Watoto wawanyooshea kidole wazazi, matukio ya ukatili dhidi yao

Arusha. Wazazi na walezi wametajwa kuwa chanzo cha kushamiri kwa matukio ya ukatili kwa watoto kutokana na kutelekeza majukumu yao ya malezi na kutumia muda mwingi kusaka fedha na mali.

Pia, viongozi wa dini wamenyooshewa vidole kupwaya katika mafundisho yao ya kidini yenye uwezo wa kutengeneza hofu ya utekelezaji wa matukio hayo ya ukatili, badala yake baadhi yao wamekuwa wakisaka fedha zaidi kwa huduma za maombezi na uponyaji.

Hayo yamebainishwa leo Jumapili Septemba 29, 224, kwenye mahubiri, nyimbo na mashairi mbalimbali yaliyowasilishwa na watoto kwenye maadhimisho ya siku ya ‘Malaika Mikaeli’  mbele ya waumini na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Engarenarok.

Akizungumza katika mahubiri yake, mtoto Junior James (12) amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakitumia muda mwingi kusaka fedha, mali na heshima machoni pa watu na kusahau kutenga muda kidogo kwa ajili ya malezi ya watoto wao.

 “Majukumu haya mmewaachia wadada wa kazi na ndugu zenu wa karibu mnaowaamini lakini mjue yako mengi tunayokabiliana nayo ambayo tunataka kuwaambia lakini tunakosa muda,” amesema Junior na kuongeza:

“Baadhi ya mambo haya wamekuwa wakitekeleza hao walezi mliowaamini na tumekuwa tukiangukia mikono isiyo salama na kujikuta wahanga wa matukio ya ukatili, wakati nyie mkipambana kututunza badala ya kutulea.”

Mbali na hilo, amesema kuwa vitendo vya ulevi, anasa na mavazi yasiyo na heshima wanayoshuhudia yanavaliwa na idadi kubwa ya watu wazima, yamekuwa ndio kama malezi yao na kutamani kuyavaa na kuyaishi kumbe yanawapotosha ukubwani.

Katika mashairi waliyoimba watoto wengine, wamewashutumu pia baadhi ya wazazi kutangatanga kwenye makanisa na mikutano ya watu wanaojiita manabii na mitume kusaka upako na uponyaji.

“Mnaacha makanisa yenu ya asili, mnakimbilia mahema ya watu wanaojiita manabii na mitume na bahati mbaya mnatupeleka na sisi watoto wenu kila siku kuombewa, huku ni kutuyumbisha na mwisho kutukosesha imani ya kweli kisa kusaka miujiza ambayo baadhi inatokana na nguvu za giza,” imesema sehemu ya shairi hilo.

Katika moja ya ngonjera, Gloria Siku amesema viongozi wa dini wamekuwa wakisaka fedha kupitia dini na kuacha njia njema ya malezi na kujenga imani ya Mungu kwa waumini na kutumia nguvu za giza, ambazo huagizwa kutekeleza matukio ya ukatili.

“Mmeacha njia ya kweli ya kurudisha imani na hofu ya kutenda dhambi sasa mnahamasisha na zaidi baadhi yenu mmekuwa mkiwatoza waumini  fedha za maombi ya uponyaji kwa kigezo cha mapepo makubwa na madogo ili kutofautisha viwango vya malipo.

“Tunaomba tumrudie Mungu wa kweli maana hadi ndugu zetu sasa tunawaogopa si wanaume wala wanawake kuishi nao, kutokana na matukio ya kila kukicha tena wakitutisha kwa vipigo na kifo,” wamesema watoto hao.

Happy Mosha (11) katika moja ya ngonjera, amesema matukio ya ukatili na mauaji waliokuwa wanatazama kama sinema sasa yamekuwa yakitikisa kila kona ya nchi na kuzua hofu kubwa kwao.

“Hivi tumewakosea nini lakini, Ee Mungu tunusuru na watu hawa, lakini kinachosikitisha baadhi ya mama zetu na baba wamekuwa wakitutekeleza pia, hivi uchungu wa kutuzaa umeishia wapi, tunaomba jamii mtulinde kwa hatma ya Taifa la kesho,” amesema.

Mwalimu Mkuu wa shule ya mafundisho ya kidini ya Jumapili kwa watoto katika kanisa hilo, Hyness Mbasha amesema Siku ya Mikaeli kwa watoto ni sherehe ya kidini inayoadhimishwa na Wakristo, ili kumuenzi Malaika Mkuu Mikaeli pamoja na malaika wengine kwa kuhusishwa na vita kati ya mema na mabaya.

“Siku hii ambayo huadhimishwa Septemba ya kila mwaka, mara nyingi inakuwa na maana ya sherehe ya ushindi wa mema, ujasiri, na kutetea haki. Pia, inafundisha watoto umuhimu wa kuwa na nguvu ya ndani na ujasiri wa kukabiliana na changamoto,” amesema Mbasha.

Related Posts