Wafunga maduka wakigoma kuuza dhahabu Benki Kuu

Geita. Wafanyabiashara wa madini katika Soko Kuu la Dhahabu Geita wamefunga maduka wakipinga uamuzi wa kutenga angalau asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa na kuiuzia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika soko hilo, kuna zaidi ya wafanyabiashara 50 wanaonunua dhahabu, ambao wamesema hawakuhusishwa kwenye uamuzi huo wakisema kwa aina ya biashara wanayofanya inawawia vigumu kutekeleza sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge la Bajeti Juni mwaka huu.

Mgomo huu wa wafanyabiashara umeanza baada ya Tume ya Madini kutoa tangazo la kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo kuanzia leo, ikiwataka wafanyabiashara kutenga asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa na kupeleka viwandani kwa ajili ya kusafishwa, ikiwemo Eyes of Africa Limited (Dodoma) na Mwanza Precious Metals Refinery Limited (Mwanza).

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko kuu la madini Geita, Dotto Ludeha, amependekeza kuwa BoT inapaswa kufungua duka lake la kununua dhahabu badala ya kuwalazimisha wanunuzi kuiuzia. Amesema: “Sisi ni wanunuzi na wauzaji wa dhahabu, lakini fedha si zetu, sisi tunawasiliana na matajiri walioko nje wanaotupa pesa tunanunua mzigo. Sasa mkisema kwenye dhahabu inayozalishwa tutenge asilimia 20 haiwezekani, mwenye pesa anataka mzigo wake.”

Firoz Khan, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilosa Kwetu Gold Limited, akizungumzia agizo la Serikali, amesema dhamira hiyo ni nzuri lakini inahitaji kuwa rafiki kwa mwekezaji. Ameeleza kuwa kampuni yake hupokea Dola za Marekani 5milioni  (Sh13.6 bilioni) kila wiki kutoka kwa wawekezaji wa nje, na fedha hizo hutumika kununua dhahabu kwa makubaliano maalumu na wawekezaji hao.

Khan aliongeza: “Leo ukisema asilimia 20 ya dhahabu niliyokusanya iende BoT, huyu aliyetoa fedha napata wapi fedha ya kurudisha wakati bei ya hapa na ya nje ni tofauti?”

Kutokana na malalamiko hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahaya Samamba, alisema Wizara itakutana na wafanyabiashara hao ndani ya wiki hii ili kutafuta suluhu ya pamoja. Samamba aliongeza: “Tutakutana nao ili kuona changamoto wanayoihisi ni ipi. Pengine wengine hawakuwepo wakati wa mchakato wa kutungwa kwa sheria hiyo au hawakufikiwa, tutawaeleza lengo na madhumuni pamoja na manufaa kwa nchi.”

Sheria iliyopitishwa na Bunge inawataka wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini na wafanyabiashara kutenga kiasi cha madini kwa ajili ya kuchakatwa, kusafishwa, na kuuzwa nchini.

Kiwango cha asilimia 20 kinachoanza kutekelezwa leo kinatakiwa kutengwa na wafanyabiashara wa madini.

Hata hivyo, hatua hii haikuhusisha kampuni za uchimbaji wa madini zilizoingia mikataba na Serikali, ili kuheshimu makubaliano hayo.

Waziri wa Fedha alieleza kuwa hatua hii inalenga pia kukuza viwanda vya kusafisha madini, kupata ithibati za kimataifa, na kuongeza akiba ya fedha za kigeni nchini.

Serikali pia imeweka vivutio kwa wafanyabiashara, ikiwa ni pamoja na kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia 0 kwa dhahabu inayouzwa kwa BoT, na kupunguza mrabaha kutoka asilimia 6 hadi 4 kwa dhahabu itakayonunuliwa na benki hiyo.

Hadi Aprili 2024, Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa imenunua dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani 26 milioni (Sh70.9 bilioni) na malengo ya Serikali ni kununua tani sita za dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani 400 milioni (SH1.1 trilioni).

Related Posts