Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameiambia Iran ambayo ndio mfadhili mkuu wa makundi yanayopambana na Israel ya Hamas na Hezbollah kwamba hakuna eneo lolote huko Mashariki ya Kati wasiloweza kulifikia huku akiwaonya watu wa Iran kwamba utawala wao unalitumbukiza eneo hilo kwenye giza na vita.
Iran ambayo imesema haitokaa kimya bila kujibu vitendo vya Israel imesisitiza pia kuwa haina nia ya kuendeleza vita, lakini wako tayari ikiwa itabidi. Nasser Kanaani ni Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran:
” Sisi hatutafuti vita. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na watu wake hawataki vita. Badala yake, wanajaribu kuimarisha amani na utulivu katika eneo hili. Lakini, hatuwezi kupuuza hatua yoyote dhidi ya usalama wa taifa au maslahi yetu. Mikono yetu haijawahi kufungwa au haitawahi kufungwa katika kuchukua hatua.”
Hezbollah kumtangaza kiongozi mpya
Kundi la Hezbollah limesema litamtangaza kiongozi wake mpya hivi karibuni na kwamba wako tayari kwa makabiliano ya ardhini na vikosi vya Israel
Hotuba ya siku ya Jumatatu (30.09.2024) ya Naibu Mkuu wa Hezbollah Naim Qassem imeweka wazi kwamba kundi hilo halijatetereshwa na mauaji ya makamanda wake akiwemo kiongozi mkuu Hassan Nasrallah na kwamba wataendeleza mwongozo ulioachwa na kiongozi huyo. Sheikh Qassem amesema wako tayari kwa lolote hata ikiwa ni makabiliano ya ardhini na vikosi vya Israel.
Soma pia: Naibu Mkuu wa Hezbollah: Tuko tayari kwa lolote
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema ulimwengu uko salama zaidi baada ya Israel kumuua mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah, huku akimtaja kiongozi huyo kama “gaidi katili.”
Hata hivyo Blinken amesisitiza kuwa diplomasia ndio njia bora na pekee ya kufikia utulivu huko Mashariki ya Kati na akaapa kuwa Marekani itaendelea na juhudi za kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la wapiganaji wa Kipalestina wa Hamas huko Gaza.
Miito ya usitishwaji mapigano huko Lebanon
Lebanon na Uingereza zimekitoa wito wa usitishwaji mapigano. Wito wa Lebanon umetolewa na Waziri Mkuu Najib Mikati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot mjini Beirut . Urusi hata hivyo imelaani mauaji ya Nasrallah na kusema yanaweza kusababisha hali mbaya na kudhoofisha utulivu katika eneo hilo,
Hata hivyo Balozi wa Israel katika Umoja wa Ulaya na NATO Haim Regev ameiambia DW kwamba miito ya kusitishwa mapigano huko Lebanon “haina maana” isipokuwa ikiambatana na suluhu la kidiplomasia au kisiasa.
Soma pia: Ulimwengu wataka Mashariki ya Kati isitumbukie vitani
Wakati Israel ikiendeleza mashambulizi yake nchini Lebanon, wizara ya Afya ya serikali mjini Beirut imesema kuanzia Jumapili asubuhi, watu 125 wameuawa. Hezbollah imesema pia kuwa imeshambulia kwa makombora mji wa kaskazini wa Israel wa Safed.
Ujerumani imetangaza kuwa imeanza mchakato wa kuwahamisha raia na wafanyikazi wa ubalozi wake nchini Lebanon kufuatia hali tete inayoendelea eneo hilo.
(Vyanzo: Mashirika)