Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuachia huru mwalimu wa mafunzo kwa vitendo, Frank Mpogoma, aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya kulawiti mtoto mwenye mlemavu mwenye umri wa miaka 13, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Septemba 30, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo. Amesema amefikia uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili na kubaini, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi bila kuacha shaka kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza.
Ametaja miongoni mwa dosari hizo kuwa ni pamoja na mwathirika kushindwa kuielezea Mahakama jinsi tukio hilo lilivyotendeka na badala yake alieleza tu mshtakiwa alimuingizia dudu nyuma.
“Upande wa mashtaka umeshindwa kumuongoza vyema mwathirika kueleza jinsi gani mshtakiwa alimfanyia kitendo hicho, aliieleza Mahakama tu kwamba aliingiziwa dudu nyuma, ikumbukwe kwamba mwathirika ni mlemavu, sasa alipaswa kueleza zaidi jinsi tukio hilo lilivyotendeka. Hii inaonyesha uwepo wa mashaka katika utendekaji wa tukio hilo,” amesema hakimu Swallo wakati akisoma hukumu hiyo.
Hakimu Swallo ameendelea kueleza kuwa dosari nyingine ni kwamba ripoti ya kitabibu kutokuwa na maelezo ya kutosha, kuthibitisha mwingiliano na kukosekana kwa ushahidi wa gwaride la utambuzi.
“Hivyo, Mahakama imeona kuna mikanganyiko mingi katika ushahidi wa upande wa mashtaka, hali hiyo inafanya kesi ya upande wa mashtaka kutothibitishwa ipasavyo. Mahakama inamwachia huru mshtakiwa” amesema hakimu Swallo.
Wakati wa usikilizwaji kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita na vielelezo kadhaa dhidi ya mshtakiwa huyo.
Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi dhidi ya mwalimu huyo ni Koplo Salome Kiula kutoka Dawati la Jinsia na Watoto katika Kituo cha Polisi Kigamboni.
Katika ushahidi wake Koplo Kiula, alidai mwalimu huyo wa mafunzo kwa vitendo alimlawiti mtoto huyo darasani baada ya kumziba mdomo.
Shahidi huyo alidai yeye ni askari mpelelezi, anahusika na dawati la jinsia kituoni hapo na kudai Februari 22, 2023 akiwa kwenye majukumu yake ya kazi walifika wanawake wawili wakiwa na mtoto huyo.
“Mmoja wa wanawake hao alijitambulisha kama mwalimu Fatuma na mwingine ni mama mzazi wa mtoto huyo. Mwalimu Fatuma alinieleza kuwa majira ya saa moja asubuhi, akiwa Shule ya Msingi Maweni, alisikia mtoto analia darasani,” alidai Kiula na kuongoza;
“Baada ya kusikia kilio, alikwenda darasani hapo na alikuta mtoto akilia na baada ya kumuhoji, alimweleza amelawitiwa na mshtakiwa ambaye alikuwa ni mwalimu wa mafunzo kwa vitendo shuleni hapo.”
Alieleza siku hiyo mtoto huyo alipelekwa shule na mama yake na kumshusha katika moja ya korido na kuingia darasani.
“Baadaye Mpogoma aliingia akiwa ameshika simu kubwa na kumuonyesha muathirika picha za ngono na kumtaka wafanye kama inavyoonesha katika picha hizo,” alidai shahidi huyo.
Shahidi aliendelea kudai mwathirika alikataa ndipo Mpogomo alimziba mdomo na kumvua nguo ya ndani, naye akajivua ya kwake na kumlawiti.
Alidai mwalimu Fatuma baada ya kutoa maelezo hayo katika dawati hilo la Jinsia na watoto, aliwapa fomu namba tatu ya Polisi (PF3), waende hospitali kuthibitisha maelezo hayo.
“Tuliongozana hadi kituo cha afya Kigamboni ambapo mwathirika alifanyiwa vipimo na kuthibitika alilawitiwa, tulipewa ripoti ya kitabibu na kurejea kituo cha polisi na mshtakiwa alikamatwa,” alidai shahidi.
Baada ya hapo, Kiuka aliandaa jalada la uchunguzi na aliteuliwa kuwa mpelelezi wa kesi hiyo, pia aliandika maelezo ya mashahidi wote muhimu na aliyeandaa vielelezo.
Shahidi alidai kuwa walifanya gwaride la utambuzi na mtoto huyo alimtambua mshakiwa aliyemfanyia kitendo hicho katika gwaride hilo.
Katika kesi ya msingi, Mpogolo alidaiwa kutenda kosa hilo Februari 22, 2023 katika Shule ya Msingi Maweni, iliyopo Kigamboni. Ilidaiwa siku hiyo mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati mtoto huyo alipokuwa darasani akisoma kitabu ambapo mshtakiwa aliingia na kumuonyesha picha za ngono kupitia simu yake ya mkononi na baadaye kumfanyia kitendo hicho.