Wanne jela miaka 20 kila mmoja kwa kupatikana na heroini

Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Ndogo ya Mtwara, imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela washitakiwa wanne baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevye aina ya heroini gramu 7,992.82.

Hukumu hiyo imetolewa Septemba 25, 2024 na Jaji Martha Mpaze katika kesi ya uhujumu uchumi namba tisa ya mwaka 2022.

Waliohukumiwa ni Rajabu Yusuph, Salum Abdallah, Jeremia Joseph na Kelvin Michael.

Jaji Mpaze baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote aliridhika kuwa Jamhuri imethibitisha mashitaka pasipo kuacha shaka, hivyo aliwatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela.

Washtakiwa wametiwa hatiani kwa kusaidia kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha kifungu cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ikisomwa pamoja na aya ya 23 ya jedwali la kwanza na kifungu cha 70 (3) cha Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Kuratibu (EOCCA). Inadaiwa walitenda kosa hilo Juni 10, 2019.

Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliwakilishwa na mawakili saba wakiongozwa na wakili Tully Helela, huku washitakiwa wakitetewa na mawakili sita wakiongozwa na Datius Faustine.

Upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 11 na vielelezo vikiwemo pikipiki, fomu za uwasilishaji, pakiti nane za heroini, simu nane na hati za kukamata mali.

Ilidaiwa mahakamani na shahidi wa nne, sita, nane na tisa ambao ni PF 17957 ASP Albert, Inspekta Patrick Ndomba, E6940 Sajenti Lugendo na G3744 D/Koplo David Lyanga kuwa wakiwa doria karibu na Mto Ruvuma, wilayani Newala walikutana na pikipiki nne.

Inadaiwa baada ya ukaguzi, pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Rajabu akiwa amebeba begi kwenye tangi la mafuta ilibainika unga uliohisiwa kuwa dawa za kulevya.

Ilidaiwa mahakamani Rajabu alikiri kupokea dawa hizo kutoka kwa dereva wa Msumbiji aliyemtaja kwa jina la Issa aliyemtaka kuzipelekea kwa Salum (mshtakiwa wa pili).

Salum alikamatwa jirani na Shule ya Msingi Butiama na wakati wa mahojiano inadaiwa alikiri kumiliki dawa hizo na kumuhusisha Kelvin (mshtakiwa wa nne), akidai ndiye alitoa maelekezo ya kukusanywa dawa hizo.

Inadaiwa Rajabu na Salum wakiwa kizuizini katika Kituo cha Polisi Newala, waliendelea kuwasiliana na Kelvin aliyedaiwa kutoa rushwa ya Sh10 milioni ili dawa hizo na mshtakiwa wa pili waachiwe.

Katika jitihada za kumnasa Kelvin, ilidaiwa Polisi walipokea fedha hizo na kuhamishwa kupitia wakala Zainab Ungaunga kwenda kwa mashahidi wa Jamhuri (ASP Albert, Halid Kablewa, Koplo Lyanga) na Salum. Zilitumwa Sh10.2 milioni.

Inadaiwa baada ya makato ikatolewa Sh10.168 milioni na baada ya fedha hizo kutumwa, Kelvin alijulishwa kuwa mshtakiwa ameachiwa hivyo alimuagiza Salum kuchukua pikipiki hadi Masasi, ambako angekutana na mtu ambaye atampatia fedha kwa ajili ya safari kuelekea Dar es Salaam.

Baada ya kufika Masasi, Salum aliwasiliana na Kelvin ambaye alimwagiza amsubiri katika moja ya nyumba za kulala wageni, muda mfupi baadaye alienda dereva wa pikipiki akiwa na abiria na alipoingia ndani Polisi walimtaka kuondoka bila kumjulisha mteja wake na kuwezesha kukamatwa Jeremia.

Baada ya kukamatwa Jeremia, Inspekta Ndomba na Koplo Lyanga walidai alipohojiwa mshtakiwa alidai ni ndugu wa Kelvin na alitumwa kupeleka fedha kwa Salum kwa ajili ya kusafiri kwenda Dar es Salaam, ambako alitakiwa kusafirisha dawa hizo.

Baada ya kukamatwa timu ya Polisi ilimkamata Kelvin nyumbani kwake Dar es Salaam, akidaiwa kukiri kumtuma Jeremia kuchukua dawa hizo lakini si zake.

Ilidaiwa operesheni ya kuwakamata watuhumiwa ilihitimishwa Juni 13, 2019 na wote walipelekwa mkoani Mtwara. Washitakiwa wanadaiwa kukamatwa wakiwa na simu nane.

Mshtakiwa Haji alifariki dunia hivyo kesi dhidi yake ilifutwa.

Inadaiwa Juni 14, 2019, pakiti nane zilizokamatwa kutoka kwa Rajabu na Salum zilichambuliwa na kufungwa upya kwenye mifuko ya nailoni, gundi na kila moja kuwekwa namba ya IR

NE/IR/609/2019, tarehe ya kukamatwa na maelezo mengine muhimu.

Juni 15, 2019, shahidi wa pili nane na maofisa wengine walisafiri hadi Dar es Salaam katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na baada ya kupimwa ilibainika ni dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa gramu 7,992.82.

Washtakiwa walikana mashitaka, Rajabu akidai akiwa mpakani mwa Mto Ruvuma akisafirisha abiria kutoka Msumbiji kwenda Newala alizuiwa na askari waliokuwa wakihakiki nyaraka za uhamiaji ambazo abiria wake hakuwa nazo.

Alidai hilo lilisababisha yeye na abiria kukamatwa na kupelekwa ofisi ya uhamiaji na wakati anashikiliwa, askari mmoja alimtaka awasiliane na Salum, jambo lililosababisha Salum kukamatwa.

Alidai baadaye alipelekwa maeneo mbalimbali na Polisi, ikiwamo nyumba ya kulala wageni na Kituo cha Polisi Newala na akiwa Polisi alipewa hati mbalimbali za kusaini lakini hakuelewa yaliyomo.

Salum alidai alipigiwa simu na Rajabu Juni 10, 2019 na baada ya kukutana naye alikamatwa na maofisa wa Polisi ambao walishindwa kumfahamisha kuhusu kosa linalomkabili.

Alidai pia alihojiwa kuhusu dawa za kulevya jambo ambalo alikanusha kuwa hajui lolote. Pia alidai aliteswa na Polisi katika jaribio la kulazimisha kukiri kosa.

Jeremia alidai alifika Masasi Juni 8, 2019 kwa ajili ya biashara ya nafaka na alikamatwa Juni 11, akahojiwa kuhusu uhusiano wake na Kelvin, ambaye alieleza ni kaka yake.

Alidai alitakiwa kuwapeleka Dar es Salaam nyumbani kwake na hakuwa na ufahamu wowote kuhusu washtakiwa wengine. Alikana kuhusika na usafirishaji dawa za kulevya.

Kelvin alidai Juni 12, 2019 maofisa wa Polisi waliingia kwa nguvu nyumbani kwake na kufanya upekuzi na alipelekwa Kituo cha Polisi cha Tazara akituhumiwa kuhusika na wizi wa magari na biashara ya dawa za kulevya, mashitaka aliyoyakana.

Alidai ingawa aliwasiliana na Jeremia siku za nyuma ila hakuwa na ufahamu kuhusu biashara ya dawa za kulevya na pia hakuwa akiwafahamu Rajabu na Salum hadi alipokutana nao katika kesi hiyo.

Mahakama katika hukumu iliongozwa na jambo moja kuu ambalo ni iwapo upande wa mashitaka umethibitisha kesi dhidi ya washtakiwa wote bila kuacha shaka.

Jaji alisema uamuzi wa Mahakama utazingatia suala la msingi la kesi likisaidiwa na maswali madogo kadhaa ambayo ni iwapo pakiti nane za unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya kama zilithibitishwa ni dawa za kulevya.

Alisema masuala hayo yakijibiwa na kuthibitishwa suala lingine itakuwa ni endapo watuhumiwa ndiyo walisafirisha na mwisho ni endapo mlolongo wa ulinzi ulidumishwa.

Alisema upande wa mashitaka umethibitisha kesi bila kuacha shaka, hivyo washtakiwa wote wana hatia na amewatia hatiani, akawahukumu kifungo cha miaka 20 jela.

Jaji Mpaze alisema kosa la aina hiyo adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 kwa mujibu wa kifungu cha 60(2) cha Sheria ya EOCCA, ila kwa kuwa wameshakaa mahabusu tangu mwaka 2019 Mahakama inawapunguzia adhabu.

“Washtakiwa wamekuwa rumande tangu 2019, miaka mitano iliyotumika tayari ina uzito mkubwa katika kesi hii, kwa kuzingatia hayo natoa adhabu kwa kila mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela,” amesema.

Ameagiza kuharibiwa kwa mujibu wa sheria pakiti zote zilizokutwa na dawa hizo za kulevya na mali zilizotumika kufanikisha kosa ikiwemo pikipiki, simu na fedha zitaifishwe na Serikali.

Related Posts