BAADHI ya wadau wa soka jijini hapa wamemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano kujiuzulu nafasi hiyo, huku wakiliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumchukulia hatua kwa kumuita katika Kamati ya Maadili na kuitisha uchaguzi mkuu wa chama hicho kwa mujibu wa katiba.
Wadau hao wakiwemo viongozi wastaafu wametoa wito huo leo Septemba 29, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza na kusoma barua waliyoliandika TFF na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na nakala kwa wadau mbalimbali wakiishtumu MZFA kwa kuvunja katiba na kushindwa kufanya uchaguzi mkuu, kuitisha mikutano na vikao vya kamati tendaji na mkutano mkuu kwa miaka minne sasa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Soka Wilaya ya Nyamagana (NDFA), Munga Lupindo, amesema wamemuomba Katibu Mkuu wa TFF amwamuru Mwenyekiti huyo apishe ofisi na kupelekwa Kamati ya Maadili ya TFF kwa hatua zaidi na kuitisha uchaguzi mkuu ambao kikatiba ulipaswa kufanyika Julai, mwaka huu.
Lupindo amesema nia ya wadau hao ni njema kwa mustakabali wa maendeleo ya soka la Mkoa wa Mwanza na hawaridhishwi na namna uongozi wa MZFA unavyokiuka katiba kwani tangu ulipoingia madarakani Julai, 2020 umeitisha kikao kimoja tu Oktoba 17, 2020 licha ya kutakiwa kuitisha mkutano mkuu na ule wa kamati tendaji mwaka 2021/2022 na 2023/2024 ili kusoma taarifa za mapato na matumizi na kupitisha mipango ya maendeleo.
“Mpira wetu wa Mwanza unaburuzwa na chama cha mkoa ambacho kinavunja katiba na viongozi mpaka sasa hawapo kihalali na kwa mantiki hiyo MZFA haina Mwenyekiti halali na kwa mujibu wa katiba anapaswa kujiuzulu. Tunaomba kamati ya maadili ya TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Rais, Wallace Karia aone namna ya kulishughulikia hili,” amesema Lupindo na kuongeza;
“Na Mwenyekiti (Vedastus Lufano) afikishwe kamati ya maadili kwa makosa ya uongozi anayoyafanya anaongoza mpira kwa maslahi yake binafsi na kusigina katiba, hii siyo afya kwa mpira wetu tunaomba hatua zichukuliwe mapema kwasababu viongozi hawa wanaburuza tu watu.”
Mdau wa soka jijini hapa, Franklin Kamalamo amesema kutokana changamoto hiyo kumekuwa na mpasuko mkubwa katika soka la mkoa huo na kufanya timu mbalimbali ikiwemo Pamba Jiji zishindwe kupata msaada huku vyama vya soka wilayani na klabu zake zikikiuka katiba baada ya kushindwa kusimamiwa vyema na uongozi wa juu wa MZFA ambao pia unasigina katiba yake.
“Hakujafanyika mikutano ya dharura na ile ya kila mwaka ya kikatiba tafsiri nyepesi ni kwamba kama hawafanyi basi hawapo kihalali, tunafanya hivi kuwaambia kwamba wastuke muda bado upo watimize wajibu wao waitishe mikutano na washirikishe wanachama na wadau katika maendeleo ya soka lakini kama hakuna mkutano wowote unaoelezea masuala haya maana yake tunakwenda kama vipofu na tutatumbukia katika shimo,” amesema Kamalamo.
Mwenyekiti wa Chama cha Makocha (TAFCA) Mkoa wa Mwanza, Kessy Mziray amesema yeye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya MZFA, kwa mujibu wa katiba lakini mwaka jana aliondolewa na kutoshirikishwa mambo mengi ikiwemo kozi za makocha baada ya kutoelewana na Mwenyekiti wa chama hicho, Vedastus Lufano, huku akiomba chama hicho kifuate katiba, kiwaunganishe wadau badala ya kujenga matabaka na kuwaadhibu watu wasiowaunga mkono.
Dominic Masumbuko kutoka wilayani Sengerema, amesema; “Mwenyekiti ana shida hataki kushirikisha wadau wa mpira ambao ni wajumbe kwahiyo tunaiomba TFF imuite Mwenyekiti aeleze shida ni nini? Mkoa wa Mwanza ni mkubwa unapaswa kuwa mfano kwenye maendeleo na uongozi wa soka lakini hali haiko hivyo,”
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano alipotafutwa kuzungumzia madai hayo amesema hayuko tayari kuzungumza chochote kwani yuko safarini jijini Dar es Salaam, huku akifafanua kuwa tuhuma za kutosaidia timu za Mwanza siyo za kweli kwani hata jana (Jumamosi) alikuwa uwanjani Azam Complex kuiunga mkono Pamba Jiji ikicheza na Coastal Union.