Fatma Rembo achangia simu janja kwaajili ya urahisishaji wa usajili wa wanachama wapya wa Ccm Iringa

Mjumbe wa kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT) kutoka mkoa wa Iringa, Mhandisi Fatma Rembo ametoa simu janja (Smartphone) 5 na Kishikwambi (Tablet) 1 ili kusaidia zoezi la usajili wa wanachama wapya katika Chama na Jumuiya mkoani Iringa.

Fatma Rembo amekabidhi simu hizo May 02, katika baraza la wanawake UWT Iringa Vijijini lililofanyika katika ukumbi wa Siasa na Kilimo ambapo amesema simu hizo zitagawiwa kwa kila wilaya ili kuongeza utendaji na ufanisi katika zoezi la Usajili wa wanawachama Wapya hasa wanawake ndani ya CCM na ndani ya Jumuiya ya UWT huku akisisitiza kuwa kukijenga chama na jumuiya zake, kujitolea ni lazima.

“kukijenga chama na Jumuiya zake lazima tujitolee, lazima tujitolee pale tunaweza, na hii ni kwa mtu yeyote na mimi nafanya kwa mapenzi yangu” – Amesema Mhandisi Fatma Rembo.

Vilevile, Mhandisi Fatma Rembo akiwa katika baraza hilo, amejitolea kununua Kadi 1000 kwa ajili ya kuongeza wanachama zaidi wa UWT katika mkoa wa Iringa huku akitoa wito kwa wanawake kujitokeza kujiunga na UWT ili waweze kukutana na kunufaika na fursa mbalimbali ndani ya CCM.

Sambamba na hilo, Mhandisi Fatma Rembo amechangia kiasi cha shilingi millioni 1 ili kusaidia kuendeleza ujenzi wa nyumba ya katibu wa UWT Iringa.

Pia Fatma Rembo ametumia wasaa huo kuwataka wanawake kuwa na umoja, mshikamano na moyo wa kusaidianana na kuacha kurudishana nyuma, kusemana na kukatishana tamaa huku akisema kuwa mwanamke anahitaji msaada wa wanawake wenzake ili kufanikisha mambo mbalimbali na muhimu katika jamii hasa katika masuala ya uchaguzi, uongozi na utekelezaji wa majukumu mengine ya kimalezi na kisiasa.

“kwangu mimi kila siku nasema, kila hatua Dua, namtanguliza mbele mwenyezi Mungu sina baya na mtu yeyote moyo wangu mweupe, na mimi nataka ninyi mama zangu mioyo yenu yote iwe myeupe, tushikamane, tupendane. Tukifanya hivyo hata kwenye uchaguzi wa serikali unaokuja tutakuwa kipaumbele kuwaunga mkono wanawake wenzetu”

 

Related Posts