KOCHA wa Bigman, Salhina Mjengwa amesema hawajapoteza matumaini kwenye Ligi ya Championship licha ya kuambulia pointi moja katika michezo miwili akiahidi kutafuta suluhu kwenye uwanja wa mazoezi ili waanze kuvuna alama tatu.
Timu hiyo ambayo ni msimu wake wa kwanza kwenye mashindano hayo baada ya kupanda daraja, awali ikijulikana kwa jina la Mwadui FC, mwishoni mwa wiki iliyopita ilichapwa mabao 2-0 na Songea United huku ikiambulia sare ya mabao 2-2 na Mbeya City katika mchezo wa kwanza.
Bigman yenye makazi yake mjini Tanga ikiwa inatumia Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, inaundwa na mastaa mbalimbali waliowahi kutamba Ligi Kuu akiwemo Salum Kanoni, Deogratias Munishi ‘Dida’, Mohamed Ibrahim, Salum Kipaga na Seleman Kibuta.
Mjengwa amesema umakini mdogo wa kikosi hususan eneo la ulinzi katika mchezo wa ugenini dhidi ya Songea United ndiyo uliosababisha kupoteza pointi tatu, huku akiamini makosa hayo yanarekebishika na watakuwa imara mechi zijazo.
“Tulimiliki mpira na kutengeneza nafasi. Tukafanya makosa ambayo yaliwapa matokeo (wapinzani) baada ya wachezaji wangu kukakosa umakini katika eneo la ulinzi. Niwapongeze Songea United walitumia vyema makosa hayo kupata ushindi,” amesema Mjengwa
Nahodha wa timu hiyo, Seleman Kibuta amesema kikosi kina morali kubwa licha ya kuanza ligi kwa kasi ya chini, lakini wana imani wataanza kufanya vizuri kutokana na kuwa na wachezaji wengi wazoefu wanaoweza kuhimili presha pamoja na uwepo wa benchi bora la ufundi.
Kocha wa viungo wa Bigman, Uhuru Seleman amesema: “Msimu huu Bigman tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapanda Ligi Kuu na timu ambazo tunakutana nazo wajipange kwa sababu tuna malengo makubwa na tupo hapa kufanya kitu ambacho kitakuwa historia kwa timu hii.”