Fadlu aongea neno zito mastaa wa Simba

KOCHA wa Simba, Fadlu Davids jioni ya leo anajiandaa kuiongoza tena timu hiyo kwa mara ya nane katika mechi za mashindano kwa msimu huu tangu alipolamba ajira kuchukua nafasi ya Abdelhak Benchika, huku akisema jambo muhimu kuhusu mastaa wa timu hiyo.

Kocha huyo ameiongoza Simba katika mechi tatu za Ligi Kuu ikishinda zote na kutoruhusu bao lolote hadi sasa huku yenyewe ikifunga mabao tisa, wakati katika Ngao ya Jamii, imecheza mechi mbili ikipoteza moja na kushinda moja, ikifunga bao moja na kuruhusu moja, huku katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika imecheza michezo miwili na kutoka suluhu moja na kushinda moja kwa mabao 3-1.

Ukijumuisha mechi hizo saba za awali, Simba imefunga jumla ya mabaoa 13 na yenyewe kufungwa mawili, ikishinda michezo mitano, sare moja na kupoteza mmoja pia.

Jambo hilo linampa furaha kocha Faldu aliyetua Msimbazi akitokea Raja Casablanca alipokuwa kocha msaidizi.

Kocha huyo alisema anafurahishwa na wachezaji wanavyoonekana kushika kwa wepesi mbinu zake na kuzitekeleza kwa ufanisi uwanjani na kwamba anaamini kadri siku zinavyozidi kusonga mbele mambo yatakuwa moto zaidi kuliko ilivyo sasa.

“Nawapongeza wachezaji kwa wanavyotekeleza mpango wetu kwa usahihi, lakini huu ni muendelezo wa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya tangu tulivyouanza msimu. Nawapongeza pia jopo la ufundi, hususani Matola (Selemani) ambaye ni kocha wa mifumo. Wamefanya kazi kubwa nyuma ya pazia, ikiwemo kupanga mipango ya pressing na kuweka mitego ya kushambulia ambayo wachezaji wanaitekeleza vyema,” alisema.

Pia kocha huyo alisema pamoja na kucheza mechi nyingi kwa muda mfupi ni changamoto kubwa, hasa kwa sababu ya mtindo wa Simba wa kucheza kwa kasi, lakini wanaendelea kukomaa ili kuhakikisha wanaenda mapumziko yajapo akiwa pazuri na kujipanga kwa mechi zijazo zikiwamo za makundi ya CAF.

“Mtindo wetu wa kucheza ni wa kasi na unahitaji wachezaji kuwa na nguvu na utimamu wa kimwili. Hivyo, mechi hizi zinatufundisha nini cha kufanya, na hadi sasa niseme tupo kama asilimia 60 ya mipango ya benchi la ufundi na tukifikia 100 tutakuwa mbali zaidi,” alisema Fadlu ambaye leo ataikabili Dodoma Jiji katika mechi ya Ligi Kuu.

Related Posts