HALI ya Kagera Sugar sio nzuri, kwani juzi imepoteza mechi ya nne kati ya sita ilizocheza katika Ligi Kuu Bara ya msimu huu na jambo hilo limewashtua baadhi ya wachezaji na mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Ibrahim Mohamed waliodai sio hali ya kawaida, lakini wakawatuliza mashabiki wakisema timu hiyo inahitaji muda wa kutulia.
Kagera imeshinda mechi moja na kutoka sare moja, huku ikikubali vichapo vinne na kukaa nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi nne, juu ya vibonde KenGold wenye pointi moja tu baada ya mechi tano, ikifunga mabao matatu na kufungwa saba hadi sasa, jambo lililomshtua CEO Ibrahim.
Akizungumza na Mwanaspoti, kigogo huyo alisema, ni kweli timu hiyo haijaanza vizuri na hata wao inawashtua kwa vile matarajio na malengo ni makubwa, lakini hakuna namna zaidi ya kuipa muda kwani ni timu mpya na ina kocha mpya vilevile.
Alisema hofu yao ni kwamba kama timu itaendelea hivyo na ushindani ulivyo mkali basi kuna uwezekano wa kumaliza vibaya.
“Tumeumia kupoteza japo tuna timu mpya ila hiyo sio sababu, ndio maana tunasubiri sana muda wa mapumziko ya kupisha timu za Taifa ufike ili tujenge palipobomoka,” alisema mtendaji huyo na kuongeza;
“Tunakwenda kuangalia ni wapi tuboreshe lakini pia kukaa na wachezaji kuwajenga kisaikolojia ili turudi kwenye ligi kumaliza nusu na robo ya mechi zilizobakia.”
Msimu uliopita, Kagera iliyopanda daraja mwaka 2005, ilimaliza katika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 34, ikishinda mechi saba, sare saba na kupoteza 10 na kwa sasa ipo chini ya kocha Paul Nkata kutoka Uganda.
Mmoja wa mastaa wa timu hiyo, Abdallah Mfuko amekiri kuwa timu hiyo ipo katika hali mbaya na wao kama wachezaji hawaelewi shida ni nini, ila wameahidi kupambana ili kuinusuru kwa mechi zilizo mbele yao.
Kagera ilipoteza mbele ya Singida BS (1-0), Yanga (2-0), Fountain Gate (3-1) na Tabora United (1-0) kisha kushinda 2-0 dhidi ya KenGold na kutoka sare na JKT Tanzania, kitu kimemfanya beki huyo kusema kama wachezaji hawatambui kitu gani kinachowaangusha kwani wanapambana sana uwanjani lakini matokeo mazuri yanawakataa, ila watarudi upya katika mchezo ujao
“Kile tunachoelekezwa ndio tunachokifanya lakini matokeo sio rafiki upande wetu tunatakiwa kukaa chini ili kujipanga upya kwa mechi zilizobaki,” alisema Mfuko na kuongeza;
“Msimu umeanza vibaya pointi nne kwenye mechi sita ni nyingi tulizozidondosha tutakaa kama wachezaji kujitafakari na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ushindani kwenye michezo iliyo baki.”
Mfuko alisema hata wao wanaumizwa na matokeo hayo na wamekuwa wakijipa imani kuwa bado wana nafasi ya kufanya vizuri licha ya changamoto inayowakabili kwa sasa.
“Pamoja na kuanza vibaya matarajio yetu ni kumaliza ndani ya nafasi tano za juu, hilo linawezekana kama tutawekeza nguvu kwa pamoja viongozi kukaa na sisi kujua nini shida na kujenga umoja kati yetu,” alisema.