Na Mohamed Saif, Ruvuma
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleleza mradi wa shilingi bilioni 14.56 wa kusambaza umeme katika vitongoji 135 Mkoani Ruvuma utakaonufaisha Kaya 4,455 mkoani humo.
Mhandisi Msimamizi wa Miradi ya Umeme REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Deogratius Nagu amebainisha hayo Septemba 30, 2024 Mkoani Ruvuma mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Kanali Ahmed Ahmed wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya CCC International Nigeria LTD.
“Katika kuhakikisha maendeleo yanafika kote nchini, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 14.56 kitumike kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 135 Mkoani hapa,” alisema Mhandisi Nagu.
Akizungumza wakati wa utambulisho wa mkandarasi huyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Ahmed aliipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia kwa vitendo na alimsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kanali Ahmed alitoa wito kwa wananchi maeneo ya miradi kuwa waadilifu kwa kulinda na kutunza miundombinu ya umeme na aliwasihi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kumrahisishia utekelezaji.
“Mkandarasi hakikisha unawashirikisha wananchi, wawe na taarifa sahihi na hii itakusaidia kupata ushirikiano kutoka kwao lakini pia ofisi yetu ipo wazi na tutakupatia ushirikiano utakaouhitaji,” alisema Kanal Ahmed.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme vitongojini, Mhandisi Nagu alisema kati ya vitongoji 3,693 vilivyopo Mkoani humo, vitongoji 1,973 vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 53 na kwamba vitongoji 135 ambavyo vitapata umeme kupitia mradi huo na kuongeza idadi ya vitongoji vyenye umeme katika Mkoa wa Ruvuma.
Aidha, alibainisha kuwa mradi huo ambao mkandarasi wake ametambulishwa hivi leo, utatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na hivyo kukamilika ifikapo Septemba 2026 na kwamba vitongoji vitakavyobaki vitaendelea kupatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mhandisi Nagu alisema mradi utatekelezwa katika majimbo Tisa katika wilaya za Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru na kwamba katika kila Jimbo Vitongoji 15 vitanufaika.
Kuhusiana na hali ya upatikanaji wa umeme vijijini kwa ujumla katika Mkoa huo, Mhandisi Nagu alisema Mkoa wa Ruvuma unajumla ya vijiji 554 ambavyo alibainisha hadi hivi sasa vyote vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 100.
“Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme vijijini nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu Wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi hiyo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa ili iweze kuwanufaisha wananchi kama ilivyopangwa,” alisema.
Alimuhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa Wakala umejipanga vyema kuhakikisha umeme unafika kwenye vijiji vyote kote nchini na kwamba baadhi ya Mikoa ikiwemo Ruvuma vijiji vyote tayari vimefikiwa na sasa unasambazwa vitongojini.