Zungu: Jamii ijitenge na taarifa zisizo sahihi

Dar es Salaam.  Jamii imeaswa kutofungama na makundi ya watu yenye lengo la kubomoa umoja uliojengeka baina yao kwa kusambaza taarifa zisizo sahihi na kuibua chuki na taharuki.

Wito huo umetolewa leo Septemba 28, 2024 jijini Dar es Salaam na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu katika siku ya pili ya mkutano wa 53 wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania.

Zungu amesema kila mtu katika jamii anapaswa kujiona ana wajibu wa kulinda amani na kuisaidia Serikali katika kuhakikisha wanaofanya vitendo vya uvunjifu wa amani wanachukuliwa hatua za kisheria.

Ametoa wito kwa viongozi wa dini kuiombea nchi na kuendelea kuhubiri masuala ya amani na upendo kwa waumini.

Vilevile ameipongeza jumuiya hiyo kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya athari ya kuchanganya masuala ya dini na siasa.

“Kuchanganywa kwa masuala ya dini na siasa kunaweza kuleta mkanganyiko na kuzalisha mianya ya ama wanasiasa kuitumia dini vibaya au watu wa dini kutumia siasa vibaya kwa ajili ya masilahi yao binafsi,” amesema.

Katika mkutano huo, Zungu pia amezungumzia mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana, akitaja utandawazi na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao kama baadhi ya visababishi.

Amesema ili kuondokana na changamoto hiyo ni muhimu wazazi kuhakikisha wanahimiza na kusimamia watoto kupata elimu ya darasani pamoja na ya dini.

Vilevile amewataka viongozi wa dini kuhakikisha jamii inapata mafunzo sahihi ya dini ili kuwajenga kuwa na hofu ya Mungu.

“Elimu sahihi ya kimaadili mnayowapa watoto wenu ndiyo inayojenga jamii imara yenye kujenga waumini wenye maadili. Mtu hawezi kuwa mpenzi wa Mungu kisha akaacha kufanya wema kwa viumbe wengine hasa wanadamu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu Msingi, Abdi Maulid amesema mtoto akipata elimu ya darasani na ya dini itasaidia kuzalisha wanataaluma katika fani mbalimbali wenye maadili.

Amir wa jumuiya hiyo, Khawaja Ahmad amesema madhehebu hayo yamekuwa yakifanya mkutano kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha waumini na kuwakumbusha wajibu wao kama binadamu hapa duniani ikiwemo kumcha Mungu.

Amesema mkutano huu unalenga kuongeza hofu ya Mwenyezi Mungu, kuhimiza kuepukana na maovu, kuchochea moyo wa huruma na upendo na kuwakumbusha waumini kuendeleza tamaduni ya kuisaidia jamii katika nyanja mbalimbali, ikiwemo utoaji wa huduma za afya, elimu na misaada ya kibinadamu kwa wenye uhitaji bila ya kujali itakadi ya imani zao.

“Vilevile  kuwaelimisha na kuwahimiza vijana kuwa na mienendo bora ya kimaisha na kuwa raia wawajibikaji kwa nchi yao, na kuwa viongozi waadilifu katika jamii kwa mustakabali wa jamii na Taifa bora,” amesema.

Related Posts