Clara ataka rekodi Saudia | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Al Nassr inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini Saudia, Clara Luvanga amesema msimu huu anataka kuweka rekodi mpya ya kufunga mabao 20.

Mtanzania huyo ni msimu wake wa pili kuichezea Al Nassr ambayo pia anatumikia nyota wa Ureno, Cristian Ronaldo anayekipiga timu ya wanaume.

Msimu uliopita Luvanga akiwa na mabingwa hao wa Saudia aliifungia timu hiyo mabao 11 kwenye Ligi na kumfanya aingie kwenye 10 bora za wafungaji nchini humo.

Akizungumza na Mwanaspoti kutokea Saudia, mshambuliaji huyo alisema baada ya kucheza msimu mmoja na kufunga mabao hayo huu ni mwaka wa kuweka rekodi nchini humo.

“Sikumbuki lini nimefunga mabao 20 tangu nianze kucheza soka la kulipwa kwahiyo msimu wa kwanza umenipa motisha ya kuendelea kufunga na natamani niweke rekodi hiyo,” alisema Clara.

Tayari chama la nyota huyo wa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ limecheza mchezo wa kwanza wa ligi juzi likiondoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Al Ula, Clara akifunga bao moja.

Related Posts