Gamondi amaliza utata kwa Baleke

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kushuka uwanjani usiku wa leo kukabiliana na KMC, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi akimaliza utata kwa kutoa sababu zinazomfanya mshambuliaji mpya, Jean Baleke aliyeibua maswali kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kwa kutoonekana uwanjani.

Baleke alisajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Al Ittihad ya Libya alikocheza kwa miezi sita tu kwa mkopo kutoka TP Mazembe ya DR Congo, ambapo awali alikuwa akikipiga Simba, lakini tangu atue amekuwa akitumika kwa muda mchache huku akikosa baadhi ya mechi za mashindano zikiwamo za Ligi Kuu.

Hadi sasa Yanga ikiwa imecheza mechi nane, zikiwamo nne za kimataifa, mbili za ligi na mbili za Ngao ya Jamii, nyota huyo aliyeondoka nchini akiwa na mabao manane, hajapata nafasi ya kucheza mchezo hata mmoja, japo michezo miwili ya awali ya CAF alikuwa na tatizo la kucheweshwa kwa hati ya uhamisho.

Kukosekana kwake kikosini kumezua mijadala mingi mitandaoni na vijiweni kwamba Gamondi anambania, lakini kocha huyo amefichua kuwa kuna mambo anayaweka sawa kwa mchezaji huyo na atakapoanza kuonekana atakuwa wa moto sana tofauti na kelele zinazopigwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema Baleke ni mshambuliaji mzuri ndio maana amesajiliwa Yanga na anaruhusiwa kucheza ila anahitaji kupigwa msasa kidogo ili awe bora zaidi na kwamba muda si mrefu mambo yatakuwa sawa na ataliamsha kwa vile bado kuna mechi nyingi ambazo Yanga itacheza.

Gamondi alisema hatua zinafanyika kwa sasa za kumboresha ambazo zimeanza muda mrefu, kwani kwanza walikuwa wanampambania apungue kidogo uzito jambo linaloendelea vizuri kwa sasa, kwa kuwa alikuwa mzito kiasi cha kushindwa kuendana na kasi ya benchi la ufundi ndio maana wenzake wanaendelea kukipiga.

“Sasa yuko na programu maalum ili kumuongezea wepesi wa kufanya uamuzi akiwa karibu ya lango na kufunga zaidi ya alivyozoeleka,” alisema Gamondi anayewatumia Clement Mzize, Prince Dube na Kennedy Musonda anayeingia zaidi kipindi cha pili akitokea benchini.

“Pia mjue kabisa Baleke ni mahiri zaidi kwa kufunga mabao ya kichwa kuliko miguu, ndio maana tunaendelea kumpa mazoezi awe mtamu kotekote,” alisisitiza Gamondi na kuongeza;

“Mshambuliaji mzuri ni yule ambaye anaweza kufunga kwa mipira ya aina zote juu na chini, kwani kazi yake kubwa ni kuipa timu matokeo ndio maana tunamnoa zaidi, lakini sio kama nina tatizo naye, wachezaji wote kwangu ni wachapakazi , kikubwa natafuta matokeo zaidi kuliko jina la mtu.”

Katika nafasi anayochezea Baleke, yuko Dube aliyesajiliwa pia msimu huu kutoka Azam FC, huku Mzize na Musonda wakiwa wazoefu kwa misimu kadhaa sasa Jangwani, huku Dube akiwa na mabao manne hadi sasa, yakiwamo matatu ya CAF na moja la Ngao ya Jamii.

Mzize ndiye anayeongoza kwa washambuliaji wa kufunga mabao mengi akiwa na matano akifunga michuano yote, matatu ya CAF, moja la Ngao ya Jamii na moja jingine la Ligi Kuu Bara, pia akiongoza kwa kutumika zaidi kulinganisha na washambuliaji wengine.

Related Posts