Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Tanzania, George Simbachawene ameagiza viongozi wa umma, kuhakikisha wanasoma kitabu cha hayati Edward Moringe Sokoine ‘Maisha na Uongozi Wake’ ili kujifunza utendaji uliotukuka.
Sokoine, mmoja wa wanasiasa walioacha alama hasa katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi katika uongozi wake, alifariki dunia Aprili 12, 1984 kwa ajali ya gari eneo la Dakawa wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro akitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Edward Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Tanzania. Alikuwa Waziri Mkuu mara mbili, tangu Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na mara ya pili kuanzia Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipofariki dunia kwa ajali ya gari.
Simbachawene amesema hayo leo Jumatatu Septemba 30, 2024 wakati akitoa salamu katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake) hafla iliyohudhuliwa na viongozi mbalimbali, akiwemo na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mgeni rasmi.
Amesema maono na fikra zake za Sokoine zinatosha kujifunza juu ya siasa za ndani na Afrika kupitia mafundisho yanayopatikana katika kitabu hicho.
“Nawasisitiza viongozi wa utumishi wa umma, wasome kitabu hiki na kuhimiza uzalendo muda wote wanapokuwa ndani na nje ya utumishi wao. Kwa hakika mtumishi muadilifu ni rahisi sana kuonekana na kutambulika kama ambavyo hivi sasa tunatambua, uadilifu wa kiongozi huyu ijapokuwa hayupo nasi tena kwa takribani miaka 40,” amesema.
Amesema Sokoine alisimamia vita dhidi ya uhujumu uchumi, usimamizi wa rasilimaji na uchumi wa kijamaa.
Simbachawene amesema kitabu hicho kinatupa fursa ya kufahamu zaidi si tu maisha ya kiongozi huyo mashuhuri pia fikra zake, maisha yake, kazi yake na changamoto alizokutana nazo na jinsi alivyojenga misingi imara ambayo nchi inanufaika nayo hadi sasa.
“Utumishi wa umma, hayati Sokoine alikuwa mfano na kiongozi aliyejali uwajibikaji, haki na uwazi. Aliamini katika dhana ya utumishi wa umma akitambua kwamba uongozi ni jukumu la kutumikia wananchi, kwa moyo wa kujitolea, akijenga nidhamu ya utendaji kazi ndani ya serikali, akisisitiza utumishi bora uadilifu na ufanisi katika kila hatua ya maendeleo.
“Leo tunapoangalia historia na mchango wake tunapata somo kubwa namna ya kiongozi wa kweli anavyoweza kuacha alama isiyofutika, juu ya kitabu hiki kizazi cha sasa na baadaye kitajifunza juu na maono na fikra za kiongozi huyu ambaye alikuwa mfano wa kuigwa katika siasa za Tanzania,” amesema.
Pamoja na hayo Simbachawene amewashukuru wote walioshiriki kuandaa kitabu hicho, wakiwemo Uongozi Institute na Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA), wahariri, wachapishaji, viongozi waliohojiwa na wengine.
“Niwashukuru familia ya Sokoine, maisha ya ndani kufikishwa kwa kiongozi huyu na wadau wa maendeleo kusoma kitabu hiki kuboresha utendajii wa kazi ili kuleta maendeleo na kufanikisha uchumi wa nchi. Huu ni urithi wa thamani utakaodumu vizazi na vizazi,” amesema Simbachawene.
Alivyopigania kuanzishwa SUA
Imeelezwa hayati Sokoine ndiye aliyeshawishi wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro na kikaanzishwa, ingawa baadhi ya wabunge hawakutaka.
Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda asema, “”Aprili 11, 1984, Bunge la Jmahuri ya Muungano lilipokea muswada wa kujadili kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro kwa kupandisha hadhi kikichokuwa kitivo cha kilimo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mjadala katika Bunge ulikiwa mkali, kwani baadhi ya wabunge hawakutaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kigawanywe.”
“Ni kutokana na nguvu ya ushawishi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Edward Moringe Sokoine na imani yake, aliamini ili kilimo kiimarike, tulihitaji chuo kikuu mahsusi cha kilimo. Ndipo muswada ulipitishwa na kuwa sheria,” amesema Profesa Chibunda.
Amesema siku moja baadaye, yaani Aprili 12, 1984 Sokoine alifariki kwa ajali ya gari.
“Kwa kutambua mchango wake, uongozi wa chuo hicho uliomba jina la Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro libadilishwe na kuwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, ili kutambua juhudi zake na imani yake katika kilimo kwa maendeleo ya nchi yetu,” amesema.
Amesema muswada ulipelekwa bungeni na kupitishwa na Julius Nyerere na lilianza kutumika Julai mosi,1984.
Ili kuendelea kumuenzi Sokoine, amesema chuo hicho kimekuwa kikiandaa mhadhara wa kumbukumbu ya Sokoine.
“Mhadhara wa kwanza ulifanyika mwaka 1992 na ulizinduliwa na hayati Waziri Mkuu mstaafu, Rashid Mfaume Kawawa.
“Aprili 8, 2024 SUA iliandaa kumbukumbu ya miaka 40 ya Sokoine na miaka 40 ya kuanzishwa kwa Chuo kikuu cha Sokoine.
Katika kumuenzi Sokoine, SUA itaendelea kutoa elimu na changamoto za wananchi hasa wanaoishi vijijini,” amesema.
Awali, akizungumzia kitabu hicho, Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Kadari Singo amesema kitabu cha Sokoine ni miongoni mwa vitabu vitatu walivyoandika vikiwamo vya Benjamin William Mkapa na Ally Hassan Mwinyi marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kupitia programu ya utafiti wa viongozi, taasisi hiyo inakusudia kuandika vitabu vya viongozi wastaafu, akiwamo Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu mstaafu, Rashid Mfaume Kawawa.
“Ni matumaini yetu, hata wewe mheshimiwa Rais utakapomaliza muda wako utaruhusu mchakato wa kukusanya taarifa na kuandika kitabu chako uanze, ili kizazi cha sasa na cha baadaye kijifunze kupitia uongozi wako,” amesema Singo.
Amewataka viongozi wengine kuandika vitabu vya maisha yao ili kutoa mafunzo kwa wananchi.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa na habari zaidi