Jaji Warioba alivyotofautiana na Sokoine agizo la Nyerere

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesimulia mambo  aliyoyasimamia pasina kuyumba, ikiwemo la kukataa kutekeleza agizo la mkuu wa nchi, Mwalimu Julius Nyerere.

Mambo hayo yalitokea wakati Warioba akiwa Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu akiwa Edward Sokoine.  Nyerere alikuwa Rais.

Ni simulizi aliyoitoa leo Jumatatu, Septemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake), hafla iliyohudhuliwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

 Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Tanzania. Alikuwa Waziri Mkuu mara mbili, tangu Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980  na mara ya pili kuanzia Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipofariki dunia kwa ajali ya gari.

Ajali hiyo ya gari ilitokea eneo la Wami-Dakawa, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro akiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam akitokea mjini Dodoma alikokuwa akishiriki vikao vya Bunge.

Katika maelezo yake, Jaji Warioba amesema agizo hilo lilihusu Sheria ya Uhujumu Uchumi iliyokuwa na vipengele vilivyokiuka haki za binadamu na alishauri viondolewe, lakini havikuondolewa.

Vipengele hivyo ni pamoja na kesi kusikilizwa kwa siri, watu kunyimwa dhamana, matumizi ya ushahidi wa kusikia na kuwa na mahakama maalum za ufisadi.

Jaji Warioba amesema mara baada ya Sokoine kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili mwaka 1983,  alisimamia uanzishwaji wa sheria hiyo.

“Alisema kesi za uhujumu uchumi zisikilizwe katika mahakama maalumu, halafu ushahidi wa kusikia uchukuliwe, kesi zisikilizwe faragha na kusiwe na dhamana,” amesema.

Hata hivyo, Jaji Warioba amesema alipinga sheria hiyo, akisema inakiuka utawala bora na haki za binadamu.

“Nikamwambia, mimi kwa kuwa ni Waziri wa Sheria na Mwanasheria mkuu siwezi kusimamia sheria ambayo siiamini. Kwa hiyo nikamwambia Mheshimiwa waziri Mkuu mimi nitakaa pembeni,” amesema.

Hata hivyo, amesema Sokoine hakupenda msimamo wake.

“Akaniambia wewe umekuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa unataka kuacha kazi kwa jambo dogo hili?

“Nikamwambia hapana, sheria zozote zinazotekelezwa kwa operesheni zinakuja kuleta madhara makubwa baadaye na kwa sheria hii italeta madhara na inavunja utawala bora na inaingilia haki za binadamu,” amesema Jaji Warioba.

Ameendelea kusimulia huku washiriki wa hafla hiyo wakimsikilzia kwa makini kuwa Sokoine alimchukua hadi Msasani kwa Mwalimu Nyerere kutaka ushauri.

“Mwalimu akaamua nusunusu, akasema nendeni mkaondoe hiyo ya kesi kusikilizwa faragha na hiyo ya hearsay evidence (ushahidi wa kusikia), lakini utaratibu maalum ubaki na dhamana isiruhusiwe na akasema hakuna mtu ku resign (kujiuzulu) hapa,” amesema.

Amesema sheria hiyo ilipitishwa Aprili 1983 na Nyerere aliisaini haraka haraka.

“Yaleyale niliyokuwa naogopa yakaanza kutokea, kwa sababu utekelezaji wake ulikuwa na vurugu kubwa. Watu walianza kukamatwa kwa taratibu mbaya, mali za watu zilichukuliwa na malalamiko ya wananchi yalikuwa mengi sana,” amesema.

Katika hilo amesimulia tukio la pili la aliyewahi kuwa kiongozi wa TANU kanda ya Ziwa aliyekamatwa na wenzake walipolalamika, Mwalimu Nyerere aliagiza apewe dhamana.

“Kulikuwa na wazee kutoka Mkoa wa Mwanza walikuja Dar es Salaam kumuona Mwalimu kwa sababu mmoja wao alikuwa amekamatwa na aliwahi kuwa Mwenyekiti wa TANU Kanda ya Ziwa.

“Wakamwambia Mwalimu wewe unajua umefanya naye kazi, huyo sio fisadi, hata akienda mahakamani watasema sio fisadi, tunaomba umpe dhamana.

“Mwalimu akakubali, akaandika katika minutes sheet (karatasi ya kumbukumbu) akisema, PM (Waziri Mkuu) apewe dhamana.

“Ikafika kwa PM naye akaandika minutes sheet ya pili akasema AG (Mwanasheria Mkuu), tekeleza.

“Ikafika kwangu, nikamwandikia PM kwamba, Haiwezekani, sheria inakataa,” amesema.

Baada ya kumkatalia Sokoine, Jaji Warioba amesema aliitwa na kiongozi huyo ofisini kwake.

“Alipiga simu yeye mwenyewe akaniita ofisini kwake. Nilipoingia hata kabla ya salamu akaniuliza, Joseph wewe ni mtu wa aina gani? Rais anatoa agizo unasema haiwezekani?

“Mimi kwa kuwa tulikuwa tunataniana nikamwambia wewe si uliniburuza kwenda Msasani? Ulisikia mkubwa amesema nini, kwamba dhamana isitolewe? Wakati wote alituambia msivunje sheria hata pale mtakapoona ni mbaya, mnaweza kuibadili, sasa unasema nitekeleze? Si maagizo yake?”

Hata hivyo, Sokoine alimshauri Warioba kutekeleza maagizo ya Nyerere na baadaye marekebisho ya sheria.

“Sheria imetungwa Aprili, imeanza kutekelezwa Mei, imebadilishwa Juni,” amesema.

Akiizungumzia sheria hiyo na msimamo wa Jaji Warioba, Profesa wa Sheria, Issa Shivji amesema sheria hiyo ilizua taharuki.

“Hata mimi niliipinga hiyo sheria na tulimwita Jaji (Yona) Mwakasendo akaja chuoni akakubaliana nasi. Kulikuwa na mahakama za mfano za kufundishia pale shuleni, kwa hiyo kukawa na mjadala mkali kuhusu hiyo sheria,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Jaji Warioba na viongozi wa sasa, Profesa Shivji amesema, “Kwa sasa hiyo haipo.”

Agosti 28, 2024, Rais Samia aliposhiriki mkutano wa wakuu wa taasisi za mashirika ya umma, aliwataka kumwambia ukweli kuhusu uwekezaji ili kuepusha hasara kuwa kama wanaona jambo haliwezekani na yeye amewaeleza wamweleze ukweli.

Akizungumza katika uzinduzi wa kitabu hicho, Rais Samia aliwataka viongozi wa kisiasa, watendaji wakuu na vijana wa vyama vyote vya siasa kusoma kitabu hicho ili wapate mafunzo ya uaminifu, nidhamu na uchapakazi.

Amesema kitabu hicho kina funzo kubwa kiuongozi na kwake alichojifunza kikubwa kutoka kwa Sokoine, aliyekuwa na uaminifu, nidhamu na uchapakazi.

“Mimi pamoja na vijana wa leo, sote tunatakiwa kujifunza kutoka kwake, sifa ambazo ningependa kusisitiza kwa viongozi wa sasa na baadaye ni uaminifu, nidhamu na uchapakazi.

“Sokoine alikuwa mtulivu kwa mamlaka za uteuzi na alikasimiwa majukumu mengi na makubwa, hata kufikia hatua ya kuwa Waziri Mkuu katika umri wake mdogo hii inatuambia kwamba hatupaswi kukimbizana na vyeo, bali vyeo vitakufuata ulipo,” amesema Rais Samia.

Amesema Sokoine alikuwa na uongozi ulioacha alama katika kila sekta aliyopita, alisimamia ujenzi wa reli ya Tazara pia aliridhia wanawake waanze kuandikishwa jeshini wakati ule nafasi ya mwanamke ilikuwa chini.

Amesema hatua hiyo imeleta manufaa makubwa mpaka leo kuna majenerali wanawake na vyeo vyao wanavipata kwa uwezo na si sababu ni wanawake.

“Kitabu hiki kinatupa funzo la kujitathmini tulipotoka na tulipo sasa na hatua tulizopiga. Yapo mafunzo mengi kwa viongozi wa sasa na wanaochipukia.

“Kupitia kitabu hiki tunapata kujua maisha yake tangu alipozaliwa, kushika nafasi za uongozi, alikumbatia mila na desturi, lakini hakukubali kukumbatia mila zinazorudisha nyuma jamii yake, hivyo tunamsoma Sokoine akihimiza watoto wa Kimaisai kutimiza fursa za elimu,” amesema.

Rais Samia amesema Sokoine alikuwa baba wa mfano kwani pamoja na jukumu la uongozi hakuacha jukumu la kulea, alilipa umuhimu mkubwa.

Amesema kwa kipindi chote alichohudumu kwa weledi na uadilifu mkubwa katika nafasi zote za uongozi, ilichangiwa na uchapakazi na alitekeleza wajibu wake kikamilifu kama msimamizi wa shughuli za Serikali katika kipindi kigumu.

Pia, Rais Samia amemhamasisha Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kumaliza kitabu chake, akimweleza kuwa amemuongezea nguvu, ili kuhakikisha anakimaliza na kizinduliwe.

Pamoja na hayo, amesema Serikali imeandaa kituo mahususi cha historia na kumbukumbu za viongozi makumbusho ya marais, eneo la Mtumba na kwamba fedha zimeshatengewa fedha.

“Tumetenga Sh34 bilioni kwa ajili ya mradi huo na tumeanza kutenga Sh1 bilioni kwa mwaka huu na eneo lina ukubwa wa ekari 50 pale Dodoma,” amesema Rais Samia.

Katika hafla hiyo, mtoto wa marehemu, Balozi Joseph Sokoine ameelezea panda shuka ya safari ya miaka 40 katika kutimiza ndoto yake ya kuweka maisha ya kiongozi huyo katika maandishi.

Amesema familia ilijitahidi kufanikisha hilo kwa miaka kadhaa, kabla ya Machi 2021 kupokea simu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, ikiwataka kuwasilisha taarifa walizonazo kuhusu hayati Sokoine.

Katika maelezo yake, Balozi Sokoine amesema: “Miaka 40 ya kusoma kitabu cha maisha na mmoja wa viongozi wa Tanzania imetimia kwa msaada wako Rais Samia Suluhu Hassan. Nakumbuka Machi 2021 nilipokea simu kutoka kwa msaidizi wa Makamu wa Rais akihitaji kupitia taarifa za mzee.

“Nilimweleza nina kitabu cha hotuba aliyoitoa Machi 1983 na nikamweleza kuna hotuba nyingine aliyoitoa Oktoba 1982 kwenye mkutano mkuu wa chama na kwamba hotuba nyingine za mzee zinaweza kupatikana kwenye hansard, nilimuahidi kumtumia kitabu hicho na nilifanya hivyo,” alisimulia.

Balozi Sokoine amesema baada ya muda mfupi alipokea simu nyingine kutoka Makamu wa Rais akiuliza kama kuna kitu kingine cha ziada ambacho Sokoine aliandika.

“Nikamweleza kipo pia kitabu cha mwaka 1984 na 1985 kilichoeleza juu ya maisha ya mzee kidogo na hotuba zake na hakikuwa na uchambuzi wa kina.

“Nilimweleza juhudi za familia kwa zaidi ya miaka 30 ya kutaka kuandika kitabu, baada ya maelezo yale alinieleza kuhusu umuhimu wa kuandika kitabu cha watu mashuhuri, ili tusipoteze urithi na sehemu ya historia ya nchi yetu. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliniambia nimwachie suala hilo na ataona cha kufanya atawasilisha na kwamba angeliwasilisha kwako Rais,” amesema.

Balozi Sokoine amesema baada ya mazungumzo hayo, Makamu wa Rais, Dk Mpango alifikisha jambo hilo kwa Rais Samia Suluhu Hassan na muda mfupi alilitolea maelekezo kwamba Uongozi Institute watakuwa waratibu wa kitabu hicho pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Related Posts