Serukamba afunga vibanda vya wafanyabiashara wasiolipa kodi Mafinga

Mufindi. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba ameagiza kufungwa kwa baadhi ya vibanda katika Soko Kuu la Mafinga lililopo katika halmashauri ya mji wa Mafinga, baada ya wafanyabiashara kushindwa kulipa kodi.

Tayari baadhi ya vibanda hivyo vimezungushiwa utepe, ikiwa ishara ya kutoruhusu wafanyabiashara ambao hawajalipa kodi ya halmashauri kuendelea na shughuli zao hadi watakapolipa kodi stahiki.

Mei 21, 2024, Serukamba pamoja na wafanyabiashara hao walikaa pamoja na kukubaliana kulipa kodi ya Sh80,000 kwa mwezi ndani ya miaka 14, ikiwa imeongezeka kutoka Sh9,000 waliyokuwa wakilipa awali. Baada ya muda huo, vibanda hivyo vilivyojengwa na wafanyabiashara wenyewe vitachukuliwa na halmashauri.

Wafanyabiashara ambao vibanda vyao vimefungwa, ni wale ambao hawakulipa kodi zao kuanzia Juni hadi Septemba 2024, huku mkuu huyo wa mkoa akiwataka walipe kodi za miezi ya nyuma, kisha kuanzia Oktoba mwaka huu ndio waanze kulipa kodi mpya ya Sh70,000, Sh60,000 pamoja na Sh50,000, kulingana na ukubwa wa kibanda.

Agosti 23 hadi 26, mwaka huu, wafanyabiashara katika soko hilo walifunga maduka yao kwa siku nne mfululizo, wakipinga ongezeko la kodi ya Sh80,000. Hata hivyo, walifungua maduka yao kabla madai yao hayajatekelezwa. Hata hivyo, baada ya tathimini ya kina, kodi hiyo ilipunguzwa kidogo.

Serukamba alitoa maelekezo hayo Septemba 28, mwaka huu baada ya kuzungukia vibanda 405 kufanya tathimini ya kiwango cha kodi ambacho wafanyabiashara hao wanatakiwa kukilipa kwa halmashauri hiyo.

Amesema haiwezekani karne hii ya 21, mfanyabiashara alipe Sh3,000, Sh6,000 au Sh9,000 wakati sehemu ambayo amepanga kwa ajili ya kufanya biashara hiyo, analipa Sh200,000 lakini kulipa kodi ya halmashauri ya Sh80,000 inakuwa vigumu, wakati wamekaa na vibanda hivyo kwa zaidi ya miaka 30.

Amesema Serikali imekuwa ikileta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo lazima halmashauri ikusanye mapato mengi, ili kupeleka maendeleo kwa wananchi.

“Mapato ya soko hili yakikusanywa vizuri, tuna uwezo wa kujenga kilomita mbili za barabara za lami katika halmashauri ya mji wa Mafinga kila mwaka, hivyo baada ya miaka mitano au 10 ijayo, mitaa yote ya mji wa Mafinga itakuwa na lami kutoka kwenye chanzo kimoja cha mapato,” amefafanua Serukamba. 

Katika hatua nyingine, Serukamba ameeleza kuwa Mei 2024 walijadili kuhusu bei mpya ya vibanda 331, lakini walitii sharti la kwanza la kulipa bei mpya na kukaa katika vibanda hivyo miaka 14, huku akisisitiza alikubali kwa makubaliano kwamba wanatakiwa kulipa Sh80,000 pamoja na kusaini mikataba ya vibanda hivyo.

“Baada ya kuona hali hiyo, wafanyabaishara hao walianza kwenda kwenye maduka yao na kufungua, ni kweli tumekuta wafanyabiashara wengine wana vibanda vidogo, tumepunguza bei kutoka Sh80,000 ya awali hadi Sh70,000, Sh60,000 na wengine watalipa Sh50,000 kulingana na biashara wanazofanya,” amesema.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa soko hilo, Philinus Mgaya amesema wamefarijika kwa kitendo cha mkuu huyo wa mkoa kufika katika soko hilo, kwa sababu mvutano huo ulikuwa wa muda mrefu bila kuwa na mafanikio yoyote.

“Mei tulidhani tumefanikiwa, kumbe tulikuwa bado hatujafanikiwa kwa kile tulichokuwa tunastahiki. Tunashukuru Mungu tumefikia mwafaka wa jambo hili kwa sababu mkuu wa mkoa ameingia duka kwa duka kukubaliana namna na kiwango cha kulipa,” amesema Mgaya.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa kwa wafanyabiashara ambao bado hawajafikiwa kutokana na uelewa mdogo, amewataka wafungue maduka ili wafikie mwafaka wa namna ya kulipa kodi ya halmashauri, lakini walichelewa kuelewa suala hilo.

“Mkuu wa mkoa amesema kwa wale ambao hawajahakikiwa, waandikwe kisha atakuja kumalizia shughuli hiyo wakati mwingine, kwa sababu jambo hilo limewatesa kwa muda mrefu. Niwaombe wafanyabiashara wenzangu, tuwe na nidhamu kwa viongozi wetu na kutii kile tulichokubaliana kutekeleza,” amesema mwenyekiti huyo.

Related Posts