Shule zageuzwa ‘madanguro’ Dar | Mwananchi

Dar es Salaam. Kutotekelezwa kikamilifu kwa Mwongozo wa Malezi, Unasihi na Ulinzi wa Mtoto kwa Shule na Vyuo vya Ualimu Tanzania wa mwaka 2020, kunahatarisha usalama na  afya kwa wanafunzi, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Mbali na hilo, hali hiyo pia inachangia kuwapo kwa mmomonyoko wa maadili miongoni mwa wanafunzi.

Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari wa Mwananchi kwa takribani miezi mitatu katika shule tisa za msingi na sekondari katika wilaya za Ilala, Ubungo na Temeke, jijini Dar es Salaam umebaini kutotekelezwa kwa mambo mengi ya msingi ya mwongozo huo, hivyo kuweka rehani maisha na makuzi ya mamia ya watoto hao.

Darasa mojawapo la Shule ya Sekondari Kisungu likiwa wazi usiku

Shule hizo ni Jica iliyopo Tabata, Yangeyange, Msongola Mpya na Sekondari za Kisungu na Ari zilizopo wilayani Ilala. Pia zipo shule za msingi Malamba Mawili na Makoka na Sekondari ya Makoka zilizoko wilayani Ubungo na Shule ya msingi Temeke iliyopo wilayani Temeke.

Madirisha na milango ya shule hizo hayafungwi, hakuna ulinzi wala taa, hivyo kutoa mwanya kwa baadhi ya watu kutumia kasoro hizo kufanya vitendo visivyoendana na maadili, ikiwamo kugeuzwa kuwa madanguro.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Ubungo, Aron Kagurumjuli, licha ya kusema hajapata taarifa kuhusu shule kugeuzwa eneo la kufanya vitendo visivyoendana na maadili, ameahidi kufanya uchunguzi. “Tukibaini kuna ukweli, tutachukua hatua stahiki,” amesema.

Wakati Kagurumjuli akiahidi uchunguzi, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema kuna mpango wa kujenga ukuta kwenye shule zote wilayani humo, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

Kifungu cha 5.2.1 cha sura ya tano ya mwongozo huo wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kinasema: “Wazo la ulinzi wa mtoto shuleni limefungamana na ujenzi wa mazingira salama shuleni, ili kuondoa hofu na kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia.”

Dhana ya mazingira salama inamaanisha na kujumuisha eneo kunakofanyika  ufundishaji kuwe katika mazingira yenye utulivu.

“Usalama shuleni humsaidia mwanafunzi kujifunza kwa furaha na hivyo kujiimarisha kimwili, kisaikolojia, kijamii na kitaaluma.

“Mazingira salama na tulivu shuleni humjengea mwanafunzi mazingira chanya ya kujifunzia na kufundishia na kuhakikisha anakuwa na mahudhurio ya kuridhisha, mwenendo unaofaa na mafanikio bora ya kitaaluma,” inaeleza sehemu ya kifungu hicho.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, ili kupata mafanikio hayo ni muhimu kuwepo na mipango ya kuzuia na kukabiliana na vihatarishi mbalimbali katika shule na jumuiya zake.

Oktoba 8 mwaka jana, Mwalimu Mkuu wa Msongola Mpya, Mabruki William alikaririwa na gazeti hili akisema kumekuwa na mwingiliano mkubwa na jamii shuleni hapo, jambo linalowanyima wanafunzi utulivu wanapokuwa darasani.

“Kwetu kukosekana kwa uzio ni changamoto kubwa, kwani wapita njia wamekuwa ni sehemu yao ya kujidai na kusahau kuwa ni eneo la shule. Wakati mwingine wanapita kwa kupiga kelele, bodaboda nao wanawasha muziki mkubwa, watoto badala ya kusoma wanaanza kuimba wimbo uliowekwa,” alisema Mabruki.

Hakuishia hapo, mwalimu Mabruki alisema, “kuwepo kwa uwanja katika eneo la shule ambao unatumiwa na wananchi imekuwa ni chaka la maovu, kwani si sehemu zote kuna taa za kuwafanya kuonekana, hivyo kutoa mwanya kwa watu hao kufanya kile wanachojisikia.”

Mwalimu Mabruki alisema imefikia hatua hata miundombinu ya shule hiyo inatumiwa pia na jamii, ikiwamo vyoo achilia mbali wizi wa mara kwa mara unaorudisha nyuma maendeleo ya shule yake.

Mwananchi akikatiza eneo la shule ya Sekondari Kisungu iliyopo Kinyerezi, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam huku masomo yakiwa yanaendelea.

“Tumeshaibiwa mashine ya kupandishia maji, koki za mabomba, pia watu wanakuja kujisaidia kwenye vyoo vya shule kitu ambacho si sawa. Wakati mwingine wanaacha vyoo vichafu watoto wanakuja kusafisha,” alisema.

Hayo tisa, kumi ni vitendo vinavyoendelea baada ya muda wa masomo. Mwalimu Mabruki alikaririwa akisema kwa madarasa yasiyo na milango, wapo watu wanaoyatumia kumalizia haja zao za kimapenzi na wakati mwingine husahau nguo na kinga, vitu ambavyo watoto hukutana navyo asubuhi.

Hayo hayapo Msongola pekee, mkazi wa Kinyerezi, Amanda Sanga alisema amewahi kushuhudia katika Shule ya Sekondari Kisungu, watu waliotoka kwenye starehe wakiingia kumaliza haja zao za kimwili kwenye maeneo ya shule.

“Kuna vitu vinafanyika kwenye mazingira ya shule hadi tunajiuliza, hivi hakuna usimamizi kuzuia vitendo hivi vinavyoweza kuathiri watoto wetu?” alihoji.

Tatizo hilo halikuishia katika shule hizo pekee, kwani dereva wa bodaboda eneo la Riverside- Ubungo, Jumanne Kambaulaya alisema amewahi kukuta watu wakifanya mapenzi usiku katika eneo la shule za Makoka.

Alisema kuna wakati bodaboda huegeshwa katika shule hizo na wahusika kuingia vichakani jirani na shule kumaliza haja zao.

Mkazi wa Temeke, Frank Kasambala alisema hadi maeneo ya shule kutumika kwa mambo maovu, kuna mahali uongozi wa shule na serikali za mtaa haufanyi kazi yake ipasavyo.

“Wananchi wanachangia pesa za ulinzi shirikishi, kwa maana ya kukagua na kulinda usalama na hii haichagui maeneo ya kulinda,” alisema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makoka, Justine Geregeza alisema wanashirikiana na walinzi shirikishi kuhakikisha usalama katika maeneo ya shule.

“Hatujapata kesi za aina hiyo, lakini tunatoa maelekezo kwa watu wanaopotea njia kuhakikisha wanajua mwelekeo sahihi,” alisema Geregeza.

Julai 15, mwaka huu, Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Temeke, Bakili Makele alikaririwa na Mwananchi akisema, “miaka ya nyuma niliomba kwa mfadhili tukajenga ukuta. Hivi sasa kuna maeneo ya uzio yamebomoka, hivyo watu wanatumia mwanya huo kufanya mambo yao. “katika Shule ya Msingi Temeke hili lipo si la kuhadithiwa. Lazima tujenge ukuta kuimarisha usalama.”

Julai 25 mwaka huu, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mtambani, Tabata, Nora Muya aliieleza Mwananchi kwamba kumekuwa na matukio ya vitendo viovu katika Shule ya Msingi Jica.

Alisema licha ya kupatiwa Sh15 milioni kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la Segerea kwa ajili ya ujenzi wa ukuta, fedha hizo hazikusaidia kitu, kwani haukuzungushwa eneo lote la shule.

Ramadhani Ally, Mkazi wa jijini Dodoma alisema aliwahi kutolewa na mlinzi katika kiwanja kilichopo kwenye moja ya shule, akiangalia mazoezi ya jioni akielezwa muda wa mazoezi umekwisha, hivyo anapaswa kuondoka.

“Nilishangaa, ananiambia najua upo peke yako, lakini siwezi kukuamini kuendelea kukaa hapa, kwani mnajifanya kushangaa mazoezi baada ya hapo mnaita wapenzi wenu mnatuachia kondomu hapa,” alisema Ally.

Mwalimu aliyezungumza kwa sharti la kutokutajwa jina kutoka Manispaa ya Ubungo, amesema kutokuwapo kwa ulinzi na uzio kunachangia kwa kiasi kikubwa maeneo ya shule kutumika vibaya.

“Mungu anawalinda watoto wetu, lakini vitendo vibaya vinafanyika na hatujui dhamira ya wanaovifanya,” amesema na kuongeza kuwa kuna wakati watoto huokota kondomu zilizotumika katika maeneo ya shule wakifikiri ni puto.

“Tunajitahidi kuwaelekeza watoto kutookota vitu ovyo,” amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Yangeyange, Mrisho Goha amesema kamati za shule zinawajibika kushughulikia changamoto kama hizo na kutoa taarifa kwa maofisa elimu, ikiwa zinashindwa kuzitatua.

Pengine hilo la kutotolewa kwa taarifa ndilo lililomfanya Mratibu wa Elimu Kata ya Kinyerezi, Radhia Mfalingundi kama ilivyokuwa kwa Kagurumjuli, kusema hana taarifa za shule kutumika kama madanguro na kuahidi kufanya utafiti kuhusu suala hilo.

Mlinzi katika shule moja iliyopo Tabata, Samwel Yohana amewatupia lawama wazazi kuchangia kuwapo kwa mambo hayo usiku, “wazazi wanapogoma kutoa michango ya ulinzi, wanatutia majaribuni. Mtu akikupa Sh5,000 au Sh10,000 huwezi kumpeleka Polisi,” amesema akieleza baadhi huwaruhusu watu kutimiza haja zao za mwili shuleni baada ya kulipwa.

Septemba 20, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda aliieleza Mwananchi kuna mpango wa kuzungusha ukuta kwenye shule zote wilayani humo, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Mpakani, Mabibo, Msafiri Mwajuma amesema walishachukua hatua kudhibiti tatizo hilo. Waliamua kuweka uzio wa mabati, ili kuimarisha usalama wa watoto. “Tulifanya hivyo baada ya kuona matukio yasiyofaa yameongezeka.”

Mmoja wa viongozi waandamizi serikalini aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina, amesema, tatizo hilo halipo kwa shule za Dar es Salaam pekee, bali karibu nchi nzima.

“Unajua hili suala ni kubwa, ukienda huko mikoani, shule ambazo hazina uzio ni nyingi na kama hakuna uzio ni ngumu kuzuia vitendo viovu kufanyika, hususan nyakati za usiku na wikiendi, watu wanaingia tu na kufanya wanachokifanya kisha wanaondoka,” amesema na kuongeza;

“Kwa sababu teknolojia imekuwa, basi kama hakuna uzio kutokana na gharama kubwa, zifungwe kamera za CCTV ambazo zitafuatilia matukio yote na hii inawezekana, kwani shule nyingi zimeunganishiwa umeme, hivyo ufanisi wa kamera unaweza kuwa suluhisho kuzilinda shule na watoto wetu.”

Related Posts