Dar es Salaam. Wakati watu 26 wakithibitishwa kuugua ugonjwa wa Marburg na sita wakifariki dunia nchini Rwanda, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kimetoa msaada wa ziada na wataalamu nchini humo.
Taarifa za awali nchini humo zinaonyesha wengi walioathirika na Marburg ni wahudumu wa afya.
Watu sita wameripotiwa kufariki dunia nchini humo kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Marburg tangu ulipothibitishwa Ijumaa Septemba 27, 2024.
Waziri wa afya nchini humo, Sabin Nsanzimana ameelezea kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii X (zamani Twitter) kwamba wengi wa waathiriwa ni wahudumu wa afya, kitengo cha wagonjwa mahututi.
Marburg ambayo inaua hadi asilimia 88 ya watu wanaoambukizwa, inatoka familia sawa na virusi vya Ebola.
Ugonjwa huo huenea kwa binadamu kutoka kwa popo na kisha huambukizwa kupitia majimaji ya mwili wa binadamu.
Rwanda inasema inaongeza juhudi za kuwatafuta watu waliokaribiana na wale walioambukizwa pamoja na hatua za kupima watu ili kidhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Hata hivyo, Serikali nchini humo imewataka wananchi kuwa makini na kuripoti wagonjwa wote wanaoshukiwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo, kuna mwingiliano mkubwa baina ya Rwanda na Tanzania na hivyo kuifanya nchi kuwa hatarini.
Mganga Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Tumaini Nagu alipotafutwa na Mwananchi iliyotaka kujua namna nchi inavyodhibiti ugonjwa huo usiingie nchini, ameomba apewe muda kwa kuwa yupo safarini kikazi.
Marburg ni ugonjwa ambao umewahi kuikumba Tanzania mwaka 2023.
Machi 21, 2023 Waziri wa Afya wa wakati huo, Ummy Mwalimu alithibitisha uwepo wa ugonjwa wa Marburg katika Wilaya ya Bukoba Vijijini, Kata ya Maruku na Kanyangereko, vijiji vya Bulinda na Butayaibega, ambao uliua watu watano na watatu kupata maambukizi.
Mpaka Mei 31, 2023 jumla ya watu waliokuwa wamepata maambukizi walikuwa tisa, kati ya hao watatu walipona, akiwemo daktari wa kituo cha afya Maruku aliyewahudumia wagonjwa wa mwanzo.
Wagonjwa sita walifariki dunia, akiwemo mtaalamu wa maabara kutoka Kituo cha afya Maruku na mtoto mwenye umri wa miezi 18 ambaye mama yake ni miongoni mwa wagonjwa waliopona.
Hata hivyo, Juni 2, 2023, Tanzania kupitia Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Nagu ilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa Marburg kumalizika nchini, baada ya kukidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambapo ilipaswa kuufuatilia kwa siku 42 tangu kupona kwa mgonjwa wa mwisho.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Septemba 30, 2024 CDC inawasiliana na maofisa wa afya nchini Rwanda na kote katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Uratibu unaoendelea wa CDC ni pamoja na ushirikiano na Balozi wa Rwanda na timu ya wadhifa huo, inayofanya kazi kushughulikia changamoto kubwa za afya ya umma nchini humo. CDC pia ina uhusiano wa muda mrefu na unaoaminika na Wizara ya Afya nchini Rwanda.
CDC imetoa msaada wa ziada kwa Rwanda kwa kupeleka wataalamu wa afya kusaidia katika uchunguzi wa nchi na majibu ya mlipuko huo.
Wafanyakazi watatumia uzoefu wa kukabiliana na milipuko ya ugonjwa wa virusi vya Marburg na magonjwa kama hayo katika nchi nyingine kusaidia uchunguzi wa magonjwa, ufuatiliaji wa mawasiliano, upimaji wa maabara, kugundua na kudhibiti magonjwa kwenye mipaka na kuzuia na kudhibiti maambukizi hospitalini.
Kwa mujibu wa WHO, virusi vya Marburg ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 29 kuambukizwa na saba kati yao kufariki dunia mwaka 1967 huko Marburg, Ujerumani.
Hata hivyo, imesema virusi vya Marburg vilipatikana kwa mara ya kwanza kwa tumbili wa kijani kibichi wa Kiafrika.
Mlipuko huo ulitokana na tumbili wa Kiafrika walioagizwa kutoka Uganda, lakini virusi hivyo vimehusishwa na wanyama wengine tangu wakati huo.
Taarifa hiyo ilieleza ugonjwa huo pia unaweza kuenezwa na binadamu anayekaa kwa muda mrefu katika mapango na migodi iliyo na popo.
Ugonjwa huo umetajwa kuwa huanza ghafla kwa homa, kuumwa vibaya, kuumwa na misuli na baada ya siku tatu hufuatwa na kuharisha, kuumwa tumbo, kichefuchefu na kutapika na baadaye huanza kutokwa damu kwenye matundu mbalimbali mwilini.