Kalambo achungulia dirisha dogo mapema

KIPA wa Geita Gold, Aaron Kalambo amesema licha ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na kikosi hicho ana uwezo pia wa kuondoka Desemba mwaka huu wakati wa dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa, huku nia yake ni kucheza Ligi Kuu Bara.

Kalambo aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Dodoma Jiji, alisema, licha ya malengo hayo aliyojiwekea bado ataipambania timu hiyo.

“Kila mchezaji malengo yake ni kucheza Ligi kubwa na yenye ushindani, nimesaini mwaka mmoja wenye kipengele ambacho nikipata timu naweza kuondoka katika dirisha dogo, najivunia kwanza hapa nilipo leo na nitapambana kwa ajili ya kikosi hiki.”

Akizungumzia ushindani wa Ligi ya Championship msimu huu, Kalambo alisema timu zote 16 zimejipanga vizuri kwa sababu ya uwepo wa wachezaji bora na wazoefu wenye hadhi ya Ligi Kuu Bara, hivyo sio ligi rahisi hata kidogo kama wengi wanavyofikiria.

Nyota huyo alikaribia kujiunga na KenGold inayoshiriki Ligi Kuu Bara ingawa walishindwana mwishoni kutokana na suala la kimaslahi, huku Geita Gold ikiwa ni timu ya pili kwake kucheza akiwa Championship baada ya awali kuitumikia Dodoma Jiji.

Related Posts