Mwanafunzi asimulia alivyotoka shule akakuta sherehe ya ndoa yake nyumbani

Nzega. “Niliambiwa nikaoge ili nije kutambulishwa kwa mume wangu, nilizunguka nyuma ya nyumba na kukimbilia porini hadi usiku, ndipo nikarudi nyumbani, mama alinipiga sana siku hiyo.” Hii ni sehemu ya simulizi ya maumivu ya binti wa miaka 17, Jane Mayunga, aliyenusurika kuozeshwa akiwa na umri wa miaka 14.

Jane, mtoto wa pili kati ya saba kwa mama yake, anaeleza namna mzazi wake huyo alipotaka aache shule akiwa darasa la saba, ili aolewe kwa mwanaume aliyetafutiwa mwaka 2021.

“Mdogo wangu alifanyiwa hivyo hivyo, akaacha shule na kuolewa Mwanza. Mimi sikukubali, nilienda kushtaki kwa mwalimu mkuu,” anasema.

Jane ni miongoni mwa mabinti walionusurika kuozeshwa katika umri mdogo mkoani Tabora.

Mkoa huo, unatajwa wa pili kwa kuwa na matukio ya ndoa za utotoni nchini, kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS) za mwaka 2015/16, ukiwa na asilimia 58 baada ya Shinyanga inayoongoza kwa asilimia 59,  Mara ni ya tatu (asilimia 55) na Dodoma asilimia 51.

Akizungumza kwa sauti iliyojaa ujasiri, Jane ambaye sasa yupo kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Isagenhe iliyopo Kijiji cha Buhulyo, Kata ya Isagenhe, Wilaya ya Nzega Vijijini, anasema mama yake hakutaka asome, hadi kufika sekondari, lakini amefika hapo kwa ubishi wake.

“Nilipambana, mama hakutaka kunihudumia chochote kinachohusu shule, ukizingatia katika familia yetu mimi peke yangu ndiye nimefika sekondari, wadogo zangu baadhi wameolewa,” anasema Jane ambaye ni mtoto wa pili kati ya saba kwa mama yake.

Binti huyo anasema hakuwahi kumfahamu baba yake, alilelewa na mama ambaye hakuamini katika elimu, hasa kwa mtoto wa kike, hivyo akawa analazimisha waolewe katika umri mdogo.

“Hadi namaliza darasa la saba ilikuwa ni bahati tu, nilitafutiwa mchumba, ikaandaliwa sherehe nyumbani bila mimi kuambiwa. Nilitoka shuleni na kuambiwa niende nikaoge nije kuonyeshwa mume wangu, nilizunguka nyuma ya nyumba na kukimbilia porini hadi usiku sana.

Anasema, sherehe ya kifamilia iliyoandaliwa nyumbani kwao haikuisha vizuri kufuatia yeye kutoroka.

“Niliambiwa mama alirejesha ng’ombe 15 alizokuwa amepewa kama mahari yangu. Mimi nilipotoka porini nilikwenda kwa bibi akanifukuza, ikabidi nirudi nyumbani, mama na kaka walinipiga sana, nikaona njia pekee ni kumweleza mwalimu mkuu, aliyekuja nyumbani na kutoa onyo nisiozeshwe. Kuanzia hapo ikawa kama nimejichongea kwani mama alikataa kunihudumia,” anasema.

Afanya vibarua kununua sare

Anasema hadi anafanya mtihani wa mwisho wa darasa la saba, nyumbani hakuwa anaachiwa chakula, hivyo akawa analazimika kula mlo mmoja pekee wa usiku pamoja na wengine.

“Nililazimika kufanya vibarua kwenye mashamba ya mpunga, nikawa natunza pesa nilizolipwa hadi zikafika Sh60, 000 wakati huo nikiwa mwanafunzi wa darasa la saba hadi nilipofanya mtihani na kuhitimu,” anasema.

Anasema matokeo yalipotoka alikuwa miongoni mwa waliochaguliwa kujiunga na sekondari, mzazi wake hakujali, ndipo akatumia fedha alizopata kwenye vibarua vya mpunga kununua sare za shule, sweta na madaftari.

“Pesa hazikutosha kununua viatu, hivyo nikawa naenda shule na ndala, walimu walinivumilia.  Sasa nipo kidato cha tatu, kidogo ugumu umepungua kwa kuwa hivi karibuni nilipata msaada wa vifaa vya shule na baiskeli kwa ajili ya usafiri kutoka shirika la Msichana Initiative.

Shirika hilo ni miongoni mwa mashirika 87 ya Mtandao wa Kupinga Ndoa za Utotoni yanayopaza sauti kutaka vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vibadilishwe ili kumaliza tatizo hilo. Vifungu hivyo vinaruhusu mtoto wa miaka 15 kuolewa.

Ofisa Miradi wa Msichana Initiative katika kituo cha Nzenga, Rosemary Batoba anasema wilayani humo wasichana wengi walikuwa wakipitia changamoto mbalimbali, zikiwemo ndoa za utotoni.

“Tulianza kutoa elimu na kuwajengea uwezo mabinti kujitambua na kupinga vitendo vya ukatili ili watimize ndoto zao, tulianzisha mradi wa “Arudi Shule” na kuwafikia wasichana 200.

“Wazazi wengi waliamini wasipompa binti sapoti ataacha shule ili aolewe, tulitoa sapoti ya baiskeli kwa mabinti wanaotoka umbali mrefu kuanzia kilomita 10 kwenye shule za Mizibaziba, Mirambo, Itobo, Tuge, Mwanyala, Isagenhe na Budushi,” anasema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Isegenhe, Jumanne Shabani anasema Jane ni miongoni mwa wasichana wenye uwezo mkubwa shuleni hapo.

“Alipokuja kuanza kidato cha kwanza alinieleza changamoto zake, kwa kuwa lengo lilikuwa apate elimu, mapungufu mengine hatukuyazingatia kwake,” anasema.

Hata hivyo, Jane ambaye ana ndoto ya kuwa mwalimu wa sekondari anasema, jitihada zake shuleni zimesababisha mama yake kumuacha afanye atakavyo.

“Japo kwa shingo upande, ameniacha nisome, ukizingatia mimi peke yangu kati ya watoto wake ndiye nimefika sekondari.

Mama yake Jane aliyejitambulisha kwa jina moja la Nyarusi anasema binti yake amempa somo kwamba mtoto wa kike anapaswa kupata elimu.

“Kweli nilitaka kumuoza, niliamini heshima ya mtoto wa kike ni ndoa lakini yeye (Jane) alisimamia ndoto zake, nimemuacha, japo kuna wadogo zake wameolewa, wengine bila hata kwenda shule,” anasema.

Mwalimu wa miradi wa Shule ya Isagenhe, Simon Shitalima anasema baadhi ya wazazi wameanza kuelewa umuhimu wa kumwendeleza mtoto wa kike kielimu.

“Mwanzo ilikuwa ni changamoto, ujio wa Mtandao wa Kutokomeza ndoa za utotoni umesaidia kubadili mtazamo wa wazazi kwa asilimia kubwa,” anasema.

Hali hiyo inashuhudiwa na Anastazia Thomas, mzazi anayesema kesi za mabinti kupata ujauzito zimeanza kupungua na wazazi wameanza kutambua umuhimu wa kuwaendeleza mabinti kielimu.

“Kesi nyingi zilikuwa za wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili,” anasema.

MbalI na Tabora, Mtandao wa Kutokomeza ndoa za utotoni (TECMN) wenye mashirika 87, unatembelea mikoa mikoa mingine mitatu inayoongoza kwa ndoa za utotoni ya Mara, Shinyanga na Dodoma.

Msafara wa TECMN katika mikoa hiyo unashirikisha mashirika ya Msichana Initiative, Medea, Plan İnternational,  My legacy, Binti Makini Foundation na Theatre Arts Feminist Group, yakipaza sauti kupinga vitendo vya ukatili ikiwamo ndoa za utotoni.

Related Posts