Songea ndio mji unaoubeba Mkoa wa Ruvuma ambao kabla ya uhuru ulikuwa sehemu ya jimbo la kusini sambamba na Mtwara na Lindi.
Kwa mujibu wa Chifu wa Wangoni, Imanuel Zulu, jina Songea lilitokana na neno songela linalomaanisha mlango na kwamba mtawala wa kwanza wa Wangoni Chifu Inkosi Mputa bin Gwazerapasi Gama, aliwafungulia watu mlango kuingia katika mji huo.
‘’Mzungu alishindwa kutamka songela akasema songea, lakini neno songea maana yake ni mlango, anasema.
Kuna simulizi pia inayoeleza kuwa kabla ya jina Songea, mji huo ulijulikana kwa jina la Ndonde lililotokana na watu wa kabila la Wandonde.
Wangoni walipoingia katika mji huo miaka ya 1840 waliwakuta Wandonde na kuwapiga vita na kuwashinda. Wandonde wakalazimika kuhama kwenda maeneo mengine.
Ujio wa Wajerumani eneo wakalifanya kuwa kituo cha kijeshi.
Songea pia ni maarufu kwa vita maarufu ya Maji Maji, huku ikishuhudiwa mashujaa wengi katika mji huo wakinyongwa.
Katika mnara wa mashujaa uliopo mjini Songea, majina ya mashujaa hao yametajwa kama wapiganaji dhidi ya ukoloni wa Kijerumani.
Kwa upande wake, Mkoa wa Ruvuma wenyewe umekopa jina hilo kutoka Mto Ruvuma uliopakana na Msumbiji, Ziwa Nyasa na mikoa ya Morogoro, Mtwara, Iringa na Lindi.
Ndio mto mrefu zaidi nchini ukiwa na urefu wa kilomita 152,200.