Okutu, Mpole wana vita Pamba Jiji

MSHAMBULIAJI wa Pamba, Mghana Eric Okutu amesema hafurahishwi na mwenendo wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara hadi sasa, huku akiweka wazi ana kazi kubwa ya kufanya ili kupambana kucheza kikosi cha kwanza na nyota mwenzake, George Mpole.

Nyota huyo amejiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na Tabora United aliyojiunga nayo mara ya kwanza msimu wa 2023-2024 akitoka Hearts of Lions ya Ghana na akiwa na kikosi hicho cha Nyuki wa Tabora, alikifungia mabao saba ya Ligi.

“Msimu uliopita nilipata nafasi zaidi ya kucheza katika kikosi cha kwanza tofauti na sasa ambapo ushindani ni mkubwa kwa kila mmoja wetu, hii ni changamoto kubwa kwangu ya kupambana ili niwe bora kuliko msimu uliopita,” alisema Okutu na kuongeza;

“Unapocheza timu yenye washambuliaji wengi wazuri na bora kama Mpole na wengine ni lazima upambane na uonyeshe utofauti ambao utasababisha benchi la ufundi kukutumia, muhimu kwangu ni kutumia vizuri nafasi pale nitakapoendelea kuaminiwa.”

Kwa upande wa kocha mkuu wa Pamba, Goran Kopunovic ambaye alimsajili mchezaji huyo baada ya kufanya naye kazi wakiwa na Tabora United alisema, timu hiyo ina wachezaji wengi bora na kila mmoja pia anastahili kucheza hivyo ni suala la nafasi tu.

Okutu amekutana na George Mpole aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na FC Lupopo ya DR Congo huku akikumbukwa msimu wa 2021-2022 alipokuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa kufunga mabao 17, akiwa na Geita Gold.

Related Posts