Kizungumkuti dhamana ya ‘Boni Yai’ leo tena

Dar es Salaam. Sakata la dhamana ya Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob, linatarajiwa kuendelea tena leo Jumanne, Oktoba mosi, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu.

Jacob, maarufu Boni Yai, mkazi wa  Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa wa upinzani anakabiliwa na kesi ya uchapishaji taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii ambayo upelelezi wake bado haujakamilika.

Ingawa mashtaka yanayomkabili yana dhamana, lakini tangu aliposomewa mashtakata yanayomkabili, Septemba 19, 2024, dhamana yake imekuwa kizungumkuti kutokana na maombi yaliyotolewa na Serikali ya kuzuia dhamaba yake.

Siku hiyo  upande wa mashtaka uliwasilisha maombi mawili, kwanza Mahakama iamuru atoe nywila (passwords) za simu zake na ya akaunti yake ya mtandao wake wa X (zamani Twitter), ili vifanyiwe uchunguzi na mpelelezi.

Pili, uliomba Mahakama izue dhamana yake kwa madai  ni kwa usalama wake, huku wakidai  mshtakiwa alimweleza Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kinondoni, Davis Msangi kuwa baada ya taarifa hizo alizoziandika anajua atatekwa na kuuawa.

Maombi hayo yalipingwa na jopo la mawakili wa Boni Yai lililoongozwa na Peter Kibatala, wakidai hoja hizo hazina mashiko na kwamba maombi hayo hayakuwasilishwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria.

Hivyo, waliiomba Mahakama iyatupilie mbali na badala yake impe masharti ya dhamana mshtakiwa wakidai dhamana ni haki ya msingi ya kikatiba na kwamba suala la usalama si moja ya mambo yanayoweza kusababisha mshtakiwa anyimwe dhamana.

Mahakama ilipanga kutoa uamuzi wa maombi hayo ya pande zote Jumatatu ya Septemba 23, 2024, lakini siku hiyo haikutoa uamuzi huo kutokana na Boni Yai kutokufikishwa mahakamani pamoja na mahabusu wengine kwa kile kilichoelezwa kutokana na hali ya usalama.

Hivyo, Hakimu Mfawidhi, Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo alipanga kutoa uamuzi huo Septemba 26, lakini siku hiyo kabla ya Mahakama kutoa uamuzi huo, upande wa mashtaka uliibua  maombi mapya ambayo pia yaliibua mvutano baada kupingwa na mawakili wa Boni Yai.

Kwanza, waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema waliiomba Mahakama waondoe ombi la kumlazimisha mshtakiwa huyo kutoa nywila zake, wakidai waliwasilisha kimakosa kinyume cha sheria.

Licha ya jopo la mawakili wa Boni Yai linaloongozwa na Peter Kibatala, akisaidiana na John Mallya na Michael Lugina kupiga, lakini Mahakama ilikubaliana na upande wa mashtaka na kuliondoa mahakamani ombi hilo.

Kisha mawakili hao wa Serikali waliomba kuwasilisha kiapo cha ziada ambalo pia limepingwa na mawakili wa Boni Yai kuwa halijafuata matakwa ya kisheria na kwamba katika hatua iliyokuwa imefikiwa ya Mahakama kutoa uamuzi haikubaliki kuwasilishwa kiapo cha ziada ambacho ni ushahidi mwingine.

Hivyo, Mahakama ilishindwa kutoa uamuzi iliokuwa imeuandaa kuhusu maombi ya awali, badala yake iliahirisha kesi hiyo mpaka leo Jumanne, Oktoba mosi kwa ajili ya uamuzi wa ombi hilo jipya la Serikali kuhusiana na kuwasilisha kiapo cha ziada.

Kama Mahakama itakubaliana na maombi ya Serikali kuwasilisha kiapo cha ziada,  maombi ya awali ya kuzuia dhamana, ambayo uamuzi wake ulishaandaliwa yatasikilizwa upya.

Lakini kama Mahakama itakataa maombi ya Serikali la kuwasilisha kiapo cha ziada, basi itatoa uamuzi wa maombi ya awali ya kuzuia dhamana na ya mawakili wa Boni Yai ya kumpa dhamana.

Boni Yai anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kuchapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Katika shtaka la kwanza Wakili Manja alidai Septemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).

Taarifa hizo zinasomeka kuwa:

 “Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa moja katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey.”

Katika shtaka la pili, Wakili Manja alidai Boni Yai alitenda kosa hilo Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam akidaiwa kuchapisha taarifa za uongo zinazowahusisha Wakuu wa Upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.

“Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu…bali Ma-RCO waliokuwa kuteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi.”

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts