NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Wananchi wamehimizwa kuendelea kuchukua tahadhari na kuondoka katika maeneo hatarishi yenye viashiria vya kuathiriwa na maafa ili kuendelea kuwa na jamii salama na tulivu hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na maafa ya mafuriko yaliyotokea tarehe 25 Aprili, 2024 katika mkoa wa Kilimanjaro ambayo ni Kata ya Msaranga, Mji Mpya na Kimochi ziliathiriwa na maafa hayo.
Dkt. Yonazi ametoa rai kwa wananchi kuzingatia taarifa zinazotolewa na Serikali pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari za mapema ili kuendelea kujilinda na kuendelea kuwa na jamii stahimilivu dhidi ya maafa.
“Serikali itaendelea kukabiliana na maafa mbalimbali nchini kwa kuendelea kutoa elimu juu ya namna ya kujiandaa na kukabili maafa ili kuondokana na madhara yatokanayo na maafa pindi yanapotokea,” alisema Dkt. Yonazi.
Alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye dhamana ya masuala ya menejimenti ya maafa hivyo itaendelea kuratibu kwa weledi na kuyafikia malengo kama inavyotakiwa.