidhi lakini wamefanya jitihada kubwa, hivyo kama mtu alikuwa analipa ada Sh1 milioni akipewa hii itamsukuma na ataweza kufanya mambo mengine,” amesema.

Ameitaka HESLB kuendelea kupokea changamoto ndogondogo watakazokuwa wakiziwasilisha na kuzifanyia kazi.

“Changamoto nyingine ilikuwa ni katika ucheleweshaji wa fedha tunashukuru Mkurugenzi amesema hautakuwepo,” amesema.

Amesema kutolewa kwa kiwango kidogo cha ada ilikuwa changamoto kwa baadhi ya wazazi wasiokuwa na uelewa wa kutosha ambao walidhani mtoto kupewa mkopo amemaliza kila kitu.

“Wazazi wengine walikuwa wakidhani kuwa ‘boom’ itaingia na mtoto atakuja shule, hivyo kuchelewa ilikuwa changamoto. Huu ni mwanzo mzuri,” amesema.

Related Posts