Beki Simba amtaka John Bocco

BEKI wa Simba, Abdulrazack Hamza amesema anatamani kumuona mshambuliaji wa JKT Tanzania, John Bocco katika benchi la timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ili kuwasaidia wachezaji chipukizi kujifunza kutoka kwake.

Hamza ameyazungumza hayo katika mahojiano na Mwanaspoti baada ya kuulizwa ni mshambuliaji gani anayemkubali muda wote na hapo amejibu: “Namkubali Bocco kutokana na rekodi yake ya mabao 154 ya mechi za Ligi Kuu. Ana mwendelezo wa kucheza kwa kiwango, nidhamu na kujiheshimu.”

Ameongeza kuwa, “ndio maana nasema anastahili kuwepo katika benchi la ufundi la Stars, kwani damu changa zitajifunza kitu kutoka kwake hasa wale ambao wanacheza nafasi yake.” 

Hamza amesema Bocco anatumia akili kubwa kufunga mabao  na ni kati ya washambuliaji ambao amewahi kupata shida kuwakaba kabla ya kujiunga Simba na Bocco kutimkia JKT Tanzania.

“Naheshimu nikimuona mzawa anajituma, siyo kazi nyepesi kwa nafasi yake kuwa na mwendelezo wa kufunga mabao na wala hajawahi kupotezwa na umarufu alionao,” amesema Hamza aliyesajiliwa na Simba kutoka SuperSport ya Afrika Kusini, kuziba pengo la Henock Inonga.

Bocco alitangaza kustaafu kuitumikia Stars ambayo ameweka rekodi ya kuifungia mabao 16 katika mechi 84 tangu alipoanza kuichezea 2009 na mara ya mwisho kuonekana na kikosi hicho ilikuwa Septemba 2023.

Related Posts