Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya Serikali kuwasilisha kiapo cha ziada katika kiapo cha awali cha kupinga dhamana ya aliyewahi kuwa Meya wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob, maarufu kama Boni Yai.
Jacob, maarufu kama Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa, anakabiliwa na kesi ya uchapishaji taarifa za uwongo kwenye mitandao, ambayo upelelezi wake bado haujakamilika.
Hata hivyo Mahakama hiyo imepiga kalenda tena uamuzi wa maombi ya awali ya upande wa mashitaka ya kuzuia dhamana ya Boni Yai, ambao awali ilikuwa imepanga kuutoa Septemba 23 ikaahirishwa mpaka Septemba 26, ambapo pia Mahakama ilishindwa kuutoa baada ya Serikali kuomba kuwasilisha kiapo cha ziada.
Sasa Mahakama hiyo imepanga kutoa uamuzi huo wa maombi ya awali ya Serikali ya zuio la dhamana Oktoba 7, 2024.
Endelea kufuatilia Mwananchi.