Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa kisiasa, watendaji wakuu na vijana wa vyama vyote vya siasa kusoma kitabu cha maisha ya Hayati Edward Moringe Sokoine ili wapate mafunzo ya uaminifu, nidhamu na uchapakazi.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 30, 2024 wakati akizindua Kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Edward Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Tanzania. Alikuwa Waziri Mkuu mara mbili, tangu Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na mara ya pili kuanzia Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipofariki dunia kwa ajali ya gari
eneo la Wami-Dakaya, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro akiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam akitokea mjini Dodoma alikokuwa akishiriki vikao vya Bunge.
Rais Samia amesema kitabu hicho kina funzo kubwa kiuongozi na kwake alichojifunza kikubwa kutoka kwa Sokoine, aliyekuwa na uaminifu, nidhamu na uchapakazi.
“Mimi pamoja na vijana wa leo, sote tunatakiwa kujifunza kutoka kwake, sifa ambazo ningependa kusisitiza kwa viongozi wa sasa na baadaye ni uaminifu, nidhamu na uchapakazi.
“Sokoine alikuwa mtulivu kwa mamlaka za uteuzi na alikasimiwa majukumu mengi na makubwa, hata kufikia hatua ya kuwa Waziri Mkuu katika umri wake mdogo hii inatuambia kwamba hatupaswi kukimbizana na vyeo, bali vyeo vitakufuata ulipo,” amesema Rais Samia.
Amesema Sokoine alikuwa na uongozi ulioacha alama, alizoziacha katika kila sekta aliyopita, alisimamia ujenzi wa reli ya Tazara pia aliridhia wanawake waanze kuandikishwa jeshini wakati ule nafasi ya mwanamke ilikuwa chini.
Amesema hatua hiyo imeleta manufaa makubwa mpaka leo kuna maofisa jenerari wanawake na vyeo vyao wanavipata kwa uwezo na si sababu ni wanawake.
“Kitabu hiki kinatupa funzo la kujitathmini tulipotoka na tulipo sasa na hatua tulizopiga. Yapo mafunzo mengi kwa viongozi wa sasa na wanaochipukia.
“Kupitia kitabu hiki tunapata kujua maisha yake tangu alipozaliwa, kushika nafasi za uongozi, alikumbatia mila na desturi, lakini hakukubali kukumbatia mila zinazorudisha nyuma jamii yake, hivyo tunamsoma Sokoine akihimiza watoto wa kimaisai kutimiza fursa za elimu,” amesema.
Rais Samia amesema Sokoine alikuwa baba wa mfano kwani pamoja na jukumu la uongozi hakuacha jukumu la kulea, alilipa umuhimu mkubwa.
Amesema kwa kipindi chote alichohudumu kwa weledi na uadilifu mkubwa katika nafasi zote za uongozi, ilichangiwa na uchapakazi na alitekeleza wajibu wake kikamilifu kama msimamizi wa shughuli za serikali katika kipindi kigumu.
Pia, Rais Samia amemhamasisha Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kumaliza kitabu chake akimweleza kuwa amemuongezea nguvu, ili kuhakikisha anakimaliza na kizinduliwe.
Pamoja na hayo, amesema Serikali imeandaa kituo mahususi cha historia na kumbukumbu za viongozi makumbusho ya marais, eneo la Mtumba na kwamba fedha zimeshatengewa fedha.
“Tumetenga Sh34 bilioni kwa ajili ya mradi huo na tumeanza kutenga Sh1 bilioni kwa mwaka huu na eneo lina ukubwa wa ekari 50 pale Dodoma,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango amewahamasisha viongozi wengine wastaafu kuandika tawasifu zao wangali hai na kusema tayari taratibu zimeanza za kuandika kitabu cha hayati Rashid Kawawa.
“Viongozi wengine wajitahidi kuandika tawasifu wangali hai, viongozi wastaafu tunaandaa utaratibu wa kupatikana fedha na rasilimali watu, ili wafanye kazi hiyo ya kuandika tawasifu zao, nakushkuru Rais kwa kuridhia kuandikwa kwa tawasifu hii, kiongozi mwingine aliyetoa ushiriki mkubwa hayati Rashid Kawawa kitabu chake tumeanza mchakato,” amesema Dk Mpango.