HII ni siku spesho. Ndio, ni Sunday Spesho kwelikweli. Kwani kama wewe ni shabiki wa soka, basi leo hupaswi kuchezea rimoti kabisa. Yaani ukikaa mbele ya runinga leo hubanduki kitini hadi kesho Jumatatu. Yes, na kama wewe ni mtu wa kucheki soka katika kibanda umiza, fanya chapu uage kabisa mapema, kwani ukiingia kibandani mchana, basi ujue unatoka usiku mwingi.
Ukiachana na mechi kali zinazopigwa barani Ulaya, ikiwamo Madrid Dabi na ile mbungi ya Man United dhidi ya Tottenham, hapa Bongo kuna mechi nne kali za bandika bandua kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 3:00 usiku.
Ule uhondo wa Ligi Kuu Bara unaendelea leo kwa michezo minne ya kibabe ndani ya Sunday Spesho. Saa 8 mchana itaanza mechi ya Singida Black Stars itakayokuwa wenyeji wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Liti, Singida kisha baada ya mbungi hiyo, itafuata mechi nyingine kali ya Mashujaa dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.
Sasa wakati mashabiki wa Man United wakiwa wanasikilizia mchezo wao wa Spurs kule England, huko kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma kuna kitupe kingine cha maana kati ya Dodoma Jiji dhidi ya Mnyama, Simba ambaye ameuanza msimu huu na moto mkali ikishinda mechi tatu mfululizo akifunga jumla mabao 9-0.
Mara baada ya pambano hilo la Dodoma, kazi itahamia Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam wakati watetezi, Yanga watakapokuwa wenyeji wa KMC katika mechi ya kufungia hesabu kwa hapa nchini, kabla ya watu kuhamia La Liga kucheki Dabi ya Madrid, kati ya Atletico Madrid na Real Madrid zitakazokuwa uwanjani mara baada ya Yanga na KMC kutoka mapumziko yaani saa 4:00 usiku.
Matokeo ya mechi zote nne za Ligi Kuu Bara kwa leo yanaweza kubadilisha taswira nzima ya msimamo wa ligi hiyo, ambayo kwa sasa inaongozwa na Fountainm Gate yenye pointi 13, ikifuatiwa na Singida BS yenye 12, kisha Simba yenye tisa, Mashujaa (8), Azam (8), huku Yanga, JKT TZ na Dodoma kila moja ina pointi sita.
Hii maana yake vigogo vikishinda mechi hizo au kupoteza kila kitu kitabadilika, bila kujali matokeo ya mechi zilizopigwa jana katika ligi hiyo iliyoingia raundi ya sita kwa sasa.
Mapema saa 8:00 mchana, Singida BS itakuwa wenyeji wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida, huku kila moja ikitoka kupata ushindi katika mechi zilizopita. Singida iliifunga Tabora Utd kwa mabao 3-1 ikiwa ugenini na JKT kushinda 2-1 nyumbani dhidi ya Coastal Union.
Ni wazi haitakuwa mechi nyepesi kwa timu hizo, kwani Singida kama itashinda itarejea kileleni ikifikisha pointi 15 na kuishusha Fountain Gate yenye alama 13 kwa sasa, lakini JKT ikiendeleza wimbi la ushindi itafikisha pointi tisa na kusikilizia matokeo ya mechi zitakazofuata baadaye kujua wanasimamia wapi.
Ni mechi yenye ufundi na inayokutanisha wachezaji wenye uzoefu wa mechi kubwa na wazoefu wa Ligi ya Bongo na ni wazi makocha wa timu zote, Patrick Aussems na Ahmad Ally watakuwa na kazi kubwa kuhakisha wachezaji wanatekeleza kile walichoelekezana uwanjani.
Baada ya mechi hiyo, Mashujaa yenye mwanzo mzuri msimu huu ikiwa imecheza mechi nne na kupata ushindi mara mbili na kutoka sare mbili, ikivuna pointi nane na mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili, itakuwa wenyeji wa Azam.
Azam ina idadi sawa ya pointi na Mashujaa, lakini yenyewe imecheza mechi tano, ikipata ushindi mara mbili sare mbili na kupoteza moja ikifunga mabao matano na kufungwa mabao mawili.
Nassor Saadun mwenye mabao mawili, bila ya shaka ndiye mchezaji wa kuchungwa zaidi kwa kikosi cha Azam leo huku kwa Mashujaa wakiwa ni Crispin Ngushi na David Ulomi ambao kila mmoja amefunga mabao mawili pia.
Wenyeji Mashujaa walitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Pamba ugenini kwenye mechi iliyopita wakati Azam FC ilipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Simba nyumbani.
Kumbukumbu zinaonyesha timu hizo zimewahi kukutana mara mbili msimu uliopita na Mashujaa ilipigwa 3-0 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika kabla ya kulazimisha suluhu Chamazi na leo itapenda kulinda heshima yake nyumbani.
Kocha wa Mashujaa, Mohammed Abdalah ‘Baresi’ alisema mchezo wa leo ni mgumu na wanaipa heshima kubwa Azam.
“Kupoteza mechi iliyopita hakufanyi tuione Azam ni timu ya kawaida au rahisi kucheza nayo. Hii ni mechi ngumu ambayo nimeshawaambia wachezaji wangu kuwa wasiweke akilini matokeo ambayo wapinzani wetu wamepata katika mechi iliyopita. Naamini mechi haitakuwa nyepesi lakini kwa maandalizi tuliyoyafanya na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, tuna matumaini ya kufanya vizuri,” alisema Baresi, huku kocha Rachid Taoussi wa Azam aliyeachwa na hasira kwenye Uwanja wa Amaan kwa kuchapwa na Simba 2-0 amesema wamejiandaa kurudi katika mstari baada ya kupoteza nyumbani mbele ya Mnyama, mechi ambayo alitaka VAR ianze kutumika haraka akidai mabao yote mawili aliyofungwa na Simba yalikuwa ni ya kuotea.
Kuanzia saa 12:30 jioni, nyasi za Uwanja wa Jamhuri, Dodoma zitawaka moto kwa mchezo huu mkali huku kila timu ikiwa na kumbukumbu tofauti kwa mechi zilizopita na kuongeza ugumu na ladha ya mechi ya leo.
Dodoma imetoka kupata sare mbili mfululizo na kiujumla imecheza mechi nne tu ambazo kati ya hizo, imepata ushindi mara moja na kupata sare tatu wakati Simba imepata ushindi mechi zote tatu ilizocheza.
Hii ina maana kwamba, Dodoma Jiji inasaka ushindi kwa mara ya kwanza katika Ligi msimu huu, huku Simba ikitamani kupata ushindi wa nne mfululizo utakaoiweka pazuri katika msimamo ikizangatia ubabe iliyonayo mbele ya wenyeji wao hao.
Dodoma Jiji imekuwa na unyonge mbele ya Simba kwani imepoteza mechi zote nane zilizowahi kukutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu.
Wenyeji hao wanapaswa kumchunga zaidi mshambuliaji Leonel Ateba ambaye katika mechi mbili zilizopita za Simba katika mashindano tofauti amefunga mabao mawili, huku Simba ikilazimika kumlinda zaidi Paul Peter mwenye mabao mawili kati ya matatu ambayo Dodoma Jiji imepachika kwenye ligi msimu huu.
Mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na straika wa Dodoma, Waziri Junior alisema; “Kocha ametuambia tuingie kwa kujiamini na kuhakikisha tunatumia nafasi zote tutakazopata kutoka kwa wapinzani wetu. Sio rahisi Simba kutoboa kwetu kwa jinsi tulivyojipanga, hata kama safu yao ya ushambuliaji imekuwa ikifunga lakini sio kwetu.”
Kuanzia saa 3:00 usiku watetezi Yanga, watakuwa kwenye Uwanja wa Azam Complex kuialika KMC huku mambo mawili yakiipa jeuri katika mchezo huo.
Kwanza ni historia ya ubabe ambayo imekuwa nayo dhidi ya KMC ambao katika mechi 12 za nyuma zilizowahi kukutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu, Yanga imeibuka na ushindi mara tisa, sare mbili na KMC imeshinda mchezo mmoja.
Lakini jambo la pili ni muendelezo wa ubora ambao kikosi chake kimekuwa nao na kuchangia matokeo mazuri katika mechi za mwanzo za ligi kulinganisha na KMC ambayo imeanza kwa mguu wa kushoto.
Yanga imepata ushindi katika mechi zake zote mbili za ligi ikifunga mabao matatu na kutoruhusu nyavu zake kutikiswa huku KMC ikipata ushindi mara moja na kupata sare moja huku ikipoteza michezo mitatu, ikifunga mabao matatu na kufungwa mabao saba.
Stephane Aziz Ki ambaye hadi sasa ametoa asisti zilizozaa mabao mawili kwenye ligi ndiye mchezaji ambaye wapinzani wake wanapaswa kumuwekea ulinzi mkubwa leo wakati huo KMC ikimtegemea zaidi Redemptus Musa ambaye ameifungia timu hiyo mabao mawili kati ya matatu iliyonayo kwenye ligi hadi sasa.
Uimara wa safu ya ulinzi ni silaha kubwa ya Yanga msimu huu kwani umeifanya timu hiyo kuruhusu bao moja tu kwenye mechi nane za mashindano tofauti ambayo imeshiriki msimu huu lakini pia ina makali katika kufumania nyavu ikifunga mabao 25.
Yanga inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi mbili mfululizo za ligi ikiwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar iliyowanyuka mabao 2-0 na KenGold iliyoilaza 1-0 mechi iliyopita, lakini ikiweka rekodi ya kufunga jumla ya mabao 25-1 katika mechi nane za mashindano msimu huu kuonyesha ina safu kali ya ushambuliaji na ukuta wa chuma.