BAO la penalti ya utata lililofungwa na kiungo mshambuliaji, Charles Ahoua dakika ya 63, limetosha kuipa Simba pointi tatu muhimu mbele ya Dodoma Jiji katika pambano la Ligi Kuu Bara lililopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Mara baada ya mchezo huo mashabiki wa soka waliijadili penalti hiyo na ushindi huo wa Simba, lakini mashabiki wa klabu hiyo walijibu mapigo kwa kusisitiza ‘muhimu pointi tatu’, baada ya timu hiyo kufikisha ushindi wa nne mfululizo katika ligi hiyo ikipanda nafasi ya tatu na alama 12.
Penalti hiyo iliyoipa ushindi wa 100% Wekundu hao msimu huu na mbele ya Dodoma, ilitokana na baada ya beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kufanyiwa madhambi eneo la hatari na kiungo wa Dodoma, Salmin Hoza na mwamuzi wa Tanga, Omary Mdoe kuipatia penalti.
Hata hivyo, marudio ya Azam TV ilionekana wazi Hoza akiucheza mpira kuutoa nje na Tshabalala kama aliyejiangusha na kujifanya kuumia, lakini alipotolewa nje kwa machela aliinuka chapu kuonyesha ‘alizuga’, lakini haikubadilisha kitu kwani Ahoua aliandika bao lake la pili msimu huu na la 10 kwa timu hiyo.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids alifanya mabadiliko mawili katika mchezo wa jana tofauti na kikosi kilichoifunga Azam mabao 2-0 mechi iliyopita iliyopigwaUwanja wa New Amaan Zanzibar.
Maeneo yaliyofanyiwa mabadiliko ni beki wa kulia, alipomuanzisha Kelvin Kijili nafasi ya Shomari Kapombe na kiungo mshambuliaji, Joshua Mutale akimpisha Mganda Steven Mukwala ili kusaidiana na Leonel Ateba.
Hata hivyo, licha ya Simba kuanza na mastraika wawili bado nyota hao walishindwa kufanya kazi kwa ufanisi hali iliyosababisha Mukwala kutolewa kipindi cha pili kumpisha kiungo Awesu Awesu.
Licha ya Simba kutawala mchezo, ilikosa utulivu eneo la mwisho la umaliziaji eneo lililochezwa na Mukwala, Ateba, Debora Mavambo na Ahoua kabla ya mabadiliko ya kipindi cha pili.
Dodoma iliyoongozwa na mabeki wa kati, Augustino Nsata na Joash Onyango ilifanya makosa mengi kipindi cha kwanza yaliyosabisha namba kubwa ya viungo na washambuliaji wa Simba kusababisha hatari nyingi kwa kipa, Alain Ngeleka.
Kocha wa Dodoma, Mecky Maxime hesabu zake zilianza kutibuliwa mapema baada ya kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Ibrahim Ajibu kupata majeraha dakika ya 20 na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na Paul Peter.
Mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa yalionekana wazi kuiathiri Dodoma Jiji kwani hakukuwa na kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kutoa pasi za mwisho kama Ajibu ambazo zingesaidia washambuliaji walioanza wakiongozwa na, Waziri Junior Shentembo.
Kitendo hicho kilimfanya Mecky kucheza kwa tahadhari na kuongeza idadi kubwa ya viungo ili kusaidiana na Apollo Otieno na Salmin Hoza.
Dodoma licha ya kupoteza, lakin imekuwa ni timu ya kwanza msimu huu kuizuia Simba isipate bao katika kipindi cha kwanza katika Ligi, kwani katika mitatu mfululizo chini ya Fadlu, Simba ilikuwa haimalizi kipindi cha kwanza bila ya kufunga bao, jambo linaloonyesha ilikutana na mchezo mgumu na wenye kuvutia.
Tangu Dodoma Jiji ipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-2021, haijawahi kuifunga Simba kwani katika michezo tisa ambayo zimekutana imepoteza yote.
Kwa mara ya kwanza timu hizo zilianza kukutana Februari 4, 2021 ambapo Simba ilishinda mabao 2-1, yaliyofungwa na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Meddie Kagere na Bernard Morrison huku lile la Dodoma Jiji likifungwa na Cleophace Mkandala.
Katika michezo hiyo, Simba imefunga jumla ya mabao 16 huku kwa upande wa Dodoma Jiji ikifunga mawili tu yaliyofungwa yote na Cleophace Mkandala akianza mechi ya Februari 4, 2021, Dodoma ilipochapwa 2-1, na Aprili 27, 2021, ikipoteza 3-1.
Mchezo wa mwisho kwa timu hizo kukutana ulipigwa pia kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ambapo Simba ilishinda kwa bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Freddy Michael Kouablan, mechi iliyopigwa Mei 17, mwaka huu.
Simba chini ya kocha mpya, Fadlu Davids imeshinda michezo yote minne ya Ligi Kuu Bara hadi sasa aliyoiongoza baada ya kuifunga Tabora United mabao 3-0, Agosti 18, akaichapa Fountain Gate 4-0, Agosti 25 na 2-0 mbele ya Azam FC Septemba 26.
DODOMA: Alain Ngeleka, Augustino Nsata, Apollo Otieno, Salmin Hoza, Dissan Galiwango, Mwana Kibuta, Joash Onyango, Dickson Mhilu, Waziri Junior/ Hassan Mwaterema, Ibrahim Ajibu/ Paul Peter, Iddi Kipagwile/ Reliants Lusajo.
SIMBA: Moussa Camara, Kelvin Kijili/ Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Abdulrazack Hamza, Che Malone Fondoh, Fabrice Ngoma/ Augustine Okejepha, Kibu Denis/ Edwin Balua, Debora Fernandes, Leonel Ateba, Jean Charles Ahoua/ Valentin Nouma, Steven Mukwala/ Awesu Awesu.