Kilio uhaba wa maji Dar bado kipo palepale

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha maji yanafika kwa wananchi, kilio cha ukosefu wa maji bado kinasikika mitaani katika Jiji la Dar es Salaam.

Miongoni mwa hatua hizo ni ujenzi wa visima 197 jijini Dar es Salaam vilivyofufuliwa mwaka 2022. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alivizindua visima hivyo ili kusaidiua upatikanaji wa maji ambapo wakati huo hali ilikuwa mbaya na lengo likiwa endapo maji yanayotoka mto Ruvu yatakosekana visima hivyo vinasaidia.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam waliozungumza na Mwananchi, wamesema visima hivyo havijaleta ahueni maji ya Ruvu yanapokatika na kuwafanya kusota kuyatafuta.

Wananchi hao wameitaka Mamlaka ya Maji safi na na Usafi wa mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kujenga utaratibu wa kutoa taarifa ya kukosekana kwa maji.

Hata hivyo, Dawasa nayo imewajibu kuwa nao wanatakiwa kujenga tabia ya kutoa taarifa pindi huduma ya maji inapokosekana kwa zaidi ya saa nane ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Pia Dawasa imewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kukagua miundombinu yao ya maji ili kuangalia kama kuna sehemu hazipo sawa.

Akizungumza na Mwananchi, Maimuna Issa, mkazi wa Kimara King’ong’o Kata ya Saranga amesema kukosekana kwa maji kwa wiki tatu katika eneo lao kulifanya hadi wauzaji wa maji kwa madumu kupandisha bei.

“Maji ya chumvi dumu la lita 20 lilikuwa Sh100 hadi Sh200 sasa hivi Sh300 na yale maji yasiyokuwa na chumvi dumu lilikuwa Sh300 sasa hivi ni Sh500 hadi Sh700,” amesema.

Amesema hali hiyo ni changamoto kwa wale walio na watoto wadogo ambao huhitaji kufua kila siku, kwani inaongeza gharama za maisha.

“Hata hao wauza maji wenyewe kwenye madumu walikuwa wanasema walifuata maji mbali na ndio maana walipandisha bei ili kufidia muda wanaoutumia,” amesema Maimuna.

Mbali na Maimuna, Dinah Chilahali mkazi wa Goba Center naye alilia juu ya ukosefu wa maji kwa wiki ya pili sasa bila taarifa kutolewa jambo ambalo linawapa wakati mgumu.

Amesema hali hiyo imewafanya kuanza kununua maji katika maboza,  huku wakiweka wazi kuwa hata kwa wasambazaji hao wamekuwa wakipata shida ya kusubiri kwa muda mrefu.

“Unaweza kuagiza maji saa 4 asubuhi gari ikakuletea saa 10 jioni, muda huu kama haukuwa na maji mengine ya kutumia unaishije? Tatizo pia hatuambiwi nini kinafanyika au sababu ya kukatika kwa maji ili tujiandae,” amesema Dinah.

Mbali na maeneo hayo, hali hiyo pia imewakuta wakazi wa Mbezi wanaodai kukaa wiki mbili bila huduma ya maji, huku wakazi wa baadhi ya maeneo ya Tabata wakiwa bado wanaugulia maumivu.

“Wiki mbili sasa maji hakuna, tunatumia maji ya chumvi kutoka kwa watu wenye visima na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa,” amesema Shadya Rashid mkazi wa Tabata.

Pia baadhi yao wamelalamika kuna wakati maji yanatoka yakiwa yana chumvi tofauti na yale waliyoyazoea hivyo wameshindwa kuelewa mchanganyiko wa maji hayo.

Baadhi ya wananchi walioandika kwenye ukurasa wa Instagram wa Mwananchi, wamelalamikia shida hiyo.

Carlyson Kessy ambaye ni mkazi wa Mbezi Kifuru kupitia ukurasa wa Instagram wa Mwananchi, alihoji hali ya upatikanaji wa maji Dar es Salaam na watu mbalimbali walichangia na yeye aliandika kuwa eneo lao changamoto ipo kwa sasa wamekuwa wakinunua maji kwenye magari.

“Magari dumu la lita 1, 000 ni Sh15, 000 hadi Sh20, 000. Tumepewa taarifa ni mpaka ujenzi wa pipa kubwa likamilike,” amesema.

Elizabeth Kitua aliandika:“Kinyerezi Kibaga B Kukatika maji mwezi hadi miezi ni kawaida sana tumeshazoea ni mwendo wa kununua tu na wala hatujali.”

Maelezo ya Elizabeth yaliungwa mkono na yale ya Mgome Moses ambaye amesema hali ya upatikanaji katika eneo hilo ni ya kusuasua.

“Kinyerezi maeneo ya Kibaga B kwa mwezi yanatoka siku moja tena sio siku nzima bali ni saa tatu tu ndani ya mwezi mzima tushazoea kutumia maji yetu ya chumvi siku zinaenda,” amesema Moses.

Bazaar Maye ameandika:“Huku Kata ya Kibamba upatikanaji wa maji ni majaaliwa. Kuna wakati wanafungua usiku wa manane tena kasi ndogo, yaani ukiyakosa utanunua unit moja kwa Sh20, 000, siwaelewi Dawasa.”

Malalamiko ya wananchi yanakuja zikiwa zimepita wiki mbili tangu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa kituo cha afya Kimara na ule tanki la maji la Mshikamano Septemba 18, 2024, akisema limekamilika kwa asilimia 83.

“Zamani Mbezi ulikuwa ukienda kwenye mkutano, nusu ya watu unawaona wananunua maji kwa wafanyabiashara ambayo nayo walikuwa hawana uhakika na usalama wake,” amesema.

Pia, kero hiyo inaendelea ikiwa ni takribani mwezi mmoja umepita tangu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso afanye ziara maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kujionea hali ya upatikanaji wa maji.

Ni katika ziara hiyo, aliwang’oa viongozi kadhaa wa Dawasa akiwemo, Kiula Kingu aliyekuwa Kaimu Ofisi Mtendaji Mkuu kwa madai ya kushindwa kusimamia majukumu yao. Kwa sasa anayekaimu nafasi hiyo ni Makame Bwire.

Akizungumzia uhaba wa maji katikati ya uwepo wa visima hivi, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro amesema mara nyingi huwa vinatumika pale kunapokuwa na tatizo la uzalishaji maji katika mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu.

“Visima vipo na vinafanya kazi pale ambapo kunakuwa na changamoto katika mitambo ya Ruvu Chini au Ruvu Juu kwa sababu mitambo hii inahudumia zaidi ya asilimia 60 ya watumiaji wote,” amesema Lyaro.

Kuhusu kukosekana kwa huduma ya maji katika maeneo tofauti ya Jiji la Dar es Salaam kunakolalamikiwa na wananchi, amesema changamoto anayoitambua ni ile inayohusiana na matengenezo yanayofanyika katika tanki la Changanyikeni.

Amesema matengenezo hayo ndiyo yaliyofanya watu kukosa huduma kwa saa 10 kati ya Jumatatu ya Septemba 23, 2024 saa saba mchana hadi saa 5 Usiku.

Amesema matengenezo hayo yaliathiri upatikanaji maji katika eneo la Mtipesa, West River, Down Hill, Camp Verde, Barabara ya Shule, Lastanza, Hekima, Precious, Camp Stone, Goba Hill, Sunset Close, Kachembele, Kantina, Shama, Magufull, Mji Mpya Barrier na Ng’ambo ya Mto.

 “Sehemu nyingine labda watu wajaribu kuangalia vizuri, huenda ni hitilafu binafsi, ndiyo maana tunapenda kuwasiliana na wahusika, mtu akikosa maji kwa saa nane atoe taarifa,” amesema Lyaro.

Amesema wakati mwingine hali hiyo huweza kusabaishwa na koki kujifunga bila wao kujua au watu wakawa wamekatiwa maji kutokana na wao kutolipa bili za maji hasa katika kipindi ambacho usomaji mita unafanyika.

 Novemba 2022 Dar es Salaam ilishuhudia ukosefu wa maji kwa kiasi kikubwa, Dawasa ilianza kufufua visima vyake vilivyo katika maeneo tofauti ili kuweza kufidia uzalishaji maji uliokuwa umepungua kutokana na ukame ulioshuhudiwa.

Novemba 10 mwaka huo, wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia usafishaji wa visima katika eneo la Tabata Relini na Mwananyamala Komakoma ilielezwa kuwa Dar es Salaam inavyo visima 197 vilivyochimbwa na Serikali mkoani na hadi siku hiyo visima 160 vilikuwa vimefufuliwa na kutoa lita milioni 29.4 kwa siku.

Kwa mujibu wa Dawasa maji hayo yaliunganishwa katika mfumo na hivyo kupunguza changamoto ya maji.

Akitoa hotuba ya kuahirisha vikao vya Bunge  Septemba 6, 2024 jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitoa tahadhari kwa wananchi kutumia chakula kwa uangalifu, akisema msimu ujao hautakuwa na mvua za kutosha.

Alisema utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) umeonyesha katika msimu huu wa kilimo mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024 kwenye maeneo mengi ya nchi zitanyesha chini ya wastani.

“Utabiri unaonyesha kuwa mvua zitakuwa chini ya wastani katika maeneo mengine yanayopata mvua hizo na zinatarajiwa kuanza kwa kusuasua na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,” amesema.

Related Posts