Serikali ya Tanzania yatetea uamuzi wa kusimamisha uvuvi Ziwa Tanganyika

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema uamuzi wa kusimamisha uvuvi kwa miezi mitatu kila mwaka kwenye Ziwa Tanganyika unalenga kuhakikisha kunakuwa na uvunaji wa rasilimali za uvuvi kwa njia endelevu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti ameyasema hayo leo Ijumaa, Mei 3, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kalambo (CCM), Joseph Kandege.

Mbunge huyo amehoji kama kuna utafiti wa kisayansi unaoonyesha kufunga shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika ili kuruhusu kuzaliana kwa samaki kutakuwa na tija ya muda mrefu.

Akijibu swali hilo, Mnyeti amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kunakuwa na uvunaji endelevu wa rasilimali za uvuvi katika Ziwa Tanganyika.

Amesema wizara kwa kushirikiana na nchi zinazounda mamlaka ya Ziwa Tanganyika inatekeleza mkataba wa kikanda wa nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, unaoweka hatua za usimamizi wa uvuvi endelevu katika Ziwa Tanganyika na bonde lake.

Aidha, Mnyeti amesema miongoni mwa hatua za usimamizi ni kuanzishwa kwa utaratibu wa kupumzisha shughuli za uvuvi katika ziwa hilo kila ifikapo Mei 15 hadi  Agosti 15, 2024.

“Upumzishaji wa Ziwa Tanganyika katika kipindi cha miezi mitatu unatarajiwa kuwa na tija ya muda mrefu kwa kuwa utafiti katika nchi zinazozunguka ziwa unaonyesha kuwa kipindi hicho kunakuwepo na samaki wengi wachanga aina ya migebuka na dagaa,” amesema.

Amesema samaki hawa wanahitaji kipindi cha miezi mitatu mpaka minne kufikia kiwango cha kuvuliwa.

Hivyo, amesema kupumzisha ziwa katika kipindi hicho kutaruhusu samaki kukua na kuongeza mavuno.

Katika maswali ya nyongeza, Kandege amesema kwa kuwa upungufu wa samaki unasababishwa na uvuvi haramu katika maziwa, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na hali hiyo.

Akijibu swali hilo, Mnyeti amesema imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa katika maziwa.

Amesema mikakati hiyo hawezi kuitaja bungeni kwa kuwa mingi ni ya kiitelejensia na kwamba jeshi nalo linafanya operesheni za kupambana na uvuvi haramu.

Mnyeti amesema wanatoa elimu kwenye ziwa hilo kupitia wataalam na hata yeye na Waziri wa Mifugo na Uvuvi wameshawahi kwenda kuhamasisha ufugaji wa samaki kwenye vizimba.

Naye Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani amesema uvuvi katika ziwa hilo ndio shamba la wananchi wanaolizunguka na hivyo akahoji Serikali imetenga shilingi ngapi kwa ajili ya kusaidia wavuvi hao ambao watasimamisha shughuli zao kwa miezi mitatu hiyo.

Akijibu swali hilo, Mnyeti amesema Serikali inawasaidia kwa kuwakopesha vizimba kwa riba nafuu, miradi itakayosaidia kuongeza uzalishaji ziwani humo.

“Tumepokea maombi ya watu wengi kutoka kwa wavuvi na Mei 5 (mwaka huu) Waziri wa Mifugo na Uvuvi anakwenda kukabidhi vizimba, bado watu wanaendelea kuomba na tutaendelea kutoa mikopo hiyo, huo ndio msaada wa Serikali,” amesema.

Related Posts