LICHA ya kusaka wachezaji bora, raundi ya nne ya Lina PG Tour pia imemuenzi Dioniz Malinzi kwa mchango wake mkubwa katika kukuza vipaji vya wacheza gofu wazawa katika mpango mahsusi aliouasisi miongo miwili iliyopita, na hivi leo, wachezaji hao ndiyo nyota wanaoifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa matano yanayoongoza katika mchezo wa gofu barani Afrika.
Madina Idd, Hawa Wanyeche na Angel Eaton, ambao waliiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili mara mbili na nafasi ya tatu mara moja katika mashindano ya ubingwa wa Afrika nzima kwa wanawake, ni baadhi ya matunda ya uwekezaji uliofanywa na Malinzi akiwa mwenyekiti wa Chama cha Gofu (TGU) nchini, Mwenyekiti wa Klabu ya Dar es Salaam Gymkhana na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Alipowasili katika viwanja vya klabu ya Moshi siku ya Ijumaa, Malinzi alikuta vijana wake aliowapika miaka 20 iliyopita wakiongoza katika mbio za kusaka taji la Lina PG Tour hususani Nuru Mollel, Elisante Lembris, John Saidi na John Leonce kwa upande wa gofu ya kulipwa.
“Malinzi ndiyo kila kitu kwangu maana bila ya yeye kunitoa uswahilini na kunilipia ada ya uanachama katika klabu ya Dar Gymkhana, ningebaki hadi leo kuwa kijana wa kawaida mtaani,” alisema Nuru Mollel ambaye anaongoza mbio za kuwania taji la Lina PG Tour kwa upande wa gofu ya kulipwa.
Mollel anasema Malinzi ndiye aliyewaingiza kwenye gofu yeye, Frank Roman, Elisante Lembris na Jimmy Mollel katika mpango wa ufundishaji gofu kwa vijana chipukizi ambao uliwaendeleza hadi wao kufikia ngazi ya kuwa wachezaji wa timu ya taifa na baadaye kuwa wacheza gofu ya kulipwa.
Licha ya kuwaendeleza kina Madina Iddi, Wanyeche na Eaton, ni Malinzi ndiye aliyemuendeleza Neema Olomi ambaye hivi sasa ni mchezaji wa timu ya taifa akichukua nafasi ya Eaton ambaye amepanda hadhi na kucheza gofu ya kulipwa.
“Nilianza kama caddie (mbeba fimbo) wake kabla ya mimi kuanza kucheza gofu kimashindano. Niko hapa kama mchezaji mzuri wa kike kwa sababu yake. Bila Malinzi sijui ningekuwa wapi hivi leo,” alisema Olomi kutoka klabu ya Arusha Gymkhana.
Akielezea kuhusu ujio wa Malinzi, mkurugenzi wa Lina PG Tour, Yasmin Challi alisema wamemualika Malinzi kwa kutambua mchango wake katika kuendeleza gofu nchini na hiyo inahusisha gofu ya kulipwa na ridhaa.
“Kama Lina PG Tour inamuenzi Lina Nkya aliyechochea maendeleo ya gofu kwa wanawake, nasi tumemuenzi kwa kuchochea maendeleo ya gofu kwa wanaume, wanawake pamoja na gofu ya kulipwa,” alifafanua Challi.
Akielezea zaidi kuhusu mchango wa Malinzi, Elisante Lembris wa Arusha Gymkhana amesema Malinzi ndiye aliyewashauri vijana wengi kujiunga na gofu ya kulipwa ambayo imewapa ajira wengi wao.
“Hivi sasa gofu ni ajira kwangu na inanipa maisha mazuri pamoja fursa ya kuijua dunia nzima kupitia mchezo huu,” alimaliza.