Dar es Salaam. Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), wamemchagua Hashimu Rungwe kuendelea kuwa Mwenyekiti wa chama hicho kwa muhula wa tatu mfululizo.
Mkutano huo umefanyika Jumamosi, Septemba 28, 2024 jijini Dar es Salaam, miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Mohamed Masoud amesema nafasi ya mwenyekiti mgombea aliyejitokeza ni mmoja na amepigiwa kura ya ndiyo au hapana. Kati ya kura 120 zilizopigwa, 118 zilikuwa za ndio na kura mbili za hapana.
Baada ya kutangazwa mshindi, Rungwe aliwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa kuendelea kumuamini na kuwa ataendelea kuisimamia sera yake ya ubwabwa shuleni na hospitalini, huku akisisitiza mpango wa chama chake kupeleka bahari Dodoma upo palepale.
Naye Nyahoza amekipongeza chama hicho kwa kufanya siasa za ustaarabu na kusimamia tunu za Taifa ikiwemo amani.
Katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti, Kayumbo Kabutari alijitosa Bara, huku Issa Abbas upande wa Zanzibar nao wakipigiwa kura na kuibuka washindi.
Rungwe alijizolea umaarufu katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo alijinadi na sera ya kupeleka ubwabwa shuleni na hospitalini, akiamini wanafunzi bila kula vizuri hawawezi kufanya vyema kwenye masomo.
Hata hivyo katika uchaguzi huo hakufanikiwa kushinda japokuwa sera yake hiyo ilizua gumzo mitandaoni.
Agenda hiyo haikuishia hapo, miaka mitatu baada ya uchaguzi kupita, Machi 7, 2023 Rungwe aliibuka tena akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mfumuko wa bei, alipigilia msumari kwa kusema kuwa ubwabwa unatakiwa kutolewa bure hospitalini na shuleni katika kipindi hicho.
“Chakula kinapaswa kitolewe bure watoto wetu wanaumia ila hawawezi kuongea wanapaswa wapewe ubwabwa bure, hata katika hospitali wagonjwa wapewe bure kwani Serikali ina uwezo kwa sababu inakusanya kodi kubwa,” alisema Rungwe.