KOCHA wa Azam FC, Rachid Taoussi ameeleza masikitiko yake kufuatia matokeo ya timu hiyo katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma ambako walivutwa shati na wenyeji wao.
Taouussi amesema walikuwa na matarajio ya kushinda mchezo, lakini mambo hayakuwa vile ambavyo walitarajia.
“Kiukweli tumeumizwa na matokeo. Tulikuja hapa kwa lengo la kushinda na kutimiza malengo yetu. Tumekatishwa tamaa na baadhi ya maamuzi, lakini tunajua kuwa waamuzi ni sehemu ya mchezo,” amesema Taoussi.
Kocha huyo ameeleza kuwa bado wanahitaji kufanya marejeo ya mchezo huo ili kufanya uchambuzi wa kina.
“Tulifunga bao, lakini hatujui kama lilikuwa la kuotea au la. Tumeona kuwa halikuwa la kuotea, na hilo lingeweza kubadilisha mchezo kwa ajili yetu na kutupa kujiamini zaidi,” amesema.
Taoussi pia amezungumzia fursa nzuri waliyoipata mwishoni mwa mchezo kupitia mchezaji wao Nassor Saadun, lakini mpira uligonga mwamba.
“Tumeumizwa kwa sababu tulikuwa tunatafuta pointi tatu kila mchezo, lakini sasa tunapaswa kukabiliana na hali hii na kujifunza kuendana nayo,” ameongeza mchezaji.
Kocha huyo aliwasifu wachezaji wake kwa jitihada walizoonyesha kwenye mchezo huo, akisema kuwa walipambana na kuonyesha ari ya timu.
“Nawashukuru sana wachezaji, kwa kweli wamejitahidi sana, walipigana na kuonyesha roho ya ushindani, lakini wakati mwingine hali ya mchezo inawafanya wachezaji washindwe kujikita kikamilifu.”
Taoussi amesema timu inapaswa kusahau mchezo huo, kuchukua mazuri na mabaya na kujiandaa kwa mechi ijayo dhidi ya Namungo.