Wawili wafariki dunia Ziwa Victoria wakitokea kwa mganga wa kienyeji

Musoma. Watu wawili wamefariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama kwenye Ziwa Victoria katika Kijiji cha Burere wilayani Rorya Mkoa wa Mara, huku wengine wawili wakiokolewa.

Tukio hilo limetokea Septemba 29, 2024 saa 11 jioni watu hao wakiwa wanatoka katika Kijiji cha Busanga walikokuwa wamekwenda kutibiwa kwa mganga wa kienyeji wakielekea kijiji cha Busimbiti wilayani Rorya.

Akizungumzia tukio hilo jana Jumatatu Septemba 30, 2024 mjini Musoma, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema baada ya mtumbwi huo kuzama watu wawili waliokolewa hai muda mfupi baada ya tukio, huku miili ya watu wawili ikiopolewa leo Oktoba Mosi, 2024

Amewataja waliofariki katika tukio hilo kuwa ni Neema Maswi (18) mkazi wa Kijiji cha Baraki na Arena Akeng’o (41) mkazi wa Kijiji cha Busanga wilayani Rorya.

“Katika ajali hiyo ambayo chanzo chake ni mtumbwi kupigwa na dhoruba kisha kushindwa kuhimili na kuzama waliokolewa wanaume wawili ambao ni Majeshi Mariba (40) na Wandiba Kisare (45) wote wakazi wa Kijiji cha Burere wilayani Rorya,” amesema

Hata hivyo, amesema mtumbwi huo uliotumiwa na watu hao kusafiria haukuwa kwa ajili ya kusafirisha abiria, bali ni kwa shughuli za uvuvi.

 Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku 14 tangu kuzama kwa mtumbwi mwingine katika Kijiji cha Igundu wilayani Bunda na kusababisha vifo vya watu sita, huku 14 wakiokolewa.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema ipo haja ya mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuwanusuru watu wanaotumia usafiri wa majini hasa ndani ya Ziwa Victoria, kwa madai kuwa hatua zisipochukuliwa mapema kuna uwezekano wa watu wengi zaidi kuendelea kupoteza maisha.

“Majuzi tu hapa walisema mtumbwi umeua watu huko Bunda na mtumbwi huo ulikuwa ni kwa ajili ya shughuli za uvuvi leo pia mtumbwi wa uvuvi umeua watu, hii inaonyesha kuwa huko ziwani taratibu hazifuatwi,” amesema Yohana Jumanne.

Jumanne amesema mamlaka zinazohusika zikitimiza wajibu wao wamiliki wa vyombo vya usafiri ndani ya Ziwa Victoria hasa maeneo ya vijijini watafanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za usalama wa usafiri majini.

Naye Loyce Manjebe amesema, “Ukiangalia matukio yote yamesababishwa na vyanzo vya kufanana, hapa ina maana kuna sehemu pana tatizo, wahusika wawajibike kabla hali haijawa mbaya na yawezekana wengi wanakufa katika mazingira ya hivyo ila taarifa hazitolewi.”

Tukio hili limetokea ikiwa ni siku nne tu tangu kuhitimishwa kwa maadhimisho ya siku ya usalama wa usafiri majini ambapo kitaifa yalifanyika katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Katika tukio jingine mtu mmoja ambaye jina lake halijapatikana amenusurika kufariki dunia baada ya kuzama ndani ya Ziwa Victoria katika Manispaa ya Musoma.

Mtu huyo anayedaiwa kuwa ni bodaboda inadaiwa alizama baada kushindwa kumudu pikipiki aliyokuwa akiendesha hali iliyosababisha kupaishwa na kurushwa ndani ya ziwa mita chache kutoka katika barabara ya Nyerere.

“Alikuwa anaendesha kutokea Nyakato sasa alipofika hapa akiwa anataka kukata kona pikipiki ikamshinda ikanyooka moja kwa moja kuelekea ziwani kabla ya kupaa na kutumbukia ndani ya ziwa,” amesema Omari Ramadhani shuhuda wa tukio hilo.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amethibitisha tukio hilo, akisema mtu huyo ameokolewa akiwa amepoteza fahamu hivyo amewahishwa hospitalini kwa matibabu.

Related Posts