Mwanza. Miili mingine minane imeopolewa Ziwa Victoria baada ya mtumbwi wa mizigo uliobeba abiria wanaodaiwa kufikia 31 kuzama Septemba 25, 2024.
Awali, Jeshi la Polisi lilisema lilikuwa likiendelea kutafuta mwili mmoja lakini imeopolewa minane, hivyo kuacha maswali kuhusu idadi ya waliokuwa kwenye mtumbwi huo.
Ajali hiyo ilitokea saa 11.00 jioni katika mwalo wa Bwiru wilayani Ilemela ikihusisha mtumbwi wenye namba za usajili TMZ 012212 (Mv Sea Falcon) unaomilikiwa na Amon Rutabanzibwa uliokuwa ukitokea mwalo wa Kirumba kwenda Kisiwa cha Goziba kilichopo Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera.
Ajali ilitokea baada ya mtumbwi huo kugonga mwamba, hivyo ulipinduka na kuzama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akitoa taarifa ya hali ya uokoaji amesema jana Septemba 27, saa 12.00 jioni mwili mmoja uliopolewa na leo Septemba 28, imeopolewa saba. Jumla ya miili iliyoopolewa imefikia tisa.
Amesema kazi ya uopoaji imefanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na wananchi wilayani Ilemela.
“Tulitoa taarifa kwamba watu 29 waliokolewa huku mtu mmoja akifariki dunia lakini tuliwapa orodha ya waathirika ambao walikuwa wanatibiwa hospitalini ambao hali zao zinaendelea vizuri na tayari wameruhusiwa,” amesema.
Akijibu swali kuhusu idadi ya abiria waliokuwamo kwenye mtumbwi, Kamanda Mutafungwa amesema ni dhahiri walikuwa zaidi ya 31 kama walivyoelezwa na nahodha wa mtumbwi huo na abiria waliokuwamo.
Mutafungwa amesema miili minne imetambuliwa na kwamba uongozi wa Mkoa wa Mwanza umetoa majeneza, fedha na usafiri kwa ajili ya mazishi.
Ametoa wito kwa wananchi kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kutambua miili.
Ametaja miili iliyotambuliwa kuwa ni ya Furaha Bundele (17), mkazi wa Luhemeja Sengerema, Kelvin Salvatory (20), mkazi wa Migombani Sengerema, Rashid Juma (33) mvuvi mkazi wa Kirumba, na Benene Boaz (57) mvuvi mkazi wa Buhongwa.
Amesema miili iliyotambuliwa imechukuliwa na ndugu kwa ajili ya maziko.
Mkazi wa Bwiru, Clement Masonyi ameiomba Serikali kuwapatia boti kwa ajili ya abiria katika Ziwa Victoria ili kupunguza ajali.