KAIMU Kocha Mkuu wa Coastal Union, Joseph Lazaro, amesema hivi sasa wameanza kuuona mwanzo mpya wa timu yao ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya hapo awali kuwa na matokeo mabaya mfululizo.
Coastal Union ambayo tayari imeshuka dimbani mara sita katika Ligi Kuu Bara msimu huu, imefanikiwa kushinda mechi moja, ikipoteza nne na sare moja.
Mchezo wa mwisho dhidi ya Pamba Jiji uliochezwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, ilishuhudiwa Coastal Union ikiambulia ushindi wa kwanza msimu huu iliposhinda 2-0.
Kabla ya hapo, ilianza na sare ya 1-1 dhidi ya KMC, kisha ikapokea vichapo mfululizo kutoka kwa Mashujaa (1-0), Namungo (2-0), Azam (1-0) na JKT Tanzania (2-1).
Akizungumza na Mwanaspoti, Lazaro alisema: “Kitu kikubwa ambacho mwanzo kilikuwa kikitutesa ni kuruhusu mabao kila mechi hasa ya mapema, lakini mchezo dhidi ya Pamba Jiji tuliingia uwanjani tukisema kama hatuwezi kufunga basi tusifungwe.
“Ilipofika mapumziko matokeo yakiwa 0-0, nikawaambia vijana wangu kwamba hii ni mechi yetu. Kweli kipindi cha pili tukafunga mabao mawili ambayo yalitupa ushindi. Hapa sasa ninaanza kuona kuna kitu kizuri kinakuja.”
Katika hatua nyingine, Kocha Lazaro amebainisha kwamba, mbali na tatizo la kuruhusu mabao walilokuwa nalo hapo awali, pia aligundua wachezaji wake walikuwa hawapigi mashuti kuelekea langoni mwa wapinzani.
“Mbali na kuruhusu mabao, pia wachezaji wangu walikuwa hawapigi, tulipoanza kupiga tukaona kuna mabadiliko, hivyo huu ni mwanzo mzuri na kwa kuanzia hapa naamini tutaendelea kufanya vizuri.
“Wachezaji wangu mazoezini nilikuwa nikiwalekeza vitu vya kufanya lakini wanashindwa kuviwasilisha siku ya mechi, kupitia ushindi wetu dhidi ya Pamba Jiji ni wazi sasa kama tukiendelea hivi tutakuwa nafasi nzuri,” alisema Lazaro.
Coastal Union kwa sasa inajiandaa na mchezo wa ugenini dhidi ya Simba katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Ijumaa ya wiki hii kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.