Mbinu mpya kupunguza foleni ya mizigo bandarini

Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni imeshuhudia ongezeko la kasi ya uhudumiaji wa makontena, ikihudumia takribani makontena 100,000 ya futi 20  kwa mwezi ambayo ni  karibu asilimia 50 zaidi ya ujazo uliochakatwa mapema mwaka 2024.

Ongezeko hilo, linalochochewa na kuongezeka kwa usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi ikichochewa na msimu wa mavuno.

Hali hii imesababisha miundombinu ya barabara inayounganisha bandari  kuwa na msongamano mkubwa hasa Barabara ya Nelson Mandela, njia kuu ya kuelekea bandarini.

Malori yaliyoegeshwa kando ya barabara, hasa karibu na lango nambari 4, yamesababisha msongamano mkubwa wa magari na kuathiri shughuli za uchukuzi wa kibiashara na wa umma.

Ili kupunguza tatizo hilo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliamua kuhamisha malori yaliyokuwa yameegeshwa katika Barabara ya Nelson Mandela na kuyapeleka katika eneo jipya la stendi kwenye eneo la Mamlaka ya Usafirishaji wa Bidhaa Nje (EPZA), maarufu Shimo la Udongo.

Hata hivyo, jitihada za TPA za kupunguza msongamano kwenye barabara za umma zimekabiliwa na changamoto kwani miundombinu katika eneo la EPZA imeonekana kutotosheleza na kusababisha matatizo zaidi.

Malori yanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kuingia na kutoka kwa ufanisi, na hivyo kuzidisha msongamano katika eneo la EPZA na lango la kuingilia bandari.

Kutokana na hali hiyo, msururu mrefu umetokea na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa muda mrefu kwa malori yanayosubiri kupakia au kupakua mizigo.

Zaidi ya hayo, kwa makadirio zaidi ya makontena 200 yaliachwa na meli ambazo zilipaswa kupakiwa ndani ya wiki mbili zilizopita.

Kilichoripotiwa kuchochea ucheleweshaji huo ni maagizo ya Serikali kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ‘kuyaskani’ makontena yote kabla ya kupakiwa kwenye meli.

Wakati mchakato huu unaolenga kuhakikisha usalama wa mizigo, imeripotiwa kuwa katika siku nne zilizopita uhakiki wa kuskani unaweza kuchukua hadi saa tano kwa kila kontena, na hivyo kuongeza msongamano zaidi.

Akizungumzia ucheleweshaji huo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plusdence Mbossa amesema:

 “Wamiliki wa mizigo wanahisi wanacheleweshwa, lakini wanaofanya scanning wanatimiza wajibu wao wa kuhakikisha usalama wa asilimia 100.”

Mbossa amesema katika hali ya kawaida, mchakato huo huchukua chini ya nusu saa kwa kila kontena.

“Ikichukua muda mrefu, ni nadra, na suluhu inatafutwa ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa,” amesema.

Hata hivyo, ametaja ucheleweshwaji wa sasa unatokana na ongezeko la mizigo inayopita bandarini na kuongeza kuwa TPA inashirikiana kwa karibu na wadau kutatua masuala hayo na kupunguza athari katika uendeshaji wa biashara.

“Wakati mwingine changamoto hutokea, lakini wahusika, tukiwamo sisi (TPA), tunajadili na kutafuta namna ya kuzitatua,” amesema.

Kuhusu uamuzi wa kuhamishia malori eneo la EPZA, Mbossa amesema hatua hiyo ililenga kupunguza msongamano katika barabara ya Nelson Mandela.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa DP World-Dar es Salaam, Martin Jacob, kituo cha kwanza kimekuwa kikifanya kazi kwa ufanisi jambo lililofanya makontena yanayohudumiwa kuongezeka karibu mara mbili.

Amesema msongamano wa barabara ya Nelson Mandela ulisababisha uamuzi wa kuhamishia malori eneo la EPZA.

Jacob amesema utaratibu umewekwa ili kurahisisha uhudumiaji wa malori kutoka EPZA hadi bandarini kwa lengo la kupunguza muda wa kusubiri kwa magari.

“Kwa ushirikiano wa karibu kati ya wadau, tunatarajia msongamano unaoendelea katika eneo la kuhifadhia lori la EPZA na kando ya barabara inayoelekea bandarini utaimarika hivi karibuni,” amesema.

Wakizungumzia suala hili, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Rahim Dossa ameelezea athari za ucheleweshaji huo kwa waendesha malori.

Amesema kutokana na msongamano huo wamiliki wa malori wamelazimika kupunguza safari wanazoweza kufanya bandarini kila siku.

“Pale ambapo tulikuwa tunafanya hadi safari tano kwa siku, sasa tumeshuka hadi moja au mbili,” amesema.

Si hivyo tu, wasafirishaji pia wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na ucheleweshaji huo ambapo Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Elitunu Mallamia amebainisha bandari hiyo inakabiliwa na uhaba wa eneo hasa katika msimu wa mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi.

Amesema msongamano huo unachangiwa na wingi wa mizigo ambayo haijatolewa bandarini kutokana na msongamano wa magari katika barabara za umma.

Malamia amesisitiza kuwa mchakato wa uhakiki wa asilimia 100 ulioagizwa na Serikali pia unapunguza kasi ya shughuli za biashara, huku malori yakitumia muda mwingi kuingia bandarini.

Lakini alionyesha wasiwasi kuwa ucheleweshaji huo unaweza kusababisha wauzaji bidhaa nje kukosa madirisha muhimu ya soko.

“Kwa mfano, bidhaa kama maharagwe zinazopelekwa katika masoko ya Asia, hasa India, yanaweza kuchelewa msimu wao wa mauzo kutokana na ucheleweshaji huu,” ameeleza.

Katika hilo, Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema hivi karibuni kulikuwa na kikao na wadau wanaohusika na usafirishaji wa mizigo inayoingia na kutoka , suluhu ilikuwa kufikiwa kwa ushirikiano.

“Washiriki wa mkutano huo ni pamoja na TPA, TRA, TASAC, TATOA, TAFFA, DP World, na wengineo tunaendelea kufuatilia kwa pamoja ili kuhakikisha mizigo inaondolewa haraka wakati wote,” amesema.

“Hali itakuwa nzuri baada ya siku chache. Tumekubaliana makontena yataruhusiwa kupanda meli hata kabla ya ripoti kukamilika, ili kuharakisha usafirishaji wa makontena ndani ya vituo,” amesema.

Related Posts