Mwezi Julai mwaka 2023, Mark Rutte alitangaza kujiuzulu katika wadhifa wake wa Waziri Mkuu wa Uholanzi na miezi michache baadaye akaanza kudhihirisha nia yake ya kumrithi Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, ambaye alitangaza kuachia wadhifa huo Septemba mwaka huu wa 2024.
Kwa miezi kadhaa, Rutte aliendesha kampeni yake ndani ya muungano wa NATO, huku viongozi wengi wakiwa tayari wanamfahamu alipokuwa waziri mkuu wa Uholanzi kwa zaidi ya miaka 13 na kufanya kazi na mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Soma pia: Je, NATO inapaswa kudungua droni za Urusi?
Mwanahistoria huyo ambaye ni mgombea aliyepigiwa pia upatu na Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wengi wa Ulaya, anakabiliwa na changamoto mbalimbali katika uongozi wake ikiwa ni pamoja na vita nchini Ukraine, hofu juu ya hatua za baadaye za Urusi na hali ya wasiwasi wa kisiasa nchini Marekani kutokana na kutofahamu kwa sasa ni nani atayeshinda urais.
Hotuba ya kuaga ya Stoltenberg
Wakati wa hotuba ya kuaga, kiongozi anayemaliza muda wake Jens Stoltenberg alizielezea baadhi ya changamoto zinazoikabilia NATO:
” Tangu nichukue wadhifa wangu kama katibu mkuu mwaka 2014, ulimwengu unaotuzunguuka umebadilika sana. Tumeshuhudia Urusi ikiinyakua kinyume cha sheria rasi ya Crimea, kuimarika kwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine, ushindani unaokua wa China, janga la Covid 19, mashambulizi zaidi ya mtandaoni na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye usalama wetu.”
Mbali na hayo, Mark Rutte anakabiliwa pia na changamoto ya kuyaleta pamoja maono ya viongozi wa nchi wanachama ili hatimaye kuwepo makubaliano ya pamoja linapokuja suala la maamuzi muhimu. Rutte ni mzoefu katika kuongoza miungano ya kisiasa nchini Uholanzi, lakini sasa atatakiwa kuvileta pamoja vyama 32 ili kufikia mwafaka unaohitajika kwa maamuzi yote ya NATO.
Msimamo mkali wa Hungary
Katika kampeni yake, Rutte alikuwa na kibarua kigumu cha kumkinaisha Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, ambaye hapo nyuma mahusiano yao yalikuwa na mkwaruzano.
Rutte alilazimika kumuahidi Orban kwamba Hungary haitalazimika kamwe kushiriki katika shughuli za kusaidia Ukraine nje ya eneo la NATO . Orban, ambaye anadumisha uhusiano wa kirafiki na Urusi, amekataa pia kupeleka silaha kwa Ukraine.
Siasa za kiliberali za Rutte na msimamo wa siasa kali za mrengo wa kulia za Orban mara nyingi huwaweka kwenye mzozo katika shughuli zao ndani ya Umoja wa Ulaya. Hungary ilipopitisha sheria dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja (LGBTQ+) mwaka wa 2021, Rutte alimwambia Orban kuwa yuko huru kuondoka katika jumuiya hiyo iwapo hakubaliani na sera zake.
Haiba ya Rutte na misimamo yake
Uwezo wake mashuhuri wa kukabiliana na changamoto za kisiasa na kuwa na misimamo isioyumba, unamfanya Rutte kuwa kiongozi anayefaa iwapo Donald Trump atarejea katika Ikulu ya White House na kuanza ukosoaji wake dhidi ya muungano huo wa kijeshi.
Hata hivyo, cha kushangaza Rutte na Trump walikuwa na uhusiano mzuri wakati wa muhula wa kwanza wa Trump kama rais wa Marekani, na Trump alifikia hata kumwita Rutte “rafiki.” Lakini Rutte alipinga vikali sera ya uchumi ya Trump. Tofauti na Trump, Rutte ni muungwaji mkono mkubwa wa Ukraine na aliwezesha uwasilishaji wa silaha mjini Kyiv, ikiwa ni pamoja na vifaru na ndege za kivita chapa F-16.
Wachambuzi wanasema Rutte atatakiwa kuonyesha dira ya uongozi wake ili kuiendeleza NATO, kwa sababu kufikia muafaka kunaweza kuchukua muda na inaweza kukatisha tamaa lakini ni muhimu kuonyesha mwelekeo wa kisiasa na maendeleo yanayofikiwa.
(DW, RTRE)