Wakati Tanzania Prisons ikitarajia kushuka uwanjani kesho dhidi ya Fountain Gate, benchi la ufundi limetumia zaidi ya dakika 35 za mazoezi ya mwisho kuwafua mastraika wake kwa ajili ya kufunga mabao.
Prisons iliyocheza mechi tano hadi sasa haijashinda wala kufunga bao ikipoteza mchezo mmoja dhidi ya Namungo na kesho Jumanne itakuwa katika Uwanja wa Sokoine kuikaribisha Fountain Gate.
Katika mazoezi iliyofanya leo, Septemba 30, katika uwanja huo mjini Mbeta chini ya Kocha Mkuu Mbwana Makata ilianza mazoezi kwa kutafuta fiziki, kumiliki mpira na pasi za hapa na pale.
Baadaye ilihitimisha kwa wachezaji kupiga penalti kufunga mabao na mipira ya mwisho, ambapo wachezaji wote walionyesha viwango bora na kuweka matumaini ya kusaka ushindi wa kwanza kesho.
Timu hizo zinakutana ikiwa Fountain Gate wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi 13 baada ya michezo sita huku Wajelajela wakiwa nafasi ya 12 kwa pointi nne baada ya kucheza mechi tano.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, beki wa timu hiyo, Wema Sadock amesema watawakabili wapinzani kwa umakini na kuwaheshimu kuhakikisha mechi hiyo wanapata pointi tatu ili kujiweka pazuri.
“Hizi ni nyakati zimetupitia wala si kwamba uwezo mdogo ila tunaenda kupambana kesho kutafuta ushindi wa kwanza ili kurejesha nguvu na furaha kwetu na mashabiki wetu,” amesema nyota huyo.
Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya amesema wanafahamu mechi itakuwa ngumu kutokana na uhitaji wa matokeo kwa wapinzani na kwamba lengo ni kuendeleza ushindi.
Amesema kabla ya kuanza msimu walikuwa na ugumu kwenye eneo la ushambuliaji ambapo matokeo ya sasa ni majibu ya kazi iliyofanywa na benchi la ufundi akidai kuwa siri ya mafanikio ni ushirikiano wa ndani na nje ya uwanja.
“Wachezaji wanajituma sana tunajua matokeo yapo ya aina ya tatu, lakini tunahitaji kuendelea kupata ushindi na tutawaheshimu wapinzani kwakuwa tunaja kiu yao na sisi wenyewe hitaji letu,” amesema Muya.