Dar es Salaam. “Alikuwa Mmasai kwelikweii asiye na mawaa, Mkatoliki kindakindaki na wakati mwingine mwenye hamasa kubwa, pia alikuwa mzalendo wa Tanzania asiyetiliwa mashaka na mwenye upendo na nchi yake na viongozi.”
“Ikiwa ni pamoja na utii usio wa kawaida na woga kwa kiongozi wake aliyemchukulia ni mzazi wake, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyemchukulia kama baba yake mdogo hayati Rashid Kawawa,” ndivyo anavyoanza kusema mchambuzi wa kitabu cha hayati Edward Moringe Sokoine, Profesa Palamagamba Kabudi.
Profesa Kabudi ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria leo Jumatatu, Septemba 30, 2024 ametumia saa moja kuchambua kitabu hicho (Maisha na Uongozi Wake) katika hafla ya uzinduzi huo iliyohudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kitabu hicho chenye taarifa lukuki za kiuongozi chenye kurasa 499, dibaji yake imeandikwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikisindikizwa na watoa taarifa 57 waliohojiwa na kueleza wanachokijua kuhusu maisha ya kiongozi huyo.
Akichambua kitabu hicho, Profesa Kabudi amesema kimemwelezea kuwa alikuwa mrefu mwenye tambo na macho makali.
“Getrude Mongela anasimulia katika kitabu hiki kuwa Sokoine alikuwa mtu wa aina gani, ‘kwanza niligundua alikuwa mrefu sana, tofauti na nilivyokuwa nafikiria futi 6 na inchi 4 na alikuwa bado mdogo tu kwa umri miaka 45 au 40 hivi’ ndivyo alivyosema Mongela.”
Amesema watoa taarifa wanamwelezea alikuwa mpole, mtulivu, msikivu na asiye na maneno mengi na mtu wa kusoma sana. Mtoto wake, Balozi Joseph Sokoine anamwelezea baba yake kuwa alikuwa mwenye kuhifadhi mambo yake moyoni, kila aliporudi nyumbani kazi yake ilikuwa kusoma vitabu.
Hata hivyo, watu wa karibu aliofanya nao kazi walimwelezea kama msiri wa maisha yake binafsi na hata siku moja hawakujua kama ana wake wawili, pia hawakuwahi kumuona akiwa na mke wake hata siku moja.
Amesema Sokoine alikuwa akichukia haropoki, bali mara nyingi akishikwa na hasira anaenda nje kuangalia mifugo au bustani na akiwa katika hali hiyo huwa mkimya zaidi.
Ameeleza kuwa kuna wakati alikuwa anakasirika sana, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu aliwahi kumtupia faili usoni ofisa mmoja wa umma alipomdanganya kuhusu kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi, na kuna nyakati aliwachapa watoto wake wakikosa.
“Hata aliwachapa watoto wake, lakini hasira yake ilikuwa tofauti kidogo kama alivyoeleza Balozi Sokoine, ambapo alisema aliwahi kumchapa mara moja ua mbili, lakini kama baba wa Kimasai watoto walikuwa utajiri wake, akifurahi alicheza nao mpira,” amesimulia.
Profesa Kabudi amesema miongoni mwa mambo yaliyomo katika kitabu hicho ni pamoja na utata mwaka halisi aliozaliwa kiongozi huyo.
“Alizaliwa kipindi ambacho wazazi hawakutunza kumbukumbu ya tarehe wala vyeti vya kuzaliwa. Rekodi zinaonyesha Agosti Mosi, 1938, hata hivyo rekodi zake za ubatizo katika Kanisa la Mtakafitu Thereza lililopo Arusha zinaonyesha alizaliwa mwaka 1939, lakini inayotambulika ni Agosti Mosi, 1938,” amesema.
Akielezea historia ya baadaye amesema kwa mujibu wa mila za Kimasai mwaka 1975 alitawazwa kuwa Mzee mdogo katika sherehe ambayo hufanyika kwenye kilima cha wazee Sanya Juu ambayo imekuwa ikifanyika kwa zaidi ya miaka 200 sasa.
Amesema Sokoine alitawazwa siku moja na Jenerali Sam Sarakikya, Mkuu wa kwanza wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na mwanzilishi wa jeshi hilo.
Ameeleza Sokoine alikuwa na wake wawili, Mama Napolo Sokoine na Mama Sekiteto Sokoine. Wote wapo hai na wameshiriki uzinduzi wa kitabu hicho.
Pia aliweka utaratibu kwamba watoto wake lazima wawapo nyumbani wazungumze lugha ya Kimasai, utajiri kwake ilikuwa ni ng’ombe wengi, wake wengi na watoto wengi ambapo alibahatika kuwa na watoto 11, ambao pia hawakuwa wengi kwa tafsiri ya Kimasai.
Kitabu hicho kinaeleza Edward Sokoine ndiyo mtoto pekee kati ya watoto watano aliyepelekwa shule na familia yake. Alisoma Monduli mwaka 1949 mpaka 1952. Na mwaka 1953 alijiunga na darasa la tano katika Shule ya ‘Monduli Middle School’ ilikuwa shule pekee eneo la Monduli.
“Alitoroka shule na hivyo ilibidi afuatwe na askari ili arudi kufanya mitihani Isaka Monduli Juu. Aliporudishwa alifanya vizuri mno na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Umbwe Sekondari iliyoko Kibosho wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, alisajiliwa kwa jina la Edward Sokoine.
“Alikatisha masomo yake akiwa kidato cha pili kwa sababu ya ugonjwa wa kidole tumbo na alipopona na kurudi ilishindikana kuendelea kwani muda ulishapita mno, hivyo hakuendelea na masomo yake,” amesimulia.
Profesa Kabudi amesimulia kwa mujibu wa Balozi Sokoine anasema baba yake alitamani sana mmoja wa binti zake awe mtawa na aishi maisha ya kitawa.
“Amesema hiyo ndiyo sababu alimpeleka mtoto wale mmoja kusoma Shule ya Wakatoliki ya Masista wa Chipole kule Songea, ili kuanza kumzoesha kuwa Mtawa, lakini alifuata nyayo za baba yake katika siasa ambaye ni Nameloki Sokoine,” amesimulia huku washiriki wakifurahia akiwemo Nameloki mwenyewe.
Sokoine aliajiriwa mwaka 1961 na Masai Federal Authority na kuwa karani wa baraza la madiwani, baadaye alienda kusomea kozi ya serikali za mitaa mwaka 1964 katika Chuo cha Mzumbe akapandishwa cheo na kuwa Ofisa Mtendaji daraja la 4 nafasi ambayo kwa sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri.
“Baadaye alikwenda Ujerumani Magharibi kusoma masuala ya utawala na fedha na aliporudi alipandishwa cheo, kipindi hicho pamoja na vitu vingine aliweka nguvu nyingi kuinua kiwango cha elimu cha jamii ya Kimasai, ambapo mmoja wa watu aliowasaidia na kuwalazimisha kwenda shule ni mheshimiwa Ole Kone mwenyeji wa wilaya ya Simanjiro,” amesema.
Profesa Kabudi amesema mwaka 1965 aliamua kuingia katika ulingo za siasa na kugombea ubunge wa eneo la jamii ya Kimasai.
Amesema umahiri wa Sokoine alioutumia katika kampeni za uchaguzi ndiyo sababu za ushindi wake na alikula kiapo Oktoba 12, 1965.
“Akiwa Bungeni aliulizwa maswali mengi na kuchangia katika mada mbalimbali, wakati huo waliitwa Wajumbe wa Bunge na aliwezesha kujengwa ofisi nyingi ikiwemo eneo analotoka. Walimuona kiongozi mwadilifu na asiye mlanguzi wa siasa na mkombozi wa jamii yao,” amesema.
Profesa Kabudi amemwelezea Sokoine kama Waziri Mkuu aliyeiongoza nchi katika kipindi kigumu akipitia mambo 12 ya mafanikio ya uongozi wa Sokoine. Ikiwemo imani kubwa katika umuhimu wa maendeleo ya kijiji hasa kilimo, kuinua maisha ya wananchi.
“Alikuwa kiongozi mkweli asiye mnafiki, alichukia uvivu na alipiga vita ubadhirifu akiishi maisha ya kawaida lakini alichukia ufukara wa kujitakia, imani ya Katoliki na mafundisho yake aliishi katika mifano aliyoiamini.
“Alitoa asilimia 50 kila mwezi kutunisha mfuko uliowekwa kulinda na kusaidia masikini. Alimshauri Mwalimu Nyerere walio na fedha na waliowekeza nje ya nchi kurudi nchini na kuanzisha maduka, usafiri wa daladala jijini Dar es Salaam,” amesema.
Profesa Kabudi amesema miongoni mwa mambo ambayo Sokoine aliyaanzisha ni mapumziko ya wafanyakazi siku ya Jumamosi, ili kujipatia muda wa kuzalisha mazao na kujitengenezea kipato nje ya mishahara yao.
Pia alianzisha vita ya uhujumu uchumi iliyotikisa kwelikweli nchi na ikawa ndiyo kazi yake kubwa katika maisha ya kisiasa akiwa waziri mkuu, lakini pia alikuwa kiongozi wa vita kwenye vita vya Uganda.
Amesema aliichukia rushwa, kusema au kuambiwa uongo. Maisha yake ya kisiasa yalikuwa ya harakati, maamuzi magumu, mikikimikiki, vitimbi, hujuma dhidi yake na masaibu na mwisho kifo kutokana na ajali ya gari.
“Moja ya mikikimikiki ni alipojiuzulu ghafla nafasi yake ya uwaziri mkuu mwaka 1980 na kwenda Yugoslvia kwa ajili ya masomo na matibabu, aliteuliwa Mzee Cleopa Msuya kuwa Waziri Mkuu mpaka mwaka 1983 aliporejeshwa kwenye nafasi hiyo baada ya kurejea nchini.
Hata hivyo, alivyorudi mambo yalikuwa yamebadilika, katika Chama cha Mapinduzi pia muundo wa uongozi ulikuwa umebadilika na nafasi ya Katibu Mkuu ilikuwa imeanzishwa badala ya ile ya awali na majina mawili yalikuwa yamewekwa Kawawa na Sokoine kuwa Waziri Mkuu.
Sokoine aliengua jina lake akisema kwamba anamuachia Kawawa kwa kuwa ni mzee kwake na anaiweza hiyo nafasi.
Katika kipindi chake chote cha uongozi, alisisitiza kuwa ujamaa haukuwa umasikini. Lakini pia alisisitiza ujamaa na kujitegemea akisema kwa nini Tanzania inanunua mahindi nje ilhali tunayo ardhi, hivyo alimshauri Mwalimu Nyerere kuwapa maeneo wafanyabiashara wa mahindi wazalishe nchi iokoe fedha za kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje. Alilisimamisha hilo na nchi ikawa na uhakika wa chakula.