Dar es Salaam. Wakati msimu wa korosho ukitarajiwa kuanza kesho, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema hatasita kuwafutia leseni wafanyabiashara wakubwa na wadogo watakaoleta janjajanja katika ununuzi wa zao hilo kuu la kibiashara kwa mikoa ya kusini.
Bashe ambaye yupo ziarani mkoani Mtwara ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 30, 2024 na kusema kuwa anatambua wanaosemea wakulima si wakulima, hivyo hatasita kufuta leseni ya biashara kwa wafanyabiashara wakubwa, wadogo, wakati na wenye viwanda wanaofanya ujanjaujanja na kunyonya wakulima.
Ameongeza kuwa ni muhimu kila mmoja kufuata bei elekezi kwa kuwezesha sekta ya kilimo cha korosho kupiga hatua.
“Kuna mtu anahangaika kuanzia Oktoba kwa mwaka mzima, anakwenda mnadani kipato chake ni kimoja kwa mwaka, halafu kuna mtu yupo katikati anafanya ujanjaujanja wa kumnyonya huyu mkulima sitakubali,” amesema Bashe.
Bashe ameongeza Serikali imebadili mfumo wa awali kwa kuwa mkulima anapewa chini ya bei, wanunuzi ambao ni wabanguaji wamegeuka kangomba na viongozi wa Amcos wamegeuka mawakala wakupokea pesa, sasa mnada ukiisha mnunuzi atalipa chama cha ushirika na ushirika walipe moja kwa moja kwa mkulima.
Pia amesisitiza Serikali imezindua mfumo mpya wa masoko, TMX kwa mazao ya kilimo ili kuhakikisha wakulima wanapata faida stahiki kutokana na kilimo.
Waziri Bashe ameeleza mfumo wa TMX unalenga kusaidia wakulima kufikia masoko kwa urahisi na uwazi, huku wakipata bei halali inayolingana na bei za kimataifa.
“Tumeanza kutumia mfumo wa TMX kwa lengo la kusaidia wakulima kufikia masoko kwa urahisi, uwazi na kupata bei halali, inayolingana na bei ya mazao katika masoko mengine yote duniani,” amesema Waziri Bashe.
Waziri Bashe amesisitiza Serikali itaendelea kuboresha na kutumia mfumo huo, huku ikiunga mkono wadau wote wanaounga mkono mfumo huo. Amepongeza benki zote nchini kwa kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimo kupitia mikopo mbalimbali kwa wakulima.
Amebainisha kuwa Serikali imepanga kuajiri maofisa ugani 400, ili kuhakikisha kila kijiji cha uzalishaji kinakuwa na ofisa ugani. Hii itasaidia Serikali kufanya mipango, kupata takwimu sahihi na makadirio sahihi kuhusu mahitaji ya wakulima katika ngazi ya uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema mkoa huo umepata tuzo ya usimamizi bora wa tasnia ya korosho na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa usambazaji wa zaidi ya lita 21,000 za salfa na viuatilifu kwa Mkoa wa Mtwara.
Hata hivyo, Kanali Sawala ameongeza kuwa wakulima wa Mtwara wameanza kutambua kuwa inawezekana kulima mazao mengine mbali na korosho, akiyataja mazao ya mbaazi na ufuta.