WAZAZI WATAKIWA KUTOKUACHA KUFANYA MAJUKUMU YA KUSIMAMIA WATOTO

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Amina Talib Ali ametoa wito kwa wazazi kutoacha kufanya majukumu yao ya kuwasimamia na kuwalinda watoto badala yake kuwatelekeza na kuwafanya kuwa watoto wa mtaani.

Hayo ameyasema wakati wa kumaliza ziara ya Siku sita katika Mkoa wa Kagera ya Kukusanya maoni ya Uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara hususani katika eneo la Haki za Watoto kutoka kwa wadau mbalimbali.

Mhe. Amina amesema kuwa katika maeneo ambayo THBUB ilipita hasa katika maeneo ya ziwani (Mwalo) na Vituo vya Kulelea Watoto wanaoishi katika mazingira magumu THBUB imebaini kuwepo kwa changamoto ya kuongezeka kwa watoto wa mtaani.

“Watoto hao wana haki kama watoto wengine hivyo ni jukumu la kila mzazi au mlezi kuhakikisha mtoto anapata haki zake zote kama zilivyoainishwa katika Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009”

Aidha, Mhe. Amina amelishukuru na kulipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto – UNICEF TANZANIA kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia jitihada za Serikali kulinda haki za watoto.

Kwa upande wake Bw. Jovith Paschale, msimamizi wa kituo cha kulelea watoto Wanaoishi katika mazingira magumu kinachoitwa Tumaini Children Centre ameeleza kuwa Kituo chao kinapokea watoto wa aina mbalimbali wakiwemo waliotekelezwa na Wazazi na wengine walioamua kukimbia nyumbani kutokana sababu mbalimbali zikiwemo umaskini, ukatili, migogoro ya ndoa na familia, na kutowajibika kwa wazazi na walezi katika kuwatunza watoto na kuwapatia malezi bora.

Bw. Paschale alieleza kuwa hata hivyo kituo cha Tumaini huwa kinatoa elimu kwa viongozi wa ngazi ya chini inayolenga kusimamia mienendo na tabia za watoto.
“Lakini pia viongozi hawa wamekua msaada sana katika kubainisha watoto wa mtaani” amesema Bw. Paschale.

Ziara ya THBUB Mkoani Kagera ilianza Septemba 23 hadi 27, 2024 na imefanikiwa kutembelea na kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa Wavuvi katika Mwalo wa Nyamukazi uliopo katika Manispaa ya Bukoba na Igabilo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya Bukoba,kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Kiwanda cha Kagera Sugar,Asasi za Kiraia,Wakulima wa Miwa na jamii inayozunguka mashamba ya miwa.

Related Posts