Dar es Salaam. Wakati wananchi wakiendelea kuhamasishwa kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira, imeelezwa kuwa baadhi yao wanaogopa kutumia gesi wakiamini si salama.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Gesi za Mitungi Tanzania (TZLPGA), Amos Jackson, akiwataka wananchi kuondoa hofu na kuitumia kwa kuwa vifaa vyake ni bora na usimamizi wa sekta nzima ni mzuri.
Akizungumza jana Ijumaa Septemba 27, 2024 katika kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na Kituo cha ITV kikiwa na mada isemayo; ‘Kampeni ya nishati safi ya kupikia kwa kila Mtanzania je ni fursa au changamoto? amesema moja ya changamoto waliyobaini katika utafiti ni woga wa wananchi kuhusu matumizi ya gesi.
“Tulichokibaini ni woga kwamba gesi si salama, inalipuka. Lakini nataka niseme, kweli gesi ukiitumia bila kufuata taratibu inaweza kukuletea matatizo.
“Tatizo kubwa la gesi linaanzia kwenye kuvuja, ikivuja na kukutana na moto inaleta shida, kwa takwimu zilizopo mwaka 2022 matukio ya moto yanayohusisha gesi yalikuwa 134, hata hivyo mwaka huohuo matumizi yalikuwa kilo milioni 160 sawa na zaidi ya mitungi milioni 20,” amesema.
Amesema usalama ndiyo jambo wanalolipa kipaumbele katika chama hicho hasa katika ujazaji wa gesi, wakitumia vifaa vya kisasa ili kuwalinda watumiaji wa nishati hiyo.
Baadhi ya mamalishe walikuwa na maoni tofauti kuhusu matumizi sahihi ya gesi katika shughuli zao za upishi.
Mamalishe kutoka Vingunguti jijini Dar es Salaam, Sofia Athuman amesema kinachomfanya kuendelea kutumia kuni na mkaa ni changamoto ya eneo la kupikia akisema yeye na wenzake wanapikia nje, hivyo inawawia vigumu kutumia gesi wakiamini inaisha haraka.
Emmy Omary anayejishughulisha na mamalishe amesema aliamua kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia kutokana na urahisi wake wa kuokoa muda tofauti akitumia kuni na mkaa katika shughuli hizo.
Katika hatua nyingine, Jackson amesema gharama zilizopo za gesi zinatokana na ununuzi na uagizaji kutoka soko la dunia.
Amefafanua gesi hiyo ni bidhaa inayozalisha pamoja na mafuta, na kwamba meli ikifika bandarini inaenda kuhifadhiwa kwenye maghala ambako kuna gharama za usafirishaji kwenda maeneo mbalimbali.
“Ukweli ni kwamba gharama ya ununuzi kwenye soko la dunia inachangia asilimia 50 hadi 55 ya bei kwa mtumiaji wa mwisho wa gesi hii,” amesema.
Ili kuondokana na changamoto zilizopo, amesema lazima bandari ipanuliwe ili kupunguza gharama za usafirishaji.